Robo fainali CAFCL moto utawaka
Muktasari:
- Michuano hii mikubwa Afrika imekuwa ikifuatiliwa na mashabiki wengi kutoka nje na ndani ya bara hili, kwa hapa nchini msimu huu zilishiriki Simba na Yanga ambazo zote kwa pamoja zilitupwa nje kwenye hatua ya makundi.
RABAT, MOROCCO: MICHUANO ya Ligi ya Mabingwa Afrika hatua ya robo fainali inafikia tamati yake leo na kesho kwa kupigwa michezo yenye hadhi kubwa kwenye soka la Afrika.
Michuano hii mikubwa Afrika imekuwa ikifuatiliwa na mashabiki wengi kutoka nje na ndani ya bara hili, kwa hapa nchini msimu huu zilishiriki Simba na Yanga ambazo zote kwa pamoja zilitupwa nje kwenye hatua ya makundi.
Mechi za kwanza za hatua ya robo fainali zilipigwa wiki moja iliyopita na mashabiki wakashuhudia michezo ya kuvutia kwa timu zote nane ambazo zilitinga kwenye hatua hii muhimu, huku sare zikitawala.
Mamelodi Soundowns pekee ndiyo inaonekana kuwa ina nafasi kubwa ya kutinga hatua ya robo fainali baada ya kushinda kwa ushindi mnono katika mchezo wa kwanza kwa kuichapa Stade Malien kwa mabao 3-0 kwenye mchezo wa kwanza ambao uliopigwa Uwanja wa Loftus Versfeld nchini Afrika Kusini, sasa timu hizo zitakuwa Mali kesho kumaliza biashara hiyo ambapo mshindi wa jumla atatinga nusu fainali kupambana na wababe wengine.
Al Ahly vs ES Tunis
Mchezo mkubwa ambao unasubiriwa kwa hamu leo jioni ni kati ya mabingwa wa kihistoria wa michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika Al Ahly watakapovaana na mabingwa wa Tunisia Esperence de Tunis nchini Misri kwenye mchezo ambao unasubiriwa kwa hamu kubwa baada ya mechi ya kwanza Al Ahly kulala kwa bao 1-0.
Kwa sasa Al Ahly imekuwa kwenye wakati mgumu katika Ligi Kuu ya Misri ikiwa nyuma ya Zamalek na Pyramids inafahamu kuwa kutakuwa na presha kubwa endapo itaondolewa kwenye michuano hii ikiwa nyumbani kutokana na kushindwa kuwa na makali kuanzia msimu huu umeanza.
Ahly imetwaa makombe 12 ya Ligi ya Mabingwa Afrika na leo itakuwa inavaana na timu inayoshika nafasi ya nne kwa kutwaa ubingwa huo baada ya kulitwaa mara nne, ikiwa msimu huu imeruhusu bao moja pekee katika michezo saba iliyopita kwenye mashindano yote.
Pyramids vs AS FAR
Mashabiki leo watakuwa tena wakiwatazama mabingwa watetezi wa kombe hilo Pyramids ambao watakuwa wakipambana kuona kama wanaweza kulitetea kombe lao watakapokuwa uwanjani kuvaana na AS FAR ya Morocco.
Pyramids wamekuwa kwenye msimu wa kupanda na kushuka na wanatarajiwa kuhakikisha kuwa wanaonyesha uwezo ili kuendeleza makali yao baada ya kulazimisha sare ya bao 1-1 kwenye mchezo wa kwanza ugenini, hivyo leo wapo sehemu yao ya kujidai kuhakikisha kuwa wanapata ushindi mbele ya wageni wao.
Pyramids ikiwa chini ya kocha Krunoslav Jurcic, imekuwa kwenye kasi ya hali ya juu kuhakikisha kuwa inapambana kwenye makombe yote makubwa msimu huu ikiwa nyuma ya Zamalek kwenye vita ya ubingwa wa Misri baada ya timu hizo kucheza michezo 20. Hata hivyo, wanakwenda kukutana na AS FAR ambao hadi sasa hawajapoteza mchezo kwenye michezo kumi iliyopita kwenye michuano yote.
Pamoja na mambo yote lakini timu hizo hazina historia kubwa kwenye mashindano haya kila moja ikiwa imetwaa ubingwa mara moja
Kesho
Baada ya michezo ya leo, kesho mashabiki wataitazama michezo mingine miwili ambao Al Hilal ambao makazi yao ni Rwanda watakuwa nyumbani kuvaana na RS Berkane baada ya mchezo wa kwanza kwa timu hizo kumalizika kwa sare ya bao 1-1.
Mashabiki wanasubiri kwa hamu kuona kama Al Hilal wataendeleza makali yao baada ya kumaliza kileleni kwenye makundi, picha ya mchezo wa kwanza inaonnyesha kuwa huu hii itakuwa kati ya mechi ngumu kwenye michuano hii. Mechi nyingine kali leo ni Mamelodi ambao watakuwa ugenini kuvaana na Stade Malien.