Tuchel ataja sababu ya kumbwaga Maguire
Muktasari:
- Hata hivyo, Tuchel amesema Harry Maguire amejinyima mwenyewe nafasi ya kurejea katika kikosi cha England baada ya kumkosoa hadharani kocha huyo kwa kutomchagua katika kikosi kilichokwenda Kombe la Dunia.
LONDON, ENGLAND: KOCHA wa timu ya taifa ya England, Thomas Tuchel, amempa beki wa Real Madrid, Trent Alexander-Arnold, nafasi nyingine ya kuthibitisha kuwa anastahili kuwa sehemu ya mipango ya baadaye ya timu hiyo.
Hata hivyo, Tuchel amesema Harry Maguire amejinyima mwenyewe nafasi ya kurejea katika kikosi cha England baada ya kumkosoa hadharani kocha huyo kwa kutomchagua katika kikosi kilichokwenda Kombe la Dunia.
Alexander-Arnold na mshambuliaji wa Chelsea, Cole Palmer, wameitwa tena katika kikosi cha Tuchel kwa mara ya kwanza tangu Kombe la Dunia.
Tuchel, ambaye amemtumia Alexander-Arnold mara moja pekee tangu alipokuwa kocha wa England, amesema beki huyo bado ana nafasi ya kupigania nafasi yake.
"Najua ana uwezo gani. Najua kipaji chake. Anatamani sana kuichezea England na atapambana kwa ajili ya nafasi yake," Tuchel amesema.
Hata hivyo, kocha huyo wa Ujerumani amesisitiza kuwa Alexander-Arnold lazima aonyeshe kiwango kizuri zaidi katika ulinzi.
"Ni lazima sasa aonyeshe uwezo wa kutosha katika ulinzi. Hilo ni jambo la lazima. Ninaamini atafanya hivyo, lakini hana chaguo," amesema Tuchel.
Alexander-Arnold, mwenye umri wa miaka 27, amepata nafasi mpya baada ya majeraha ya Djed Spence, Reece James na Ben White. Amecheza mechi tano kati ya saba za Real Madrid msimu huu, akianza tatu.
Katika moja ya mechi hizo, kocha wa Real Madrid alimchezesha Alexander-Arnold kama kiungo wa kati katika ushindi wa Champions League dhidi ya Inter Milan.
Lakini Tuchel amesema Alexander-Arnold atatumika kama beki wa kulia akiwa na England.
"Alianza vizuri akiwa katika nafasi mbili tofauti Real Madrid, lakini kwetu anakuja kama beki wa kulia," amesema.
Tuchel pia alizungumza kwa matumaini kuhusu Palmer na Alex Scott, ambaye anatarajiwa kucheza mechi yake ya kwanza ya kimataifa.
Kuhusu Palmer, Tuchel amesema: "Takwimu zake zimerudi, pasi za mabao na mabao muhimu. Ana jambo la kuthibitisha."
Kuhusu Scott, Tuchel amesema: "Alex Scott ni mchezaji na mtu mwenye tabia nzuri sana, mnyenyekevu, na ni mmoja wa viungo bora katika Premier League."
Katika kikosi hicho, Dominic Calvert-Lewin wa Leeds amerejea akiwa msaidizi wa nahodha Harry Kane katika safu ya ushambuliaji. Beki wa Everton, Jarrad Branthwaite, naye amechaguliwa badala ya Levi Colwill.
Pia kulikuwa na kurejea kwa mabeki wa Newcastle, Lewis Hall na Tino Livramento, pamoja na Myles Lewis-Skelly wa Arsenal.
Kwa upande mwingine, nahodha wa Nottingham Forest, Morgan Gibbs-White, hajaingia tena kwenye kikosi, huku kiungo wa Manchester City, Phil Foden, pia akikosa nafasi.