Ronaldinho na mikasa ya mastaa waliokataa kuzeeka
Muktasari:
- Ronaldinho aliyewahi kung'ara Barcelona, AC Milan na Paris Saint-Germain alicheza mechi yake ya kwanza ya ushindani baada ya miaka 11, akiitumikia Ravenna ya Ligi Daraja la Tatu nchini Italia dhidi ya Forli, jana Jumapili, Novemba 15, 2026.
MILAN, ITALIA: KUREJEA kwa staa wa zamani wa Brazil, Ronaldinho, katika soka la ushindani akiwa na umri wa miaka 46, si jambo la kawaida katika michezo, lakini historia inaonyesha kuwa umri mkubwa haujawazuia baadhi ya wanamichezo kurejea au kuendelea kufanya makubwa baada ya wengi kudhani muda wao wa mafanikio umepita.
Ronaldinho aliyewahi kung'ara Barcelona, AC Milan na Paris Saint-Germain alicheza mechi yake ya kwanza ya ushindani baada ya miaka 11, akiitumikia Ravenna ya Ligi Daraja la Tatu nchini Italia dhidi ya Forli, jana Jumapili, Novemba 15, 2026.
Mchezaji huyo aliyestaafu rasmi mwaka 2018, alicheza mechi yake ya mwisho ya ushindani akiwa Fluminense ya Brazil Septemba 2015. Sasa anarejea akiwa na lengo la kuisaidia Ravenna, lakini pia ana ndoto binafsi ya kufikisha mabao 300 katika maisha yake ya soka, akiwa amefunga mabao 299.
Hamu ya mashabiki kumuona nyota huyo akirejea uwanjani imekuwa kubwa kiasi cha kituo cha televisheni cha Sky Sport Italia kuandaa matangazo maalumu ya mchezo huo, ambayo kwa kawaida huandaliwa kwa mechi kubwa za soka barani Ulaya.
Kituo hicho kitaweka studio maalumu pembeni mwa uwanja wa Stadio Bruno Benelli, nyumbani kwa Ravenna, ambapo mchambuzi wa masuala ya usajili, Gianluca Di Marzio, ataungana na wageni maalumu kuchambua mchezo huo.
Watangazaji Antonio Nucera na Lorenzo Minotti walitoa matangazo ya moja kwa moja ya pambano hilo la Serie C.
Mbali na matangazo hayo, Sky iliweka kamera maalumu iliyofuatilia kila hatua ya Ronaldinho, kuanzia mazoezini kabla ya mchezo hadi atakapoingia uwanjani.
Mtangazaji maarufu wa Italia, Fabio Caressa, pia alishiriki katika utangulizi maalumu wa mchezo huo, huku mashabiki nchini Uingereza wakipata nafasi ya kuutazama bure kupitia chaneli ya YouTube ya Sky Sports Football.
Akizungumza na kituo cha CBS, Ronaldinho alisema anafurahia kurejea uwanjani baada ya miaka 11, akieleza kuwa amekuwa akifanya mazoezi tofauti na yale aliyokuwa akiyazoea awali.
“Nina furaha kubwa kurejea baada ya miaka 11. Ravenna ni klabu kubwa na nina shauku kubwa. Kwa sasa nafanya mazoezi mengi ya Footvolley. Nafanya mazoezi kwa mtindo tofauti na tutaona kitakachotokea,” alisema.
Hamu ya kumuona nyota huyo imeikumba pia jamii ya Ravenna, ambapo klabu hiyo imejenga jukwaa la muda lenye uwezo wa kuchukua mashabiki 1,800 na kulipa jina la R10 kwa heshima ya Ronaldinho.
Nyota huyo alichapisha video kwenye mitandao ya kijamii akionyesha umahiri wake wa kuchezea mpira, akiambatanisha na ujumbe uliosomeka: “Watu watasema hii ni akili mnemba (AI), haha!”
Jukwaa hilo jipya litaongeza uwezo wa uwanja huo kufikia mashabiki takribani 7,000, huku tiketi za mchezo huo zikiuzwa kwa bei ya hadi pauni 130.
Ronaldinho aliwasili Italia Ijumaa na kupokelewa kwa shangwe kubwa.
Rejea hiyo imeamsha kumbukumbu za wanamichezo wengine waliowahi kufanya uamuzi kama hayo, huku baadhi yao wakifanikiwa kurejesha makali yao na hata kuweka rekodi ambazo zimeendelea kuwa sehemu ya historia ya michezo duniani.
FOREMAN, BONDIA ALIYEVUNJA REKODI YA UMRI
Katika ndondi, jina la George Foreman haliwezi kukosekana katika mjadala wa wanamichezo waliorejea baada ya kustaafu na kufanikiwa.
Foreman alistaafu mwaka 1977 akiwa na miaka 28 baada ya kushindwa na Jimmy Young, lakini aliamua kurejea ulingoni mwaka 1987 akiwa na umri wa miaka 38.
Kilichofuatia kilikuwa historia kubwa zaidi ya maisha yake ya ndondi. Novemba 5, 1994, akiwa na miaka 45 na siku 299, Foreman alimtwanga Michael Moorer kwa KO raundi ya 10 na kutwaa ubingwa wa dunia wa uzito wa juu.
Ushindi huo ulimfanya kuwa bondia mwenye umri mkubwa zaidi kutwaa ubingwa mkubwa wa dunia wa uzito wa juu, rekodi inayotambuliwa na Guinness World Records.
