Real Madrid yamtaka Van Dijk
Muktasari:
- Beki huyo wa Uholanzi atakuwa mchezaji huru endapo hatasaini mkataba mpya na Liverpool, jambo linaloweza kuifanya Real Madrid kuanza rasmi harakati za kumshawishi kuhamia Santiago Bernabeu.
REAL Madrid inafikiria kumsajili nahodha wa Liverpool, Virgil van Dijk, 35, ambaye mkataba wake na klabu hiyo unamalizika mwishoni mwa msimu huu.
Beki huyo wa Uholanzi atakuwa mchezaji huru endapo hatasaini mkataba mpya na Liverpool, jambo linaloweza kuifanya Real Madrid kuanza rasmi harakati za kumshawishi kuhamia Santiago Bernabeu.
Kwa mujibu wa vyombo vya habari vya Uingereza, uwezekano wa Liverpool kumpa mkataba mpya beki huyo bado haujawekwa wazi, jambo ambalo limeanza kuzua tetesi kuhusu klabu zinazoweza kumsajili.
Real Madrid imetajwa miongoni mwa klabu zinazoweza kumuwania beki huyo wa kimataifa wa Uholanzi, hasa kutokana na uwezekano wa kumpata kwa uhamisho wa bure.
Mbali na Real Madrid, AC Milan, Inter Miami na Galatasaray pia zimetajwa kuwa miongoni mwa klabu zinazoweza kuonyesha nia ya kumsajili Van Dijk.
Real Madrid ilimsajili beki wa Ufaransa, Ibrahima Konate, kwa uhamisho wa bure kutoka Liverpool katika dirisha lililopita, na uwezekano wa Van Dijk kufuata njia hiyo umeanza kuibua mjadala.
Vin Dijk alijiunga na Liverpool msimu wa 2018/19 na amecheza zaidi ya mechi 270 akiisaidia timu hiyo kutwaa mataji ya Ligi Kuu England na Ligi ya Mabingwa Ulaya akiwa kama nahodha na beki kisiki.
Phil Foden
Bayern Munich iko tayari kumuwania kiungo wa Manchester City na timu ya taifa ya England, Phil Foden, 26, iwapo atapatikana kwa ajili ya uhamisho. Foden anaweza kuwa kwenye rada za mabingwa hao wa Ujerumani endapo Manchester City itaweka wazi uwezekano wa kumuuza kiungo huyo katika dirisha lijalo la usajili.
Giorgio Scalvini
Beki wa Atalanta na timu ya taifa ya Italia, Giorgio Scalvini, 22, anataka kupata uzoefu wa kucheza nje ya Italia katika hatua fulani ya maisha yake ya soka. Scalvini tayari ameshaanza kuwindwa na klabu za England, Newcastle United na Chelsea, ambazo zimeonyesha nia ya kumsajili beki huyo.
Yankuba Minteh
Winga wa Brighton na timu ya taifa ya Gambia, Yankuba Minteh, 22, bado ana nia ya kujiunga na Liverpool licha ya mpango wa kuhamia klabuni hapo kushindikana katika dirisha la usajili la majira ya kiangazi. Minteh bado anatajwa kuwa na hamu ya kuvaa jezi ya Liverpool, huku uwezekano wa uhamisho wake kuendelea kuwa suala la kufuatiliwa katika dirisha lijalo.
Kim Min-jae
Tottenham Hotspur imeonyesha nia ya kumsajili beki wa Bayern Munich na timu ya taifa ya Korea Kusini, Kim Min-jae, 29.Klabu hiyo ya London inamtazama Min-jae kama miongoni mwa wachezaji wanaoweza kuimarisha safu yake ya ulinzi, huku ikifuatilia kwa karibu uwezekano wa kumnasa kutoka Bayern.
Matteo Darmian
Beki wa zamani wa Manchester United, Matteo Darmian, 36, anatarajiwa kuanza mazoezi na Bologna kesho Jumatano, baada ya kuachana na Inter Milan mwishoni mwa msimu uliopita. Darmian, ambaye pia amewahi kuitumikia timu ya taifa ya Italia, yuko huru kwa sasa baada ya kumaliza mkataba wake na Inter na sasa anatarajiwa kuungana na Bologna kwa ajili ya mazoezi.
Lautaro Martinez
Barcelona imekiri kuwa ilijaribu kumsajili mshambuliaji wa Argentina na Inter Milan, Lautaro Martinez, 29, katika dirisha la usajili lililopita, lakini ikashindwa kukamilisha dili hilo. Lautaro, ambaye anaendelea kuitumikia Inter Milan, alikuwa miongoni mwa wachezaji waliolengwa na Barcelona katika dirisha hilo, lakini mipango ya kumsajili haikufanikiwa.
Jules Kounde
Bayern Munich imeanza kuangalia uwezekano wa kumsajili beki wa Barcelona na timu ya taifa ya Ufaransa, Jules Kounde, 27, ambaye ameanza msimu huu akiwa nje ya mipango ya kikosi cha kwanza cha Barcelona. Kounde sasa ameingia kwenye rada za Bayern, huku mabingwa hao wa Ujerumani wakitazama uwezekano wa kumshawishi beki huyo kuhamia Bundesliga.
Jean-Philippe Mateta
MANCHESTER United inamuwinda mshambuliaji wa Crystal Palace na timu ya taifa ya Ufaransa, Jean-Philippe Mateta, 29, ikiwa sehemu ya mpango wa kuimarisha safu yake ya ushambuliaji. Mateta amekuwa kwenye orodha ya wachezaji wanaolengwa na United, ambayo inaendelea kutafuta chaguo la kuongeza nguvu katika eneo la mbele.
Michael Olise
Bayern Munich ipo kwenye mpango wa kumpa mkataba mpya mshambuliaji wake Mfaransa, Michael Olise, utakaomfanya aendelee kuitumikia klabu hiyo hadi mwaka 2032. Olise, 24, kwa sasa ana mkataba na miamba hiyo ya Bundesliga unaomalizika mwaka 2029, lakini Bayern inataka kuongeza muda wa kukaa kwake kwa miaka mingine mitatu.