Ruben Amorim akata tamaa Man United
Muktasari:
- Amorim amesisitiza kuwa bado ana imani kuwa anaweza kuubadilisha mwanzo mbaya wa Man United msimu huu baada ya kupoteza mechi tatu kati ya sita.
MANCHESTER, ENGLAND: KOCHA wa Manchester United, Ruben Amorim amesema hajali kama atafukuzwa kazi au atabaki kwa sababu huo sio uamuzi wake, lakini atafanya kadri awezavyo kuhakikisha timu hiyo inarudi katika mstari.
Amorim amesisitiza kuwa bado ana imani kuwa anaweza kuubadilisha mwanzo mbaya wa Man United msimu huu baada ya kupoteza mechi tatu kati ya sita.
Kipigo cha mabao 3-1 kutoka kwa Brentford kimemfanya Amorim kuwa na rekodi mbaya ya kukusanya pointi 34 katika mechi 33 ambayo hakuna kocha yoyote wa timu hiyo tangu kuondoka kwa Sir Alex Ferguson amewahi kuiweka.
"Mimi daima naamini katika kazi yangu. Sijali kuhusu kitakachoamuliwa kuhusu ajira yangu kwa sababu si uamuzi wangu. Mimi nitafanya kadri niwezavyo muda wote nitakaokuwa hapa. Sijawahi kuwa na wasiwasi kuhusu kazi yangu, mimi si mtu wa aina hiyo. Daima nafanya kazi yangu na nina imani kwa sababu najua nini cha kufanya.
"Najua tunaweza kucheza vizuri zaidi na tunahitaji kucheza vizuri zaidi, kwa sasa kinachotokea ni kama kupanda na kushuka. Tunaposhinda huwa inaonekana kila kitu kipo sawa, tukipoteza, tunarudi pale pale na inatulazimu kushinda mechi moja ili kurudi kwenye hali ya mwanzo, tunahitaji mwendelezo, wakati mwingine naona timu ikicheza vizuri sana lakini muda mwingine unacheza mechi ambazo unaona hakuna yale mambo mazuri ambayo yalikuwepo katika mechi ya nyuma.
"Hapo ndipo unapopata imani ya kusema kwamba Manchester United itarejea kwani kuna muda inaonekana kucheza vizuri na kupata matokeo, inachokosa ni muendelezo tu."
Amorim alisema pia alikasirishwa sana na mabao mawili ya mapema ya Igor Thiago ambayo aliwafundisha wachezaji wake mazoezini namna ya kuzuia kwa wiki nzima.
"Tulifanya kazi kwenye kila kitu kuhusu mechi hii. Kinachokera ni kwamba kila bao tuliloruhusu leo tulikuwa tumelifanyia kazi wiki nzima. Hatukuweza kucheza vile nilivyohitaji."
Katika mechi hiyo, straika wa Man United, Benjamin Sesko alifunga bao lake la kwanza akiwa na mashetani hao tangu aliposajiliwa kwa ajili ya msimu huu.
Kipigo hicho kiliishusha Man United hadi nafasi ya 14 ikiwa na pointi saba wakati Brentford ikisogea hadi nafasi ya 13, nayo pia ikiwa na alama saba.
Man United itakuwa na kibarua kigumu tena katika mechi ijayo ya ligi ambapo itakutana na Sunderland ambayo licha ya kupanda daraja msimu huu, imeonekana kuwa bora sana na sasa inashika nafasi ya nne ikiwa na pointi 11 ilizokusanya baada ya kushinda mechi tatu, sare mbili na kufungwa moja.
Baada ya mechi ya Sunderland ambayo itapigwa Oktoba 4 kwenye Uwanja wa Old Trafford, Man United itasafiri hadi Anfield kuvaana na Liverpol, Oktoba 19.
TANO ZIJAZO
Sunderland (H)
Liverpool (A)
Nottingham Forest (H)
Tottenham (A)
Everton (H)