Rice anusurika kadi nyekundu, mashabiki wacharuka
Muktasari:
- Arsenal ilipata kichapo chake cha kwanza katika mashindano yote msimu huu baada ya Brighton kuichapa mabao 3-0 kwenye Uwanja wa Amex, kupitia Pascal Gross, Babis Kostoulas na Chema Andres.
LONDON, ENGLAND: MASHABIKI wa Ligi Kuu England wameonyesha hasira baada ya kiungo wa Arsenal, Declan Rice, kuonyeshwa kadi ya njano pekee kufuatia tukio la kutatanisha la kumchezea vibaya Malick Yalcouye wa Brighton bila mpira.
Arsenal ilipata kichapo chake cha kwanza katika mashindano yote msimu huu baada ya Brighton kuichapa mabao 3-0 kwenye Uwanja wa Amex, kupitia Pascal Gross, Babis Kostoulas na Chema Andres.
Hata hivyo, mambo yangeweza kuwa mabaya zaidi kwa Arsenal katika muda wa nyongeza, baada ya Yalcouye, 20, kujaribu kuunyang'anya mpira Rice, 27, katika eneo la timu ya wageni.
Rice, raia wa England, alifanikiwa kuutoa mpira akiwa chini ya presha, lakini ilionekana Yalcouye alimsukuma muda mfupi baadaye.
Marudio ya video yanaonyesha Rice akimjibu kwa kumpiga teke la kisiri kiungo huyo wa kimataifa wa Ivory Coast, lililomwangusha chini katika dakika ya saba ya muda wa nyongeza.
Mwamuzi Darren England alisimamisha mchezo na kumuonyesha Rice kadi ya njano kwa kitendo chake cha kulipiza kisasi.
Hata hivyo, kiungo huyo wa Arsenal alionekana kuwa na bahati, kwani mashabiki wengi waliamini alistahili kuonyeshwa kadi nyekundu, wakimshambulia mwamuzi na mfumo wa VAR kupitia mitandao ya kijamii.
Shabiki mmoja aliandika kwenye mtandao wa X: “Inaonekana VAR ilikuwa kwenye mapumziko ya kunywa chai...”
Mwingine amesema: “Sielewi kwa nini hili halikuhesabiwa kama kitendo cha vurugu.”
Shabiki wa tatu akaandika: “Hiyo ni kadi nyekundu katika kila kiwango cha soka!”
Mwingine akasema: “Mpe kadi hiyo, rafiki.”
Shabiki mwingine amesisitiza: “Kadi nyekundu ya moja kwa moja.”
Tukio hilo limetokea takribani wiki mbili baada ya Rice kuhusika katika tukio linalofanana na Morgan Rogers wakati wa ushindi wa Arsenal wa mabao 2-1 dhidi ya Chelsea kwenye Uwanja wa Emirates.
Rice, aliyewahi kuichezea West Ham, alimkwaza Rogers, ambaye aliamini kiungo huyo mwenzake wa timu ya taifa ya England alifanya hivyo kwa makusudi ili kuzuia shambulizi la Chelsea.
Hali ya mvutano ilizuka kati ya wachezaji hao wawili, huku wakikabiliana kwa hasira kabla ya wachezaji wengine kuingilia kati na kutuliza mambo.
Rogers alionyeshwa kadi ya njano, lakini Rice hakuchukuliwa hatua yoyote kufuatia tukio hilo lililozua mjadala.