WAKATI mashabiki wakiwatazama makipa wa Simba, Djibrilla Kassali na Yanga, Djigui Diarra wanaofanya vizuri, lakini takwimu zinaonyesha kuna wengine wanaofanya vizuri zaidi.
Ukimtoa Kassali wa Simba na Diarra ambao wana mashabiki wengi, takwimu zinaonyesha Chuma Mgeni wa Coastal Union ndiye kipa aliyeokoa michomo mingi langoni kwake katika mechi 10 zilizochezwa Ligi Kuu Bara hadi sasa.
Chuma ameingia kwenye mjadala huo kutokana na takwimu za michomo aliyozuia, akiongoza orodha ya makipa 10 waliowekwa kwenye uchambuzi huu akiwa na 26 katika mechi tisa alizocheza, akitumia dakika 798 langoni mwa Coastal Union.
Idadi hiyo inamfanya kuwa na wastani wa sevu 2.9 kwa kila mechi, takwimu zinazomuweka mbele ya makipa wenye majina makubwa zaidi katika ligi hiyo ikilinganishwa na Djigui Diarra wa Yanga mwenye tisa katika mechi tisa, wakati Kassali wa Simba akiwa nazo nne katika mechi nane.
Hiyo ina maana Chuma amefanya sevu karibu mara tatu ya Diarra na zaidi ya mara sita ya Kassali katika takwimu hizo. Hata hivyo, tofauti hiyo haimaanishi moja kwa moja kuwa Chuma ni kipa bora kuliko wote, bali inaonyesha namna ambavyo amekuwa akikutana na michomo mingi inayolazimu aingilie kati kuokoa lango lake. Hiyo ina maana kuwa pamoja na mabeki wake kufanya kazi lakini kipa huyo anafanya ziada. Katika mechi ambayo kipa huyo alifanya sevu nyingi ni ile na Yanga Agosti 20 ambapo Coastal iliichapa mabao 4-1 katika Uwanja wa KMC Complex.
Takwimu zinaonyesha kwenye mechi hiyo Yanga ilipiga mashuti 13 yaliyolenga lango huku Chuma akifanya sevu tisa kwenye mechi hiyo tano ilikuwa kipindi cha kwanza na nne dakika 45 za mwisho. Hii ina maana kwamba kama isingekuwa uimara wake na ubora wa kuokoa michomo hiyo ina maana kuwa Coastal walikuwa na asilimia kubwa ya kuruhusu mabao zaidi ya 10 kwenye mechi hiyo.
Sio hiyo tu hata kwenye mechi dhidi ya Simba iliyopigwa Agosti 27, 2026 Uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo ambapo Wekundu hao wa Msimbazi waliondoka na ushindi mwembamba wa bao 1-0 lililofungwa na beki Ismail Toure, kipa huyo alifanya sevu saba kwenye dakika 90 na kuinyima timu hiyo ushindi mnono. Mechi nyingine alizofanya sevu nyingi ni dhidi ya TRA United akiokoa michomo mitatu na kuiwezesha Coastal kuondoka na pointi moja nyumbani.
Christopher Nyakanda wa Polisi Tanzania amekusanya sevu 20 katika mechi 10 alizocheza, akifuatiwa na Suleiman Abraham wa Namungo mwenye saves 19 katika mechi 10. Nyakanda amefanya wastani wa sevu mbili kwa mchezo, wakati Abraham ana wastani wa 1.9.
Kwa takwimu hizo, Chuma bado anaongoza kwa wastani wa michomo aliyozuia kwa kila mechi, akionyesha tofauti ya karibu sevu moja kwa mchezo dhidi ya Nyakanda. Kila mmoja wana saves nne wakicheza dakika 900 kwenye mechi 10
Ramadhani Chalamanda (JKT) kwenye mechi 11 alizocheza amefanya saves 13 akiondoka na clean sheet tatu kwenye dakika 990.
Musa Mbisa wa Dodoma Jiji anayeongoza kwa kuwa na cleansheet sita hadi sasa naye amefanya sevu nane katika mechi nane, sawa na wastani wa moja kwa kila mechi. Lakini, Toba Kutisha wa Mbeya City ana saves nane katika mechi nane, huku Zuberi Masudi wa Azam FC akiwa na sita katika mechi sita. Kwa upande wa Daniel Mgore wa TRA, amefanya sevu nne katika mechi saba. Takwimu hizo zinaonyesha namna ambavyo makipa wanavyotofautiana katika idadi ya michomo wanayokutana nayo na uwezo wa kuizuia.
DIARRA, KASSALI WAKO WAPI?
Kwa upande wa timu kubwa, Diarra na Kassali wanaingia kwenye mjadala huu wakiwa na takwimu ambazo haziwafanyi kuwa vinara wa saves, lakini haziondoi mchango wao katika kuilinda milingoti mitatu ya timu. Diarra ana sevu tisa, amefungwa mabao matano na ana clean sheet tano katika mechi tisa. Kassali, kwa upande wake, ana sevu nne, amefungwa mabao manne na ana clean sheet tano katika mechi nane.
Hapa ndipo uchambuzi wa makipa unapohitaji kuangalia zaidi ya idadi ya saves. Kipa anaweza kuokoa michomo michache kwa sababu mabeki wake wanazuia mashambulizi mengi kabla hayajafika langoni, lakini pia anaweza kuwa na saves nyingi kwa sababu timu yake inaruhusu wapinzani kufika mara kwa mara katika eneo la hatari.
Kwa mfano, Chuma ana sevu 26, lakini pia amefungwa mabao 10 na ana clean sheets tatu. Diarra ana sevu tisa, amefungwa mabao matano na ana clean sheets tano. Hivyo, idadi kubwa ya sevu kwa Chuma inaonyesha kazi anayokutana nayo, huku takwimu za Diarra zikionyesha pia uwezo wa timu yake kuzuia mabao na namna mabeki wanavyomrahisishia kazi kabla ya washambuliaji kufika kwake.
Kwa kuangalia takwimu za jumla, Chuma amekuwa akifanya kazi kubwa ya kuzuia mipira inayolenga lango. Sevu 26 katika mechi tisa ni wastani unaomuweka juu ya makipa wengine waliotajwa, huku Nyakanda akiwa mpinzani wake wa karibu katika orodha hiyo. Lakini, kipimo cha ubora wa kipa hakipaswi kuishia kwenye michomo aliyozuia. Idadi ya mabao aliyofungwa, clean sheet, ubora wa maamuzi, namna anavyoshirikiana na mabeki na uwezo wa kudhibiti eneo lake ni sehemu nyingine muhimu za tathmini.