Masai; Meneja, mchezaji mwenye vyeti uwanjani
Muktasari:
- Hii ni kutokana na kipaji alichonacho, uwezo na juhudi binafsi zinazotawaliwa na elimu ya uongozi wa soka alionao, lakini zaidi taaluma zake zinazomfanya kuishi maisha yoyote.
MWENYE mbili havai moja. Ni msemo unaoweza kutumia kuelezea majukumu anayofanya mchezaji wa Ken Gold, Charles Masai akitumika kuongoza na kucheza soka kwa wakati mmoja.
Hii ni kutokana na kipaji alichonacho, uwezo na juhudi binafsi zinazotawaliwa na elimu ya uongozi wa soka alionao, lakini zaidi taaluma zake zinazomfanya kuishi maisha yoyote.
Akiwa kikosi hicho alichotumikia kwa zaidi ya miaka mitano sasa, kiungo huyo anatumika kama Meneja wa timu lakini wakati huohuo ni mchezaji tegemeo uwanjani na majukumu yake ameyamudu vyema.
Katika mahojiano maalumu na Mwanaspoti, Masai mwenye shahada ya elimu amezungumza mengi na namna anavyomudu majukumu na mustakabali wa KenGold ambayo imepotea Ligi Kuu Bara kwa misimu miwili sasa.
Mkongwe kikosini
Masai huenda akawa moja ya wachezaji waandamizi na wakongwe kikosini kwani tangu ilipohamishiwa wilayani Chunya ikibadilishwa jina kutoka Gipco (Geita) kuitwa KenGold, nyota huyo yuko nayo.
Hata hivyo Masai alihama na timu hiyo ikiitwa awali Gipco iliyokuwa daraja la pili (kwa sasa First League), ambapo alihusika kuipandisha Championship na hatimaye Ligi Kuu.
Kiungo huyo anaeleza kuwa kuaminiwa na kufanya majukumu yake kwa uweledi ndio siyo siri ya kudumu muda mrefu kikosini humo akieleza kuwa maisha ni popote na hawezi kujizuia kufanya kazi pale anapopata kazi.
“Kimsingi ni kufanya kazi kwa uaminifu na kutimiza wajibu, waliniamini na mimi napambana kuonyesha uaminifu wangu, japokuwa maisha ni popote nikipata sehemu tukaelewana naaga hapa,” anasema mchezaji huyo.
ALIA NA LIBASSE
Nyota huyo anasema licha ya kutimiza ndoto yake ya kucheza Ligi Kuu, lakini tangu timu iliposhuka daraja misimu minne sasa, yapo mengi anayokumbuka na kutamani yajirudie.
Anasema miongoni mwa vitu anatamani kukutana navyo ni nyota wa Simba, Libasse Gueye ambaye anamvutia zaidi kwa namna anavyocheza, huku akiwataja mastaa wengine waliomkuna zaidi enzi akiwa Ligi Kuu.
“Katika ndoto zangu tangu nilipoanza kucheza soka la ushindani 2016, nilitamani sana kucheza Ligi Kuu, nashukuru Mungu nilifanikisha japokuwa hadi sasa natamani tena kurejea huko.€
“Wapo wachezaji wengi walinikosha sana na muda mwingine tulipokutana uwanjani tulipeana ushindani kama Erick Mwijage aliyekuwa Kagera Sugar (kwa sasa Yanga), Feisal Salum na Kelvin Yondan,”€ anasema.
TAALUMA MBILI
Pamoja na kutundikwa majukumu mengi, Masai anasema haimuumizi popote kwakuwa elimu aliyonayo inamuwezesha kumudu kazi anazopangiwa ikiwamo kipaji alichopewa na Mungu.
Anabainisha kuwa hadi sasa anayo shahada ya Elimu aliyopata Chuo Kikuu Jocuko kilichopo mkoani Kagera pamoja na taaluma ya uongozi na usimamizi wa michezo ‘Sports Management’.
Anasema kutokana na taaluma hizo pamoja na kipaji alicho nacho haikumpa tatizo lolote kwenye kucheza, huku akiongoza timu katika sehemu ya meneja na kwamba hiyo ilitokana na kufungiwa kusajili timu.
“Nina shahada ya elimu ya sekondari niliyoipata 2016, taaluma ya uongozi na usimamizi wa michezo na kipaji, hivyo baada ya timu kufungiwa kusajili msimu huu nikaamua kuingia uwanjani,” anasema.
“Nikiwa na wenzangu uwanjani naacha kofia ya uongozi nje nawapanga kama wenzangu na tunashirikiana, vinginevyo sipati tatizo lolote kwakuwa ninao uwezo na uzoefu wa soka.”
Anaeleza kuwa kwa sasa hafikirii sana kurudi kwenye taaluma ya ualimu badala yake anapambania kuendeleza kipaji chake ikiwamo kusimamia na kuongoza mpira, akizigomea Simba na Yanga kuzichezea akitaka kuziongoza.
KUHUSU KENGOLD
Mkongwe huyo kikosini anakiri mwenendo kutokuwa mzuri akieleza kuwa sababu kubwa za kukosa ligi kuu muda mrefu ni kutokana na usajili usiozingatia mahitaji akitoa matumaini msimu huu kufanya kweli.
Anasema kwa misimu miwili nyuma wamekuwa wakikosea kwenye usajili akieleza kuwa hata walipojaribu kufanya hivyo, walijikuta wamechelewa na kushindwa kufanikiwa kufikia malengo.
“Kuna muda tulipoteana ikatubidi kusajili wachezaji wenye uzoefu japokuwa tulikuwa tumeshachelewa, msimu huu nafasi ipo tukikazana kushinda mechi zilizobaki tunaweza kurudi tena,” anasema mchezaji huyo.
Anaeleza kuwa Ligi Kuu inahitaji akili nyingi na hesabu kubwa, ilhali Championship ikitumika nguvu akikiri kuwapo ugumu na ushindani katika michuano hiyo.
Anafafanua kuwa msimu huu timu hiyo imekuwa na wachezaji wengi chipukizi wanaojitafuta, akibainisha kuwa kutokana na kiu waliyonayo kufikia malengo, inawafanya kupambana kuipa matokeo mazuri.
“Msimu huu kikosi kimesheheni nyota wenye vipaji, chipuki na wanaojitafuta, kutokana na kiu ya wote kuhitaji mafanikio wanaonesha kujituma hali inayoipa mafanikio timu kwa ujumla,” anasema.
ATAKA TISA
Nyota huyo aliyewahi kuzichezea Namungo iliyomtambulisha rasmi kwenye ramani za soka, anasema kwa mechi sita nyuma hawakuwa na matokeo mazuri akieleza kuwa ni kutokana na kuwa ugenini michezo mfululizo.
Anasema kuvuna pointi mbili katika michezo sita si mwenendo mzuri, akieleza kuwa kwa sasa wanarejea nyumbani wilayani Chunya kucheza dakika 270 mfululizo akisisitiza kuwa hawataki kuacha kitu.
“Katika michezo sita, mitano tumekuwa ugenini tukavuna pointi mbili si matokeo mazuri kwa timu yenye malengo badala yake lazima tujitathimini kwenye michezo mitatu ijayo tujue tunatokaje,” anasema