Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Mchezaji akamatwa kwa tuhuma za kumuua mwenzake kwa sumu

Muktasari:

  • Mchezaji huyo, anayetajwa kwa jina la Marius, alikamatwa Jumanne, Septemba 1, baada ya kutuhumiwa kumpa kwa siri sumu mchezaji mwenzake, Philipp, mwenye umri wa miaka 30.

DRESDEN, UJERUMANI: Mchezaji wa soka mwenye umri wa miaka 35 amekamatwa kwa tuhuma za kumpa sumu mwenzake aliyefariki dunia, huku tukio hilo likitokea wiki mbili tu kabla ya marehemu kufunga ndoa.

Mchezaji huyo, anayetajwa kwa jina la Marius, alikamatwa Jumanne, Septemba 1, baada ya kutuhumiwa kumpa kwa siri sumu mchezaji mwenzake, Philipp, mwenye umri wa miaka 30.

Wote walikuwa wakiichezea klabu ya daraja la chini ya TuS Rockenberg na walikuwa kwenye safari ya kusherehekea kumalizika kwa msimu mjini Dresden, Ujerumani, wakati tukio hilo lilipotokea.

Philipp alianza kujisikia vibaya akiwa kwenye safari hiyo. Baada ya kurejea nyumbani, hali yake ilizidi kuwa mbaya ghafla na familia yake ikalazimika kuwaita wahudumu wa dharura.

Alikimbizwa hospitalini, lakini alifariki siku iliyofuata licha ya madaktari kujaribu kumuokoa.

Baadaye uchunguzi wa kitabibu ulibaini kuwa alifariki kutokana na kushindwa kufanya kazi kwa viungo vingi vya mwili kwa sababu ya sumu, kwa mujibu wa taarifa za NeedToKnow.

Awali, watu wa karibu na marehemu waliamini huenda alipata sumu kutokana na kula samaki, kwa sababu timu hiyo ilikula samaki wakati wa safari.

Hata hivyo, uchunguzi wa polisi ulipoendelea, Marius alianza kuhusishwa na kifo hicho.


‘ILIKUWA KISASI’

Mwendesha mashtaka mkuu, Thomas Hauburger, aliambia vyombo vya habari vya eneo hilo kwamba wachunguzi wanaamini tukio hilo huenda lilitokana na kisasi.

“Tunadhani hili lilikuwa tendo la kulipiza kisasi,” alisema Hauburger.

Kwa mujibu wa tetesi zilizoenea Rockenberg, wachezaji hao wawili walikuwa wamewahi kugombana kuhusu mwanamke mmoja.

Marius, ambaye kwa sasa anashikiliwa akisubiri kesi yake, bado hajatoa kauli yoyote kuhusu tuhuma zinazomkabili.


KLABU YASHTUKA

Baada ya taarifa za kukamatwa kwake kusambaa, mkuu wa kitengo cha soka cha TuS Rockenberg, Manuel Barufe, alisema klabu hiyo imeshtushwa na tukio hilo.

“Sote tumeshangaa na kushtuka. Hakuna mtu aliyetarajia jambo kama hili. Tunatumaini polisi wataweza kubaini kikamilifu kilichotokea,” alisema.

TuS Rockenberg pia ilitoa salamu za rambirambi baada ya kifo cha Philipp, ikimuelezea kama “rafiki, mpiganaji uwanjani na mtu mwenye moyo mkubwa.”

Familia yake nayo ilimkumbuka kwa kusema alikuwa mtu wa “kicheko cha sauti, vitendo vya upole na moyo mkubwa.”

Philipp alikuwa tayari amefunga ndoa ya kiserikali kabla ya tukio hilo linalodaiwa kutokea, lakini sherehe kubwa ya harusi yake ilipangwa kufanyika mwezi huu.