Rekodi mbovu... Man United ya Amorim ni hovyo
Muktasari:
- Juzi Jumapili usiku, Man United ilipokea kichapo cha kwanza cha ligi msimu huu katika mchezo wa kwanza kwa bao 1-0 nyumbani kutoka kwa Arsenal na wa 15 kwa kocha huyo kupoteza Ligi Kuu.
MANCHESTER, ENGLAND: KOCHA wa Manchester United, Ruben Amorim ameweka rekodi mbaya Ligi Kuu England ya kuwa kocha aliyepoteza mechi nyingi zaidi kati ya 28 walizosimamia, huku mwenyewe akidai ubora upo.
Juzi Jumapili usiku, Man United ilipokea kichapo cha kwanza cha ligi msimu huu katika mchezo wa kwanza kwa bao 1-0 nyumbani kutoka kwa Arsenal na wa 15 kwa kocha huyo kupoteza Ligi Kuu.
Kocha huyo aliyetua United akitokea Sporting Lisbon ya Ureno Novemba mwaka jana, amepoteza michezo hiyo kati ya 28 ikiwa ni rekodi mbaya kwa timu ambazo hazijatoka kupanda daraja.
Ni rekodi mbaya pia katika klabu hiyo kwa makocha waliopita baada ya Sir Alex Ferguson na wengine walipoteza mechi chache katika mechi 28 za EPL, ambao ni David Moyes (8), Luis Van Gal (6), Jose Morinho (5), Ole Gunnar Solskjaer na Erik Ten Hag wote (5).
Kwa timu zinazopanda daraja, imekuwa ni kawaida kwao kupoteza michezo mingi, lakini zile ambazo ziko Ligi Kuu England, makocha wao wamekuwa wakipoteza idadi ndogo ya mechi na rekodi hii inaifikia ya Kocha wa Portsmouth, Paul Hart aliyepoteza idadi kama hiyo lakini timu yake ikiwa imepanda daraja kutoka Championship.
Licha ya kusajili kwa pesa nyingi dirisha hili la usajili linaloendelea, lakini mambo hayakuwa mazuri kwa kikosi cha Amorim ingawa kilitawala sehemu kubwa ya mchezo huo.
Baada ya mechi hiyo, mchezaji wa zamani wa Man United, Roy Keane alitoa maoni yake, kipa aliyeanza Altay Bayındir ndiyo sababu ya timu kupoteza pointi.
"Kama wewe ni kipa, chukua udhibiti wa boksi lako, Unajua makipa na mabeki walionekana wakilalamika muda wote, kwa sababu kulikuwa na wachezaji mbele yao lakini walichotakiwa kufanya ni kwenda mbele yao na kutumia nguvu kisha kuwa watawala wa eneo hilo. Kipa lazima uwe mtawala wa boksi na muda wote uwe unaangalia mpira. Nimesema mara nyingi kwa kuwa kipa akiwa eneo lile inatakiwa aingie kwa nguvu kwa sababu lile ni eneo lake."
"Arsenal wanafanya vizuri sana katika hili. Lakini Man United ni dhaifu na laini."
Kwa upande wake, kocha wa Man United alisema ameridhishwa na kiwango ambacho timu yake ilikionyesha ingawa hawakupata matokeo, lakini kikosi kilionyesha kuwa na ubora kwa asilimia kadhaa.
Amorim amekumbana na changamoto nyingi tangu alipochukua nafasi ya Erik ten Hag Manchester mwaka jana na aliiongoza Red Devils kumaliza nafasi ya 15 katika ligi msimu uliopita na ikashindwa kufuzu michuano ya kimataifa kwani licha ya kuwa na matumaini ya kupitia Europa League huko nako walipoteza mbele Tottenham.