Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Ronaldo aanza mambo Ureno akiandika rekodi mpya Kombe la Dunia

Muktasari:

  • Mabao mawili aliyoifungia timu hiyo katika ushindi wa 5-0 dhidi ya Uzbekistan, yamemfanya kuandika rekodi mpya ya mchezaji wa kwanza wa kiume kufunga katika fainali sita tofauti za Kombe la Dunia kuanzia mwaka 2006, 2010, 2014, 2018, 2022 na 2026.

TEXAS, MAREKANI: UMRI ni namba tu. Ndivyo unavyoweza kusema kwa mshambuliaji wa timu ya taifa ya Ureno, Cristiano Ronaldo baada ya leo kuandika rekodi mpya katika Fainali za Kombe la Dunia.

Mabao mawili aliyoifungia timu hiyo katika ushindi wa 5-0 dhidi ya Uzbekistan, yamemfanya kuandika rekodi mpya ya mchezaji wa kwanza wa kiume kufunga katika fainali sita tofauti za Kombe la Dunia kuanzia mwaka 2006, 2010, 2014, 2018, 2022 na 2026.

Katika mechi ya leo ya kundi K iliyopigwa kwenye Uwanja wa NRG uliopo mji wa Houston jimbo la Texas, Marekani, ilimchukua Ronaldo dakika sita tu kuandika rekodi hiyo baada ya kuifungia Ureno bao la utangulizi akimalizia kazi nzuri iliyofanywa na beki wa kulia wa kikosi hicho, Joao Cancelo.

Dakika ya 17, beki wa timu hiyo, Nuno Mendes akaifungia Ureno bao la pili kwa Frii-Kiki kali iliyomshinda kipa wa Uzbekistan, Abduvohid Nematov na kikosi hicho kuanza vyema baada ya mechi ya kwanza kushindwa kutamba kikitoka 1-1 dhidi ya DR Congo.

Uzbekistan ikajibu mapigo hayo na dakika ya 29, kiungo wa timu hiyo, Azizjon Ganiev aliifungia bao ingawa baada ya usaidizi wa mwamuzi wa video (VAR), lilikataliwa kutokana na madhambi yaliyofanyika wakati wa shambulizi lililopatikana kwa bao hilo.

Ronaldo akaiandikia Ureno bao la tatu na la pili kwake dakika ya 39, akimalizia pasi ya kiungo wa timu hiyo, Bruno Fernandes na kufikisha jumla ya mabao 10, ya Kombe la Dunia na kuandika rekodi mpya kwa taifa hilo.

Bao hilo la pili la Ronaldo limemfanya kufikisha mabao 10 katika Kombe la Dunia akiwa na timu ya taifa ya Ureno na kuwa mfungaji bora wa muda wote wa taifa hilo, baada ya kuivunja rekodi iliyokuwa inashikiliwa na aliyekuwa nyota wa kikosi hicho, Eusebio da Silva Ferreira aliyefunga tisa katika fainali za Kombe la Dunia mwaka 1966 nchini England.

Kipindi cha pili kilianza kwa Ureno pia kutawala mechi na dakika ya 60, ikapata bao la nne la kujifunga la kipa wa Uzbekistan, Abduvohid Nematov katika harakati za kuokoa shambulizi la kona.

Dakika ya 87, Rafael Leao akaiandikia Ureno bao la tano na kuihakikishia ushindi mkubwa timu hiyo inayosaka taji la kwanza la Kombe la Dunia katika historia ya taifa hilo tangu lilipoanza kushiriki mwaka 1966.

Ureno ilianza Fainali za Kombe la Dunia 2026 kwa kulazimishwa sare ya kufungana bao 1-1 dhidi ya DR Congo, Juni 17, 2026, huku kwa upande wa Uzbekistan ikianza vibaya baada ya timu hiyo kuchapwa mabao 3-1 na Colombia, Juni 18, 2026.

