Barcola akubali kutua Liverpool
Muktasari:
- Endapo Barcola ataondoka kwenda Liverpool, mabingwa wa Ligue 1, PSG, wanaweza kujaribu kuipiku Real Madrid katika mbio za kumsajili winga wa Ivory Coast Yan Diomande (19) kutoka RB Leipzig.
MSHAMBULIAJI wa Paris Saint-Germain na timu ya taifa ya Ufaransa, Bradley Barcola (23), ameripotiwa kukubali kwa maneno kujiunga na Liverpool. Hata hivyo, uhamisho huo bado haujathibitishwa kutokana na tofauti kubwa ya makubaliano ya ada ya usajili kati ya klabu hizo mbili.
Endapo Barcola ataondoka kwenda Liverpool, mabingwa wa Ligue 1, PSG, wanaweza kujaribu kuipiku Real Madrid katika mbio za kumsajili winga wa Ivory Coast Yan Diomande (19) kutoka RB Leipzig.
Vita kubwa inaonekana kuongezeka katika usajili baina ya timu hizo mbili ambazo kila moja imeweka mtego, ingawa inadaiwa kwamba Barcola ameshaanza kusaka makazi jijini Liverpool mahali ambapo anaweza kwenda kuishi iwapo makubaliano yatafikiwa.
Kwa sasa Liverpool inapambana kusaka mshambuliaji anayeweza kwenda kuongeza kitu kwenye kikosi chake kufuatia kuondoka kwa Mohamed Salah mwishoni mwa msimu uliopita, ambapo pengo aliloliacha linaendelea kuwaumiza vichwa mabosi wa mabingwa hao wa zamani wa England.
Kwa upande wa Barcola, inadaiwa kwamba amechoshwa na namna mbinu za benchi la ufundi la PSG zinavyofanya kutokuwapo kwa mchezaji mwenye uhakika wa kuanza kikosini kila inapokuwa katika maandalizi ya mchezo, huku eneo analocheza la winga wa kushoto kukiwa na Desire Doue ambaye msimu uliopita alimpa wakati mgumu kocha Luis Enrique kufanya chaguo.
Bruno Guimaraes
VYANZO kutoka Newcastle United vinasisitiza kuwa klabu hiyo haifanyi mazungumzo na Arsenal kuhusu kumuuza nahodha wake, Bruno Guimaraes (28), ambapo inaelezwa kwamba kiungo huyo wa Brazil anatarajiwa kurejea mazoezini kesho, Ijumaa. Nyota huyo amekuwa akigonganisha vichwa makocha wa timu mbalimbali England katika dirisha hili la usajili Ulaya.
Luis Diaz
BAYERN Munich haina mpango wa kumuuza mshambuliaji wa kimataifa wa Colombia, Luis Diaz (29), licha ya kuhusishwa na Al-Hilal. Mchezaji huyo pia ameiambia klabu hiyo kuwa anataka kubaki Ujerumani, ingawa kambi yake inazingatia zaidi ofa ambazo zimekuwa zikiwasilishwa mezani tangu msimu uliopita na kwamba lolote linaweza kutokea kuanzia sasa.
Iliman Ndiaye
EVERTON inatarajia kudai takribani Pauni 70 milioni kwa ajili ya mauzo ya winga wa kimataifa wa Senegal, Iliman Ndiaye (26), anayewindwa na Manchester United pamoja na Al-Hilal. Hata hivyo, kiasi hicho cha fedha kinaweza kupungua iwapo mchezaji huyo hataonyesha utayari wa kutaka kuondoka katika kikosi hicho licha ya kutakiwa na timu kubwa.
Joshua Zirkzee
MANCHESTER United iko tayari kumruhusu mshambuliaji wa kimataifa wa Uholanzi, Joshua Zirkzee (25), kuondoka katika dirisha hili la usajili wa majira ya kiangazi, huku mazungumzo na Juventus kuhusu uhamisho wake yakiendelea. Mchezaji huyo amekuwa katikati ya mijadala inayoendelea Old Trafford ya ama abaki au apigwe bei kwani hajaonyesha maajabu tangu alipotua kikosini.
Ousmane Diomande
NOTTINGHAM Forest iko karibu kukamilisha usajili wa beki wa kati wa kimataifa wa Ivory Coast, Ousmane Diomande (22), kutoka Sporting Lisbon kwa ada ya Pauni 34 milioni. Diomande amekuwa akihusishwa na timu mbalimbali Ulaya kutokana na ubora aliouonyesha katika mashindano msimu uliopita. Mkataba wa mchezaji huyo Sporting unatarajiwa kumalizika Juni 30, 2030.
CarlRushworth
COVENTRY City inadaiwa kukubaliana na Brighton kumsajili kipa wa England, Carl Rushworth (25), kwa ada ya awali ya Pauni 22.5 milioni ambayo ni rekodi mpya ya usajili kwa klabu hiyo. Hata hivyo, Rushworth pia amekuwa akihushwa na Fulham, Watford na Ipswich katika dirisha hili la usajili kutokana na ubora aliouonyesha msimu uliopota kwenye Ligi Kuu England.
Takehiro Tomiyasu
BEKI wa zamani wa Arsenal, Takehiro Tomiyasu (27), kwa sasa anafanya mazoezi na Crystal Palace baada ya kuondoka Ajax msimu huu wa kiangazi. Hata hivyo, bado hakuna mazungumzo rasmi kuhusu kujiunga na klabu hiyo. Tomiyasu, raia wa Japan alikuwa na wakati mgumu katika kikosi hicho cha Uholanzi ambako hakupata muda mwingi wa kucheza, suala ambalo limemfanya aachwe.
Kalvin Phillips
KIUNGO wa Manchester City na England, Kalvin Phillips, anadaiwa kuwa katika hatua za mwisho za kukamilisha uhamisho wa mkopo kwenda Sheffield United inayoshiriki Championship, baada ya kuachwa kwenye kikosi cha ziara ya maandalizi ya msimu mpya. Phillips aliyeichezea Sheffield United msimu uliopita ameamua kubakia katika kikosi hicho kupambania namba kikosini.
Radek Vitek
MIDDLESBROUGH inadaiwa kuwa na mpango wa kumsajili kipa wa Manchester United, Radek Vitek, katika dirisha hili la usajili la majira ya kiangazi, baada ya kipa huyo mwenye umri wa miaka 22 raia wa Jamhuri ya Czech kutumia msimu uliopita kwa mkopo katika Klabu ya Bristol City. Hata hivyo, Bristol pia inadaiwa kutaka kubaki naye ingawa ni kwa mkopo wa mwaka mmoja.