Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Utaamua mwenyewe kama Vinicius ni malaika au shetani

PAZIA Pict


INAJITOKEZA mara chache katika zama mpya. Katika dunia mpya. Mara ya mwisho tulisikia simulizi hii miaka 15 iliyopita. Nyakati zimekwenda wapi? Tayari tukio lililodaiwa Luis Suarez alimbagua Patrice Evra pale Merseyside dimba la Anfield limeshatimiza miaka 15 sasa hivi. Umri wa binti mkubwa au kijana mkubwa kwa sasa.


Jumanne usiku katikati ya dimba la Estadio da Luz, Vinicius Junior alidai aliisikia sauti kama ile ya Evra ikitoka katika mdomo wa Gianluca Pestrianni, kijana mdogo wa Kiargentina anayesaka maisha katika klabu ya Benfica. Tofauti ni Evra anadaiwa aliitwa 'mtu mweusi' na Suarez wakati Vinicius anadai aliitwa 'nyani' na Pestrianni. Anadai aliitwa Mono. Kwa Kihispaniola nyani ni Mono.


Joto lilikuwa kali baada ya tukio na mechi ikasimama kwa takribani dakika 10 kupisha joto lipoe. Kulikuwa na mgawanyiko wa hisia baada ya tukio lenyewe. Kwanza ni namna ambavyo Vinicius alishangilia bao lenyewe. Alishangilia kwa maudhi mbele ya mashabiki wa Benfica. Alipewa kadi ya njano kwa kosa hilo. Kwa mujibu wa kanuni zao wenyewe, mchezaji hapaswi kwenda kushangilia kwa maudhi mbele ya mashabiki wa timu pinzani.

PAZ 01
PAZ 05

Wazungu wanatafsiri mchezaji anaweza kusababisha vita kubwa uwanjani na kuletea maafa makubwa endapo atafanya kosa hilo. Emmanuel Adebayor aliwahi kufungiwa mechi mbili na kutozwa faini ya Pauni 5,000 za Kiingereza baada ya kukimbia umbali wa mita 40 kuwafuata mashabiki wa Arsenal walipo ili awakere baada ya kufunga bao dhidi yao. Muda mwingi mashabiki hao walikuwa wanamzomea yeye.

Baada ya kudai Vinicius alikuwa amebaguliwa na Pestrianni kulizuka zogo kubwa huku yeye mwenyewe akisusia mechi. Mwamuzi asingeweza kufanya lolote kwa Pestrianni kwa sababu ni jambo ambalo lilihitaji uchunguzi mkubwa nje ya uwanja. Kuna kitu Pestrianni alikuwa amesema huku akiwa amefunika shingo ya jezi yake. Hata wale wasomaji wa lugha ya mdomo watapata shida kujua ambacho Pestrianni alikisema kwa Vinicius.

Tukio limetugawanya. Vinicius anapata watetezi wengi kwa sababu ni mtu mweusi na limekuwa jambo la kawaida wachezaji weusi kufanyiwa vituko vingi vya ubaguzi. Kabla ya Evra kudai alibaguliwa na Suarez tayari kina Samuel Etoo waliwahi kutoka uwanjani kule Hispania akijaribu kukatisha mechi kwa sababu kama hii ya juzi ya Vinicius.

PAZ 02

Kule Italia 'Super' Mario Balotelli naye alijaribu kuondoka uwanjani baada ya kubaguliwa. Sio jambo jipya ingawa katika miaka ya karibuni linatokea mara chache. Zamani lilikuwa jambo la kawaida kwa akina John Barnes kutupiwa ndizi wakifananishwa na nyani. Siku hizi matukio haya yanakuja kila baada ya miaka kadhaa.

Kwa Vinicius utetezi wa Pestrianni unatia shaka kidogo. Anajaribu kubadili maneno lakini historia ya Waargentina inatia shaka katika ubaguzi dhidi ya watu weusi. Kuanzia miaka hiyo ya 1600, karne nyingi zilizopita inasemwa Waargentina walikuwa wanaua watu weusi. Hawakuwapenda na inadaiwa hili limerithishwa kwa vizazi na vizazi. Mpaka leo hakuna mtu mweusi ambaye amewahi kuchezea timu ya taifa ya Argentina.

Mataifa yote makubwa ya kandanda yameshuhudia watu weusi wakichezea timu zao za taifa. Brazil, Ujerumani, Uholanzi, Italia, England na mengineyo yameshuhudia watu weusi wakivaa jezi za nchi hizo lakini sio Argentina. Haijawahi kutokea na haionekani kama itatokea katika siku za karibuni. Nimepita katika ukurasa nyingi za wazungu huko majuu na wapo watu wengi ambao wanamuhukumu Pestrianni kwa sababu ni Muargentina.

PAZ 03

Tusubiri Uefa watagundua nini. Wakati tukisubiri tukumbuke kuna kundi jingine la watu ambalo linamtazama Vinicius vibaya. Halipo upande wa Vinicius. Siyo kwa sababu wana uhakika hakubaguliwa, hapana, bali kutokana na vitendo vyake vya maudhi vya mara kwa mara uwanjani. Kwa nini yeye ndiye mlengwa mkubwa wa matukio haya? Kwa nini yeye ndiye mlengwa mkubwa wa kuzomewa mara kwa mara?

