Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Anthony Martial akataa Sh33 bil, aichagua Malaga

FUNUNU Pict

Muktasari:

  • Martial, 30, anatarajiwa kutua Malaga baada ya klabu hiyo inayoshika nafasi ya 18 kwenye LaLiga kukaribia kukamilisha usajili wake, kwa mujibu wa Foot Mercato.

MALAGA, HISPANIA: Mshambuliaji wa zamani wa Manchester United, Anthony Martial, yuko mbioni kujiunga na Malaga kama mchezaji huru baada ya kukataa ofa nono iliyokuwa na thamani ya pauni 13 milioni (zaidi ya Sh33 bilioni).

Martial, 30, anatarajiwa kutua Malaga baada ya klabu hiyo inayoshika nafasi ya 18 kwenye LaLiga kukaribia kukamilisha usajili wake, kwa mujibu wa Foot Mercato.

Mfaransa huyo alikatisha mkataba wake na CF Monterrey mwanzoni mwa majira ya kiangazi na tangu wakati huo amekuwa akitafuta klabu mpya.

Ripoti zinaeleza kuwa Martial amekataa ofa mbili kutoka klabu za Ligue 1 nchini Ufaransa, huku klabu ya Al-Ittihad Tripoli ya Libya nayo ikitajwa kuwa ilijaribu kumshawishi mshambuliaji huyo.

Al-Ittihad Tripoli hivi karibuni ilifanya usajili wa winga wa Morocco, Sofiane Boufal, mwenye umri wa miaka 32.

Klabu hiyo ilimpa Martial ofa yenye mshahara wa jumla wa pauni 8.6 milioni kwa kipindi cha miaka miwili, pamoja na bonasi ya kusaini mkataba ya pauni milioni 4.3.

Endapo angekubali, Martial angeweza kuvuna jumla ya pauni12.9 milioni, sawa na zaidi ya Sh33 bilioni, hadi mwishoni mwa mwaka 2028.

Uamuzi wa kukataa fedha hizo unaashiria kuwa Martial anaangalia zaidi nafasi ya kufufua tena maisha yake ya soka kuliko kukimbilia maslahi ya kifedha. Malaga inaweza kuwa sehemu ya kuanzia safari hiyo mpya.

Klabu hiyo ilipanda daraja kutoka LaLiga 2 msimu wa 2025/26 baada ya kumaliza katika nafasi ya nne na kufanikiwa kuwashinda Las Palmas na Almeria katika mechi za mchujo.

Katika michezo yake mitano ya kwanza baada ya kurejea LaLiga, Malaga imepoteza mara mbili pekee, dhidi ya vigogo Real Madrid na Atletico Madrid.

Katika michezo yake mingine mitatu, Los Boquerones imetoka sare mara zote, ikiwamo sare dhidi ya Villarreal iliyomaliza katika nafasi ya nne msimu uliopita.


Rio Ngumoha

Arsenal imeanza kufuatilia kwa karibu maendeleo ya kinda wa Liverpool, Rio Ngumoha, huku mazungumzo ya mkataba mpya kati ya mchezaji huyo na miamba hiyo ya Anfield yakiendelea. Ngumoha, 18, amepiga hatua kubwa tangu msimu uliopita na sasa anaonekana kama mmoja wa vipaji vinavyotajwa kuwa na uwezo wa kuwa nyota mkubwa wa baadaye, hali inayovutia macho ya Arsenal.


Luca Weinhandl

Arsenal, Brighton na Aston Villa zimeanza kufuatilia kwa karibu maendeleo ya kiungo kinda wa Austria, Luca Weinhandl, 17, anayeng’ara katika kikosi cha Sturm Graz. Weinhandl anatajwa kuwa anaweza kuuzwa kwa ada ya karibu Pauni 17 milioni, huku klabu hizo za Ligi Kuu England zikifuatilia uwezekano wa kumnasa kinda huyo anayechukuliwa kuwa mmoja wa vipaji vya baadaye.


Mauro Icardi

Tottenham imeingia kwenye orodha ya klabu zinazohusishwa na mshambuliaji wa Argentina, Mauro Icardi, ambaye kwa sasa hana klabu baada ya kuondoka Galatasaray mwezi Julai. Icardi, 33, sasa anaweza kujiunga na timu yoyote kama mchezaji huru huku Tottenham ikitajwa kuwa miongoni mwa klabu zinazofuatilia uwezekano wa kumnasa.


Yves Bissouma

Kiungo wa Mali, Yves Bissouma, yuko mbioni kujiunga na Ajax kama mchezaji huru baada ya mkataba wake na Tottenham kumalizika. Ajax inatajwa kuwa tayari kumpa nafasi nyota huyo mwenye umri wa miaka 30, ambaye ana uzoefu mkubwa wa Ligi Kuu England akiwa amecheza jumla ya mechi 202 katika misimu minane.


Noah Ajayi

Manchester United iko kwenye hatua za mwisho za kumsainisha mkataba wake wa kwanza wa kitaalamu kiungo kinda wa Ujerumani, Noah Ajayi (17). Ajayi, ambaye ni miongoni mwa vipaji vinavyokuzwa na klabu hiyo, anatarajiwa kuweka saini mkataba huo hivi karibuni.


Rodrygo

Arsenal inaendelea kufuatilia hali ya mshambuliaji wa Real Madrid, Rodrygo, 25, ambaye kwa sasa yupo kwenye kipindi cha kupona majeraha, baada ya klabu hiyo ya London kuonyesha nia ya kumsajili Mbrazil huyo katika dirisha la usajili lililopita. Arsenal sasa inafuatilia kwa karibu maendeleo ya afya yake kabla ya kuchukua hatua zaidi kuhusu uwezekano wa kumleta Emirates.


Luke Shaw

Beki wa Manchester United, Luke Shaw, anaweza kuondoka kwenye klabu hiyo mwishoni mwa msimu ujao, huku kukiwa hakuna dalili za mazungumzo ya kuongeza mkataba kati yake na mabosi wa klabu hiyo. Shaw, 31, ambaye ni raia wa England, bado hajafikia hatua ya kupewa ofa mpya ya mkataba, jambo linalozua uwezekano wa kuondoka Old Trafford baada ya msimu ujao.


Lamine Camara

Liverpool inafikiria kumsajili kiungo wa Monaco na Senegal, Lamine Camara, katika dirisha la usajili la Januari, baada ya nyota huyo mwenye umri wa miaka 22 kushindwa kukamilisha uhamisho wa siku ya mwisho kwenda Chelsea. Camara sasa ameibua hamu ya Liverpool, ambayo inatajwa kuangalia uwezekano wa kumnasa katika dirisha lijalo.


Jean-Matteo Bahoya

Leeds United haitaki kufanya haraka katika uamuzi wa kumsajili moja kwa moja mshambuliaji wa Eintracht Frankfurt, Jean-Matteo Bahoya, baada ya kumchukua kwa mkopo. Klabu hiyo ina kipengele cha kumnunua moja kwa moja Mfaransa huyo mwenye umri wa miaka 21 kwa ada ya Pauni 19.7 milioni, lakini bado inataka kumpa muda kabla ya kuamua iwapo itatumia fursa hiyo.