Sagna: Konsa ataipa Arsenal ubingwa wa Ulaya
Muktasari:
- Konsa, 28, alijiunga na Arsenal wiki iliyopita akitokea Aston Villa kwa ada ya Pauni milioni 51 na anaweza kuichezea timu hiyo kwa mara ya kwanza kesho Jumatatu dhidi ya klabu yake ya zamani, Aston Villa, kwenye Uwanja wa Villa Park.
LONDON, ENGLAND: GWIJI wa zamani wa Arsenal, Bacary Sagna anaamini usajili wa beki Ezri Konsa unaweza kuwa ni kipande kilichokuwa kinakosekana kwenye kikosi hicho ili kutimiza ndoto ya kutwaa Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Konsa, 28, alijiunga na Arsenal wiki iliyopita akitokea Aston Villa kwa ada ya Pauni milioni 51 na anaweza kuichezea timu hiyo kwa mara ya kwanza kesho Jumatatu dhidi ya klabu yake ya zamani, Aston Villa, kwenye Uwanja wa Villa Park.
Ingawa usajili wa Konsa huenda usiwe na mvuto mkubwa ukilinganisha na majina makubwa ambayo Arsenal ilikuwa ikiyawania katika dirisha hili la usajili, Sagna anaamini ujio wake ulikuwa muhimu kwa kocha Mikel Arteta.
Arsenal ilitumia muda mwingi ikiwafuatilia nyota kama Vinicius Junior na Morgan Rogers, lakini ilihitaji kuimarisha safu yake ya ulinzi baada ya beki William Saliba kupata jeraha la mgongo linalotarajiwa kumweka nje kwa muda mrefu.
Konsa amesajiliwa kuziba pengo hilo na pia kuongeza ushindani mkali katika nafasi ya beki wa kati pindi Saliba atakaporejea.
Sagna, aliyefanya mechi 284 akiwa Arsenal kabla ya kuondoka mwaka 2014, anaamini ushindani huo ndani ya kikosi unaweza kuwa na mchango mkubwa katika safari ya Arsenal ya kutafuta mafanikio ya Ulaya.
Akizungumza na SunSport kupitia Action Network, Sagna, 43, amesema ili uwe mshindani, unahitaji kuwa na wachezaji wawili katika kila nafasi kwa sababu msimu ni mrefu.
“Haimaanishi kwamba kuna ushindani wa kugombania nafasi ndani ya kikosi. Kikosi hiki kina umoja na wachezaji wanaelewana vizuri.
“Lakini ili kuwa mshindani na kupata mafanikio, wachezaji wanapaswa kuelewa kwamba wanahitaji kuwa na mbadala.
“Kwa hiyo, yeyote anayecheza hapaswi kushusha kiwango cha timu. Kama Arsenal inataka kupiga hatua, kufikia ndoto yao ambayo bila shaka ni kutwaa Ligi ya Mabingwa, Konsa ni aina ya mchezaji unayehitaji kuwa naye.
“Unahitaji wachezaji wenye uwezo na mitindo tofauti. Kila nafasi lazima iwe na mtu wa kuicheza na Mikel Arteta anaelewa hilo.”
Arteta tayari amefanya usajili kadhaa katika dirisha hili, akiwaleta Christos Tzolis kutoka Club Brugge na Bruno Guimaraes kutoka Newcastle, huku bado akitafuta kuongeza nguvu katika safu ya ushambuliaji kabla ya kufungwa kwa dirisha la usajili Jumanne.
Hata hivyo, huenda Konsa akawa mmoja wa wachezaji muhimu zaidi katika usajili wa Arsenal msimu huu.
ULINZI NDIO SILAHA YA ARSENAL
Arsenal ilitegemea kwa kiasi kikubwa uimara wa safu yake ya ulinzi katika safari ya kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu England msimu uliopita, baada ya kusubiri miaka 22, na huenda ikahitaji kufanya hivyo tena msimu huu.
Arteta amejenga msingi wa timu yake kwenye safu imara ya ulinzi.
Ubora huo ulidhihirika wiki hii baada ya Saliba, Gabriel, Jurrien Timber na kipa David Raya kuchaguliwa katika Kikosi Bora cha Msimu cha Chama cha Wanasoka wa Kulipwa England (PFA).
Licha ya ubora huo, Konsa alikuwa bora kuliko mabeki wote wa Arsenal msimu uliopita katika kiwango cha kushinda mapambano ya mpira ardhini na mafanikio ya kukaba.
Pia, alikuwa miongoni mwa wachezaji muhimu wa England katika Kombe la Dunia la mwaka huu.
Mtindo wa Konsa wa kucheza kwa nguvu na kutokwepa mapambano umemfanya kuwa miongoni mwa mabeki bora wa Ligi Kuu England, jambo ambalo limemfanya Sagna kuamini atafanya vizuri Arsenal.
Sagna, ambaye pia aliwahi kuichezea Manchester City, amesema amejithibitisha akiwa Aston Villa na pia akiwa na timu ya taifa ya England.
“Nadhani alifanya vizuri kwenye mashindano na ni mzuri sana katika kumkabili mpinzani mmoja dhidi ya mmoja. Haogopi kukabiliana naye moja kwa moja.
“Ni mzuri katika mapambano na kushindana kwa nguvu. Hilo ndilo Arsenal inahitaji kwa sababu mara nyingi unapokuwa na mpira kwa muda mrefu, unaacha nafasi nyuma na kujikuta unahitaji beki anayeweza kumudu hali ya mmoja dhidi ya mmoja.
“Unahitaji mchezaji mwenye akili ya kulinda lango katika mazingira hayo, na Konsa ni mmoja wao.
“Kuwa na mpira na kutawala mchezo ni jambo moja, lakini kuweza pia kujilinda katika hali ya mmoja dhidi ya mmoja kama Saliba na Gabriel wanavyofanya, na Konsa anavyoweza kufanya, ni jambo muhimu kwa kikosi.”