Sancho akubali sharti zito ili atue Borussia Dortmund
Muktasari:
- Winga huyo wa kimataifa wa England mwenye umri wa miaka 25, msimu uliopita alicheza kwa mkopo Chelsea ambapo alicheza mechi 42 za michuano yote.
JADON Sancho, ambaye ameachwa nje ya kikosi cha Manchester United ambacho kinaendelea na maandalizi ya msimu mpya, yuko tayari kukubali kupunguziwa mshahara kwa asilimia 50 ili kurejea Borussia Dortmund ya Bundesliga katika dirisha hili.
Winga huyo wa kimataifa wa England mwenye umri wa miaka 25, msimu uliopita alicheza kwa mkopo Chelsea ambapo alicheza mechi 42 za michuano yote.
Kwa sasa mazungumzo baina ya Dortmund na wawakilishi wa Sancho yanaendelea na mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 25 ameonyesha kuwa tayari kujiunga nao.
Hata hivyo, moja ya sharti ambalo lilikuwa mezani ni Sancho kukubali kupunguziwa mshahara kwa kiasi kikubwa kwani timu hiyo haina uwezo wa kumpa Pauni 300,000 kwa wiki anayoipata kwa sasa OT.
Kwa sasa, Sancho analipwa Euro 16 milioni kwa mwaka akiwa Man United na Dortmund, ipo tayari kumpa mshahara wa takriban Euro 8 milioni kwa mwaka.
Hii itamweka katika kundi la wachezaji wanaolipwa pesa nyingi zaidi katika kikosi cha Dortmund, lakini si kile cha juu kabisa.
Iwapo uhamisho huu utafanyika, utakuwa ni mara ya tatu kwa Sancho kujiunga na Borussia Dortmund. Kipindi chake cha kwanza kilimuweka kwenye ramani ya soka duniani kuanzia mwaka 2017 hadi 2021 na kilimwezesha kupata uhamisho wa Euro 85 milioni kwenda Man United, kipindi chake cha pili ilikuwa kwa mkopo akitokea Man United ambako hakuwa anapata nafasi.
Alejandro Garnacho
WINGA wa Manchester United ambaye ni raia wa Argentina, Alejandro Garnacho, mwenye umri wa miaka 21, anatamani sana kujiunga na Chelsea katika dirisha hili. Garnacho ni mmoja kati ya mastaa waliopewa ruhusa ya kutafuta timu mpya za kujiunga nazo katika dirisha hili kwa sababu hawapo katika mipango ya kocha Ruben Amorim. Mkataba wa sasa wa Garnacho unatarajiwa kumalizika mwaka 2028, msimu uliopita alicheza mechi 58 za michuano yote.
Randal Kolo Muani
TOTTENHAM , Manchester United na Newcastle zinafuatilia kwa karibu mustakabali wa mshambuliaji wa Paris St-Germain, Randal Kolo Muani, mwenye umri wa miaka 26, baada ya mpango wake wa kujiunga na Juventus kukwama. Timu hizi zinahitaji sana huduma ya fundi huyu wa kimataifa wa Ufaransa ili kuboresha maeneo yao ya ushambuliaji. Mkataba wake wa sasa unatarajiwa kumalizika mwaka 2028.
Javi Guerra
VALENCIA iko karibu kufikia makubaliano ya kumsainisha mkataba mpya kiungo wao raia wa Hispania Javi Guerra, mwenye umri wa miaka 22, ambaye anawindwa sana na Manchester United na AC Milan katika dirisha hili. Guerra ambaye ni miongoni mwa wachezaji tegemeo katika kikosi cha kwanza cha Valencia, msimu uliopita alicheza mechi 38 za michuano yote. Mkataba wake unatarajiwa kumalizika mwaka 2027.
John Victor
WEST Ham imewasilisha ofa ya Euro 8 milioni kwa ajili ya kumsajili kipa wa Botafogo ambaye ni raia wa Brazil, John Victor, 29, ambaye anahitajika sana na Galatasaray, Everton na Manchester United baada ya kiwango bora alichoonyesha katika michuano ya Kombe la Dunia la Klabu. Mkataba wake wa sasa unatarajiwa kumalizika mwaka 2028. Kipa huyu anaonekana kuvutiwa sana na ofa ya kucheza Ligi Kuu England kwa msimu ujao.
Tyler Morton
OLYMPIQUE Lyon inataka kumsajili Tyler Morton, 22 wa LIverpool. Taarifa kutoka Sky Sports zimefichua kuwa wawakilishi wa Lyon wamewasili England kwa ajili ya kumalizia hatua ya mwisho ya mazungumzo kabla ya kumsajili staa huyo. Morton hakuwa anapata nafasi ya kucheza katika kikosi cha kwanza cha Liverpool na awali alihitaji kuondoka hata kwa mkopo. Msimu uliopita alicheza mechi 11 za michuano yote.
Kalvin Phillips
MANCHESTER City inawauza mastaa wake ambao ni kiungo Jack Grealish, 29, James McAtee, 22, Kalvin Phillips miaka 29, pamoja na kipa wa kimataifa wa Ujerumani, Stefan Ortega, 32 katika dirisha hili la majira haya ya kiangazi, iwapo itapata ofa nzuri.Tovuti ya The Athletic imethibisha kuwa City inatarajiwa kupata zaidi ya Pauni 100 milioni kiujumla.
David Moller Wolfe
BEKI wa kushoto wa AZ Alkmaar, David Moller Wolfe, 23, yuko safarini kwenda England kufanya vipimo vya afya kabla ya kukamilisha uhamisho wake wa kujiunga na Wolves. Skysports imefichua kuwa kila kitu kimefikiwa makubaliano na staa huyo atasaini mkataba kwa ada ya Pauni 12 milioni katika dirisha hili. Msimu uliopita alicheza mechi 47 akafunga mabao matatu na asisti nane.