Foreman alionyesha kuwa kurejea baada ya miaka mingi nje ya ulingo hakumaanishi kuwa mwanamichezo amepoteza kila kitu alichokuwa nacho, ingawa mafanikio yake yalihitaji maandalizi makubwa na nidhamu.
MIURA, MFANO WA UMRI KUTOKUWA KIKWAZO
Mfano mkubwa ni mshambuliaji wa Japan, Kazuyoshi Miura maarufu kama King Kazu, ambaye akiwa na miaka 59 bado anacheza soka la kulipwa.
Miura alijiunga na Fukushima United inayoshiriki Ligi Daraja la Tatu nchini Japan mwaka 2026. Julai mwaka huo aliandika historia nyingine kwa kufunga bao katika ushindi wa mabao 7-0 dhidi ya Iwaki Furukawa, ikiwa ni mara yake ya kwanza kufunga katika mechi ya ushindani baada ya takribani miaka minne.
Miura alianza maisha yake ya soka la kulipwa mwaka 1986 akiwa na Santos ya Brazil na amekuwa mfano wa mwanamichezo anayepambana na changamoto za umri. Tofauti na Ronaldinho, ambaye amerejea baada ya kustaafu, Miura amekuwa akiendelea kucheza kwa miongo kadhaa bila kukatiza rasmi maisha yake ya soka.
RIVALDO ALIVYOREJEA NA KUFUNGA
Mbrazil mwingine aliyewahi kufanya jambo linalofanana na Ronaldinho ni Rivaldo.
Baada ya kutangaza kustaafu mwaka 2014, Rivaldo alirejea uwanjani mwaka uliofuata akiwa na Mogi Mirim ya Brazil, klabu ambayo pia aliwahi kuhusishwa na umiliki wake.
Kilichofanya kurejea kwake kuwa na mvuto zaidi ni kwamba alicheza pamoja na mwanawe, Rivaldinho, katika mchezo dhidi ya Macae mwaka 2015. Wote wawili walifunga mabao katika ushindi wa mabao 3-1.
Huo ulikuwa mfano wa kipekee wa baba na mwana kucheza pamoja na kufunga katika mchezo mmoja wa ushindani. Rivaldo aliendelea kucheza hadi mwaka 2015 akiwa na umri wa miaka 43.
HOPKINS ALIVYOTAWALA AKIWA NA MIAKA 46
Bondia mwingine ni Bernard Hopkins wa Marekani, ambaye aliendelea kufanya vizuri katika ndondi akiwa katika umri ambao mabondia wengi huwa wamestaafu.
Mei 2011, Hopkins alimshinda Jean Pascal na kutwaa ubingwa wa dunia wa WBC uzito wa light heavyweight akiwa na miaka 46 na miezi minne.
Ushindi huo ulimfanya avunje rekodi ya Foreman na kuwa bondia mwenye umri mkubwa zaidi kutwaa ubingwa mkubwa wa dunia wakati huo.
Kilichovutia zaidi ni namna alivyotumia uzoefu, mbinu za kujilinda na uwezo wa kudhibiti mapambano dhidi ya mpinzani aliyekuwa mdogo kwake kwa miaka 18.
Hopkins aliendelea na mapambano ya kulipwa hadi mwaka 2016 alipokuwa na miaka 51.
ZOFF, MALDINI NA ZANETTI
Katika soka la Ulaya, historia pia inawakumbuka wachezaji walioweza kucheza katika kiwango cha juu wakiwa na umri mkubwa.
Dino Zoff aliiongoza Italia kutwaa Kombe la Dunia mwaka 1982 akiwa na miaka 40, akiwa mmoja wa manahodha wenye umri mkubwa zaidi kuwahi kutwaa taji hilo.
Beki Paolo Maldini aliendelea kuitumikia AC Milan hadi mwaka 2009 alipokuwa na miaka 40, akimaliza maisha yake ya soka akiwa ameshinda mataji matano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Javier Zanetti naye aliendelea kucheza hadi alipokuwa na miaka 40, akiiongoza Inter Milan kutwaa mataji matatu makubwa katika msimu wa 2009/10, likiwamo Ligi ya Mabingwa Ulaya.
RONALDINHO ANATAFUTA NINI?
Kwa kuangalia mifano hiyo, kurejea kwa Ronaldinho kunaweza kuwa tukio kubwa katika historia ya soka, lakini mafanikio yake hayatapimwa kwa umaarufu aliokuwa nao pekee, bali pia mchango atakaoutoa ndani ya uwanja.
Tofauti na Miura ambaye ameendelea kucheza kwa muda mrefu, Ronaldinho amekaa nje ya soka la ushindani kwa takribani miaka 11. Hilo linafanya kurejea kwake kuwa na changamoto kubwa zaidi, hasa katika suala la utimamu wa mwili, kasi ya mchezo na uwezo wa kuhimili ushindani.
Pia, akiwa na miaka 46, hawezi kutarajiwa kucheza kwa kiwango kilekile alichokionyesha alipokuwa Barcelona, ambako alijenga jina kubwa kupitia ufundi, chenga, pasi na mabao yaliyomfanya kuwa miongoni mwa wachezaji waliopendwa zaidi duniani.
Hata hivyo, historia ya Foreman, Hopkins na Rivaldo inaonyesha kuwa kurejea baada ya kustaafu kunaweza kuzaa matunda, ingawa mafanikio hayo si jambo la uhakika kwa kila mwanamichezo.
Kwa Ronaldinho, kufikisha mabao 300 kutakuwa hatua nyingine ya kihistoria, lakini kubwa zaidi litakuwa kurejea kwake uwanjani na kuweza kuisaidia Ravenna katika malengo yake ya kupanda daraja.