Rodrygo afanya uamuzi dili la England, Saudia
Muktasari:
- Rodrygo, ambaye alikuwa na msimu mzuri wa 2024/25, alifunga jumla ya mabao 17 na kutoa assisti nane katika michuano yote, alikuwa akihusishwa kuondoka bara baada ya Xabi Alonso kuwa kocha wa Madrid.
Winga wa kimataifa wa Brazil, Rodrygo,24, imeripotiwa kufanya uamuzi wa kubaki Real Madrid, licha ya kuvutiwa na ofa nono kutoka klabu za Ligi Kuu England kama Arsenal, Liverpool na Tottenham Hotspur, pamoja na miamba ya Ujerumani Bayern Munich.
Rodrygo, ambaye alikuwa na msimu mzuri wa 2024/25, alifunga jumla ya mabao 17 na kutoa assisti nane katika michuano yote, alikuwa akihusishwa kuondoka bara baada ya Xabi Alonso kuwa kocha wa Madrid.
Kwa mujibu wa ripoti kutoka Hispania, Rodrygo alifanya mazungumzo ya ana kwa ana na kocha mpya wa Real Madrid, Xabi Alonso, aliyerithi mikoba ya Carlo Ancelotti aliyechukua majukumu ya timu ya taifa ya Brazil.
Katika mazungumzo hayo, Xabi alimhakikishia atakuwa sehemu muhimu ya kikosi chake kipya na atatumika kama winga wa kulia au mchezaji huru nyuma ya mshambuliaji.
Rodrygo, aliyesajiliwa kutoka Santos mwaka 2019 kwa Euro 45 milioni, alionekana kuwa na mashaka kuhusu nafasi yake kikosini baada ya ujio wa nyota Kylian Mbappe na kuibuka kwa Endrick, lakini sasa inaelezwa amejihakikishia nafasi yake msimu ujao.
Klabu kama Arsenal ilikuwa tayari kutoa takriban Euro 90 milioni, huku Liverpool nao wakimtazama kama mbadala wa muda mrefu wa Mohamed Salah iwapo atatimkia Saudi Arabia.
Aidha, Bayern Munich ilikuwa tayari kuanzisha mazungumzo ya awali na mawakala wa Rodrygo, lakini sasa mpango huo unaonekana kufa rasmi kutokana na uamuzi wake wa kuendelea kubaki Santiago Bernabeu.
Marc Guehi
NEWCASTLE United inajiandaa kuwasilisha tena ofa ya Pauni 40 milioni Crystal Palace ili kumnunua beki wa kati wa klabu hiyo na timu ya taifa ya England, Marc Guehi dirisha hili. Hata hivyo, Palace inahitaji kiasi kisichopungua Pauni 50 milioni ili kumuuza Guehi,25, aliyeonyesha ubora mkubwa tangu ajiunge na Palace mwaka 2021, na tayari amecheza mechi zaidi ya 100 akiwa na timu hiyo. Newcastle inahitaji kuimarisha safu yake ya ulinzi.
Ross Barkley
KOCHA wa Everton, David Moyes anapanga kusajili wachezaji wapya wasiopungua sita ili kuimarisha kikosi chake na miongoni mwa wachezaji hao, wawili watakuwa ni viungo wa kati na wawili watakuwa mawinga. Everton iliepuka kushuka daraja kwa taabu msimu uliopita na sasa inataka kujenga kikosi thabiti kitakachoweza kupambana kumaliza nafasi za juu zaidi. Hadi sasa tayari imemsajili kwa mkopo kiungo wao wa zamani Ross Barkley.
Marc Casado
TOTTENHAM Hotspur imeambiwa ili impate kiungo Mhispania, Marc Casado, 21 kutoka Barcelona, ni lazima ilipe Euro 30 milioni kama ada ya uhamisho. Casado kwa sasa ni nahodha wa kikosi cha pili cha Barcelona na tayari ameanza kuingia katika mipango ya timu ya wakubwa. Spurs inamtazama kama mbadala wa muda mrefu wa kiungo wao Pierre-Emile Hijbjerg anayetajwa ataondoka mwisho wa msimu.
Arnau Martinez
CRYSTAL Palace inapambana sana kuhakikisha inampata beki wa kulia wa Girona na timu ya taifa ya vijana ya Hispania, Arnau Martinez, 22, lakini inakumbana na ushindani mkubwa kutoka kwa Juventus ya Italia. Martinez ni miongoni mwa mabeki waliotoa pasi nyingi za mabao (sita) ndani ya La Liga msimu uliopita. Palace inamtazama kama mrithi wa Joel Ward.
Jens Cajuste
KIUNGO wa kati wa Napoli, Jens Cajuste inaripotiwa kuwa karibu kurejea England kujiunga na Ipswich Town na amekataa ofa za Burnley na klabu kutoka Saudi Arabia. Cajuste alihusishwa na uhamisho kwenda Mashariki ya Kati, lakini anaonekana kupendelea kucheza ligi ya ushindani kama EPL. Staa huyu mwenye umri wa miaka 25, amekubali ofa ya Ipswich ambayo itampa mshahara wa Pauni 80000 kwa wiki.
Fabio Vieira
STUTTGART ya Ujerumani ipo katika mazungumzo na Arsenal ili kumsajili kiungo mshambuliaji wa klabu hiyo Fabio Vieira 25, katika dirisha hili. Vieira hajapata nafasi kubwa ya kucheza katika kikosi cha kwanza cha Arsenal a kutosha tangu ajiunge nao mwaka 2022 akitokea FC Porto. Katika msimu uliopita alicheza mechi 18 tu EPL na kufunga bao moja pekee.
Jakub Kiwior
MABOSI wa FC Porto walikuwa na nia ya kumsajili beki wa kati wa Arsenal, Jakub Kiwior dirisha hili, lakini wameamua kujiondoa kwenye dili hilo baada ya Arsenal kutaka ada ya uhamisho ya Euro 30 milioni. Fundi huyu kimataifa wa Poland anataka kuondoka dirisha hili ili kujiunga na timu itakayompa nafasi kubwa ya kucheza.