Ronaldo apigwa faini ya sekunde 38
Muktasari:
- Kwa mujibu wa taarifa kutoka nchini Ureno, adhabu hiyo ya nahodha huyo mwenye umri wa miaka 41 imeanza kuhesabiwa kuanzia Septemba 30, siku inayohusishwa na mgogoro wake na benchi la ufundi la timu ya taifa.
LISBON, URENO: SUPASTAA wa soka duniani, Cristiano Ronaldo, amepigwa faini ya Pauni 215 (takriban Sh300,000), lakini hatakosa mchezo wowote wa timu ya taifa ya Ureno licha ya kupewa adhabu ya kufungiwa kwa mwezi mmoja.
Kwa mujibu wa taarifa kutoka nchini Ureno, adhabu hiyo ya nahodha huyo mwenye umri wa miaka 41 imeanza kuhesabiwa kuanzia Septemba 30, siku inayohusishwa na mgogoro wake na benchi la ufundi la timu ya taifa.
Hali hiyo inamaanisha kuwa adhabu yake itakuwa imekamilika kabla ya Ureno kucheza mchezo wake unaofuata dhidi ya Denmark, Novemba 14, hivyo Ronaldo atakuwa huru kurejea uwanjani iwapo ataitwa kikosini.
Kinachovutia zaidi ni kiasi cha faini alichotozwa nyota huyo wa Al-Nassr ya Saudi Arabia, ambaye anaripotiwa kulipwa takribani Pauni 488,000 kwa siku (takriban Sh 1.2 bilioni. Kwa hesabu hizo, Ronaldo anahitaji sekunde 38 tu kurejesha fedha alizotozwa kama faini kupitia mshahara wake.
CHANZO CHA MGOGORO
Mgogoro huo ulizuka baada ya Ronaldo kutoridhishwa na uamuzi wa kocha Jorge Jesus wa kutomtumia katika mchezo wa Ligi ya Mataifa dhidi ya Norway, Septemba 27, 2026 licha ya kumtaka afanye mazoezi ya kupasha mwili joto.
Ilikuwa mara ya kwanza katika kipindi chake cha miaka 18 akiichezea timu ya taifa ya Ureno kukaa benchi bila kuingia uwanjani.
Uamuzi huo ulimkera mshindi huyo mara tano wa tuzo ya Ballon d'Or, ambaye alidai kuwa kocha huyo alivunja ahadi ya kumtumia kwa dakika 30 dhidi ya Norway.
Ronaldo pia alidai Jesus alipaswa kuomba radhi kwa wananchi wa Ureno na wachezaji wenzake kwa kutompa nafasi ya kucheza, hasa baada ya kuwepo kwa mazungumzo yaliyohusisha mustakabali wake katika timu ya taifa.
Baada ya tukio hilo, Ronaldo aliripotiwa kukosa vikao vitatu vya mazoezi na kuondoka kambini kabla ya michezo miwili iliyofuata ya mapumziko ya kimataifa. Aliondoka kwa ndege binafsi kuelekea Hispania akiwa na familia yake, huku akiwa mbali na kikosi wakati wa maandalizi na mchezo uliofuata.
RONALDO ALIMPA PRESHA JESUS
Katika hatua nyingine, Ronaldo alitoa tamko refu la maneno 1,996 akimshutumu Jesus kwa kutotekeleza ahadi walizokuwa wamekubaliana kuhusu nafasi yake uwanjani.
Kwa mujibu wa taarifa hizo, Ronaldo alitaka kocha huyo akiri kuwa alifanya makosa kumtaka ajipashe moto kisha asimwingize uwanjani, akilinganisha hali hiyo na namna ambavyo wachezaji wakubwa wa kihistoria kama Pele na Diego Maradona wangepaswa kuheshimiwa.
Jesus alikiri kuwa huenda alikosea katika namna alivyomshughulikia Ronaldo, hasa kumtaka apashe moto mapema, lakini alisisitiza kuwa maamuzi ya nani acheze ni jukumu lake kama kocha.
Akieleza upande wake, Jesus amesema hakuwa amepanga kumtumia Ronaldo katika michezo hiyo miwili, ingawa wakati wa mchezo dhidi ya Norway aliona uwezekano wa kumhitaji na hivyo kumtaka ajiandae.
Jesus amesema Ronaldo alikubali kufanya hivyo, lakini mabadiliko ya mchezo yakamfanya abadili uamuzi na hatimaye kutomtumia.
JESUS BADO ANAMTAKA RONALDO
Licha ya mvutano huo, Jesus amekuwa akisisitiza kuwa hana kinyongo na Ronaldo na kwamba mlango wa timu ya taifa bado uko wazi kwa nahodha huyo.
Kocha huyo amesema mustakabali wa Ronaldo ndani ya timu ya taifa unategemea uamuzi wa mchezaji mwenyewe, ikiwa ataendelea kucheza katika kiwango kinachohitajika na kutamani kuitumikia nchi yake.
Jesus pia aliwahi kumtaja Ronaldo kama alama muhimu ya Ureno, akisisitiza kuwa heshima anayopata kutokana na historia yake haiwezi kupuuzwa.
Kauli hiyo imeungwa mkono hadharani na baadhi ya wachezaji wenzake, ambao wameonyesha kuwa bado wanamkaribisha nyota huyo kurejea kikosini.
Jesus alieleza kuwa mgogoro huo ulitokana na kutokuelewana na kwamba suluhu inaweza kupatikana kupitia mazungumzo kati ya pande hizo mbili.
URENO YANUFAIKA
Wakati Ronaldo akipambana na hali hiyo nje ya uwanja, Jesus amekuwa na mwanzo mzuri tangu achukue jukumu la kuinoa Ureno, akishinda michezo yake minne ya kwanza akiwa kocha mkuu, kwa mujibu wa taarifa zilizotolewa.
Matokeo hayo yamezua mjadala kuhusu namna timu hiyo inavyoweza kufanya vizuri zaidi kwa kutumia mfumo wenye uwiano mzuri wa wachezaji, huku Ronaldo akiwa sehemu ya mipango hiyo au akiwa nje ya kikosi.
Hata hivyo, licha ya mvutano huo, Jesus hajaonyesha nia ya kumfungia kabisa Ronaldo nje ya timu ya taifa.
Kwa sasa, kinachoonekana ni kuwa Ronaldo ameepuka adhabu itakayomnyima nafasi ya kucheza mechi zijazo, huku faini ya pauni 215 ikiwa kiasi kidogo ikilinganishwa na mapato yake ya kila siku.