Salah kabeba tuzo yake huko
Muktasari:
- Mo Salah alishinda pia tuzo ya Mchezaji Bora wa Mwaka wa Chama cha Waandishi wa Habari za Michezo England baada ya kuonyesha kiwango bora kwenye msimu, akifunga mabao 29 na asisti 19, huku akiisaidia Liverpool kubeba taji la Ligi Kuu England.
MANCHESTER, ENGLAND: SUPASTAA wa Liverpool, Mohamed Salah amekuwa mchezaji wa kwanza kushinda tuzo ya Mchezaji Bora wa Mwaka wa Chama cha Wanasoka wa kulipwa England mara tatu.
Mo Salah alishinda pia tuzo ya Mchezaji Bora wa Mwaka wa Chama cha Waandishi wa Habari za Michezo England baada ya kuonyesha kiwango bora kwenye msimu, akifunga mabao 29 na asisti 19, huku akiisaidia Liverpool kubeba taji la Ligi Kuu England.
Kiwango bora cha Salah kimemfanya pia kuingia kwenye Kikosi Bora cha Mwaka cha Wanasoka wa Kulipwa England, kilichotajwa kwenye sherehe hizo za tuzo zilizofanyika jijini Manchester. Liverpool imeingiza mastaa kadhaa kwenye tuzo hizo baada ya kubeba taji la ligi kwa tofauti ya pointi 10 dhidi ya Arsenal iliyomaliza kwenye nafasi ya pili kwa msimu wa tatu mfululizo. Pamoja na Mo Salah wachezaji wengine wa Liverpool waliotajwa ni Virgil van Dijk, Alexis Mac Allister na Ryan Gravenberch. Staa mpya wa miamba hiyo ya Anfield, Milos Kerkez, naye amejumuishwa, lakini uteuzi wake umekuja baada ya kufanya vizuri Bournemouth msimu uliopita. Arsenal nayo imewakilishwa vyema kwenye kikosi hicho, ambapo mabeki wake wawili wa kati, William Saliba na Gabriel wamepata nafasi ya kupenya kikosini baada ya msimu uliopita kuruhusu mabao 34 tu kwenye ligi na wataungana na kiungo wao Declan Rice, ambaye ameonyesha ubora mkubwa tangu aliponaswa na Arsenal akitokea West Ham kwa ada ya Pauni 105 milioni.
Alexander Isak, ambaye pia ametajwa kwenye kikosi hicho alikosekana kwenye sherehe za tuzo kutokana na sakata lake la uhamisho kwenda Liverpool akitaka kuachana na Newcastle, huku wakali wengine waliopata nafasi kwenye kikosi ni kipa wa Nottingham Forest, Matz Selz na straika wa miamba hiyo, Chris Wood, ambaye alifunga mabao 20 msimu uliopita.
Mo Salah ameshinda tuzo hiyo akiwashinda mastaa wengine, Bruno Fernandes, Isak, Cole Palmer, Rice na Mac Allister, wakati staa wa Arsenal na England, Alessia Russo, aliyeshinda tuzo hiyo ya PFA kwa upande wa wanawake. Staa wa Aston Villa, Morgan Rogers, alishinda tuzo ya PFA kwa upande wa Mchezaji Bora Kijana wa Mwaka kwenye Ligi Kuu England. Kikosi kamili cha PFA hiki hapa: Matz Selz (Nottingham Forest); Virgil van Dijk (Liverpool), Willam Saliba (Arsenal), Gabriel (Arsenal), Milos Kerkez (Liverpool*); Declan Rice (Arsenal), Alexis Mac Allister (Liverpool), Ryan Gravenberch (Liverpool); Mohamed Salah (Liverpool), Chris Wood (Forest), Alexander Isak (Newcastle).