Watu wanajiuliza. Kuna mastaa wangapi weusi ambao wanatamba kwa sasa lakini hawaandamwi sana na mashabiki? Kuanzia katika timu zake hadi kwingineko. Pale katika timu yake kuna akina Kylian Mbappe, Aurelian Tchouameni, Eduardo Camavinga. Mbona huwa hawalengwi sana kama ambavyo Vinicius amekuwa akilengwa mara kwa mara na mashabiki wa timu pinzani.

Nje ya timu yake kuna akina Sadio Mane, Bukayo Saka, Rafael Leao na wengine wengi. Mbona wamekuwa hawalengwi sana kama anavyolengwa yeye? Lakini hata mfalme wa soka duniani Pele ambaye alikuwa anatoka katika nchi ya Vinicius Brazil alikuwa ni mweusi. Licha ya kucheza katika zama za ubaguzi mkubwa lakini hatukumwona Pele akiingia katika harakati ambazo Vinicius ameziingia.

PAZ 04

Jibu ni inawezekana Vinicius ana shida. Ana Kipaji kikubwa lakini ana ukorofi mwingi dhidi ya wachezaji wa timu pinzani na mashabiki wa timu pinzani. Kule Hispania mara kadhaa amekuwa akiingia matatizoni na wachezaji wa timu pinzani. Dan Carjaval aliwahi kutuambia atakwenda kuongea na Vinicius kuhusu tabia zake lakini hadi leo hajatupa mrejesho yakinifu kuhusu mazungumzo yao.

Niliwahi kuandika humu kwamba Vinicius na Lamine Yamal wana shida. Makuzi yao ya ustaa ni tofauti na yale ambayo tulikuwa tunayaona kwa mastaa wawili wakubwa wanaokaribia kupita kwa sasa katika soka, Lionel Messi na Cristiano Ronaldo. Wao walikuwa wapole na ambao walikuwa busy na vipaji vyao. Na wao kwa wao pia hawakuwa na shida yoyote kati yao pindi walipokuwa wanakutana uwanjani.

Lakini ni katika El Clasico iliyopita tu Lamine Yamal na Vinicius wamegombana uwanjani wakitaka kutupiana ngumi. Ronaldo na Messi licha ya mashabiki wao kuingia katika vita vya mara kwa mara kuhusu nani ni bora zaidi kuliko mwenzake lakini wamekuwa wakiheshimiana pindi walipokutana kuanzia katika El Clasico hadi katika mechi za timu zao za taifa. Vinicius na Lamine wanaonekana kutofuata nyayo.

Wakati mwingine inakuwa ngumu kusimama nyuma ya Vinicius katika jambo hili kwa sababu ya tabia zake. Hata katika mechi hii hii tulimuona Nicolas Otamendi akimuonyesha kwa dharau Vinicius tattoo za mataji aliyoshinda katika soka ikiwemo kombe la dunia. Inadaiwa Vinicius alimwambia Otamendi ana sura mbaya.

PAZ 05

Utaamua mwenyewe Vinicius ni malaika au shetani. Na kilichonishangaza kingine katika ugomvi wake na Pestrianni ni ukweli kwa miaka mingi wachezaji wa Brazil na Argentina licha ya kuwa na uhasama katika mataifa yao ya Amerika Kusini lakini wamekuwa hawana shida kabisa wakikutana. Wengi kati yao wamecheza timu moja au tofauti lakini wamekuwa marafiki wakubwa.

Diego Maradona na Careca walikuwa marafiki wakubwa wakati wakicheza pamoja Napoli. Ronaldinho alimlea vyema Lionel Messi na alikuwa rafiki yake mkubwa kiasi kwamba alimsaidia Ronaldinho kiasi cha pesa wakati alipopata matatizo katika miaka ya karibuni. Messi pia alikuwa rafiki mkubwa wa Neymar kuanzia Barcelona hadi alipomfuata PSG.

Mifano ni mingi. Angel Di Maria na Marcelo ambao walicheza wote Santiago Bernabeu walikuwa marafiki wakubwa kama ambavyo ilikuwa kwa Ricardo Kaka na Gonzalo Higuain. Tatizo la Vinicius na Pestrianni wala halitokani na upinzani wa kimpira uliopo baina ya Brazil na Argentina kule Amerika Kusini. Labda ni tatizo lao wenyewe tu la ghafla ambalo limetokea uwanjani.

Mwishowe utaamua mwenyewe kama ni malaika au shetani katika tukio lililomtokea. Kuna upande mkubwa unaweza kumtetea ingawa wakati mwingine tabia zake binafsi zinatia shaka. Fikiria hata mtu mweusi Rio Ferdinand amekaririwa akidai Vinicius alikuwa chanzo cha yote ambayo yalitokea Jumanne usiku pale Estadio Da Luz.