Matokeo ya leo yanaifanya Ureno kuongoza kundi K na pointi zake nne, nyuma yake kuna Colombia yenye tatu wakati DR Congo ina moja, huku Uzbekistan ikiburuza mkiani baada ya kuchapwa mechi zote mbili za hatua ya makundi.

Timu ya taifa ya Ureno imekuwa na historia mbalimbali nzuri katika Fainali za Kombe la Dunia, ingawa haijawahi kuchukua taji hilo, licha ya kushiriki kwake mara tisa ambazo ni mwaka 1966, 1986, 2002, 2006, 2010, 2014, 2018, 2022 na sasa 2026.

Ushiriki wa kwanza wa fainali za mwaka 1966 huko England, Ureno ilipata mafanikio makubwa kwa kumaliza nafasi ya tatu baada ya kuifunga Umoja wa Kisovieti (USSR) mabao 2-1, mechi iliyopigwa kwenye Uwanja wa Goodison Park, Julai 28, 1966.

Mafanikio mengine ni kufika nusu fainali Kombe la Dunia mwaka 2006, zilizofanyika Ujerumani, ambapo Ureno ilichapwa na Ufaransa bao 1-0 kwa penalti ya dakika ya 13, ya Zinedine Zidane, kwenye mechi iliyopigwa Allianz Arena, Julai 5, 2006.

Pia, Ureno ilifika robo fainali ya Kombe la Dunia mwaka 2022, zilizofanyika Qatar ambapo kikosi hicho kilichapwa bao 1-0 na Morocco, mfungaji akiwa Youssef En-Nesyri dakika ya 42, mechi iliyopigwa kwenye Uwanja wa Al Thumama, Desemba 10, 2022.

Kwa upande wa Uzbekistan inacheza kwa mara ya kwanza Kombe la Dunia mwaka 2026, tangu taifa hilo lilipojitenga baada ya kuvunjika kwa Umoja wa Kisovieti mwaka 1991, huku timu hiyo ikibeba matumaini makubwa kwa mashabiki wa kikosi hicho licha ya ugeni wao.

Timu hiyo maarufu kwa jina la 'White Wolves' (Mbwa Mwitu Weupe), iliandika rekodi mpya ya kufuzu Kombe la Dunia, Juni 5, 2025, baada ya suluhu (0-0) dhidi ya Falme za Kiarabu (UAE), ikishinda mechi 10, sare tano na kupoteza moja kati ya 16.

Uzbekistan inafundishwa na Kocha, Fabio Cannavaro aliyekuwa nahodha aliyeshinda Kombe la Dunia mwaka 2006, akiwa na Italia, akipewa jukumu hilo kubwa ili kuleta uzoefu katika timu hiyo inayoshiriki mashindano hayo kwa mara ya kwanza.

Kabla ya Cannavaro kuteuliwa Oktoba 6, 2025, timu hiyo ilianza kampeni za kuisaka tiketi ya kufuzu Kombe la Dunia kwa kufundishwa na makocha wawili akianza, Srecko Katanec, kisha Timur Kapadze aliyeondoka pia na kumwachia mikoba Muitaliano huyo.

Uwepo wa makocha hao wawili ambao ni Srecko Katanec na Timur Kapadze ulichangia kwa kiasi kikubwa mafanikio ya kikosi hicho kiujumla, ambapo kimefuzu Kombe la Dunia 2026, baada ya kumaliza nafasi ya pili hatua ya makundi nyuma ya Iran. 

Licha ya uchanga wa timu hiyo katika michuano ya Kombe la Dunia, ila miongoni mwa wachezaji wenye majina makubwa kwa taifa hilo ni nahodha, Eldor Shomurodov aliyechangia mabao tisa ya kikosi hicho hatua ya kufuzu akiwa ndiye muhimili kikosini.

Mbali na Shomurodov anayeichezea Klabu ya Istanbul Basaksehir ya Uturuki kutegemewa katika ushambuliaji, ila nyota wa Manchester City ya England, Abdukodir Khusanov ni beki anayetegemewa kwenye eneo la safu ya kujilinda kikosini hapo.