Real Madrid ‘kimeumana’ tena
Muktasari:
- Kwa mujibu wa taarifa za kituo cha redio cha Hispania, Cadena SER, hali ya uhusiano baina ya wachezaji wa Los Blancos bado ni ya mvutano, huku kukiwa na madai ya wachezaji wawili kuingia katika mzozo ndani ya vyumba vya kubadilishia nguo hivi karibuni.
MADRID, HISPANIA: KLABU ya Real Madrid inadaiwa kuendelea kukabiliwa na misuguano ya ndani ya kikosi, licha ya kurejea kwa kocha Jose Mourinho, ambaye ameshindwa kurejesha utulivu katika vyumba vya kubadilishia nguo vya timu hiyo hali inayosababisha wachezaji kupigana kila mara.
Kwa mujibu wa taarifa za kituo cha redio cha Hispania, Cadena SER, hali ya uhusiano baina ya wachezaji wa Los Blancos bado ni ya mvutano, huku kukiwa na madai ya wachezaji wawili kuingia katika mzozo ndani ya vyumba vya kubadilishia nguo hivi karibuni.
Wachezaji hao hawajatajwa majina, lakini mwandishi wa habari wa kituo hicho, Anton Meana, amesema hali ya hewa ndani ya kikosi hicho bado ni ya baridi, licha ya Mourinho kurejea kwa mbinu zake kali za uongozi.
Meana amesema hali hiyo inaendelea kufanana na ilivyokuwa miezi mitano iliyopita, akiongeza kuwa misuguano ya ndani pamoja na sakata linalomzunguka mshambuliaji Kylian Mbappe vimeongeza presha kwa timu hiyo katika kipindi muhimu cha msimu.
Real Madrid ilikumbwa na matukio kadhaa ya sintofahamu msimu wa 2025/26, yakihusisha madai ya kutokuelewana kati ya wachezaji na makocha. Hali ilifikia hatua mbaya mwezi Mei, wakati viungo Federico Valverde na Aurelien Tchouameni waliporipotiwa kuhusika katika mzozo wa kimwili.
Pia, kikosi hicho kiliripotiwa kushindwa kuwa na uhusiano mzuri na makocha Xabi Alonso na Alvaro Arbeloa katika vipindi vyao vya uongozi, jambo lililochangia wasiwasi kuhusu umoja wa timu hiyo.
SAKATA LA MBAPPE
Mbali na mvutano huo, Mbappe naye amekuwa sehemu ya mjadala baada ya namna alivyosimamia kipindi chake cha kupona jeraha.
Mshambuliaji huyo alilazimika kujiondoa katika kikosi cha timu ya taifa ya Ufaransa baada ya kufunga bao la ushindi dhidi ya Uturuki katika mchezo wa kwanza wa michuano ya kimataifa.
Shirikisho la Soka la Ufaransa lilieleza kuwa Mbappe alikuwa akisumbuliwa na jeraha la goti la kushoto. Hata hivyo, mshambuliaji huyo alirejea mazoezini Jumatano na anatarajiwa kuwa tayari kuisaidia Real Madrid katika mchezo wake ujao wa ligi.
Kabla ya kurejea Hispania, Mbappe alionekana katika klabu ya burudani jijini Paris akiwa na mwenzi wake, Ester Exposito. Baadaye alionekana akifanya mazoezi ya kuendesha baiskeli katika milima ya Alps nchini Uswisi, hatua inayodaiwa kutomfurahisha Mourinho.
Mbappe alichapisha video yake akionekana kufurahia safari hiyo ya baiskeli Jumapili, jambo lililoibua mjadala kuhusu nidhamu na namna wachezaji wanavyopaswa kujitunza wanapokuwa katika kipindi cha kupona majeraha.
Mwezi uliopita, Mourinho alieleza wazi kuwa anatarajia wachezaji wake kuzingatia taaluma yao wakati wote, akionya dhidi ya shughuli zinazoweza kuwaweka katika hatari ya kupata majeraha.
Kocha huyo raia wa Ureno amesisitiza kuwa maisha ya mchezaji wa soka yanapaswa kuzingatia mambo kama lishe, usingizi, vinywaji na shughuli za nje ya uwanja.
Amesema hata kuendesha baiskeli kunaweza kuwa hatari ikiwa mchezaji ataanguka na kupata jeraha linaloweza kumuweka nje ya uwanja kwa muda mrefu.
Kwa mujibu wa taarifa zilizochapishwa na mwandishi wa habari wa Marca, Pablo Polo, Mourinho hakufurahishwa na namna Mbappe alivyoshughulikia kipindi chake cha kupona, pamoja na ratiba ya kurejea kwake mazoezini.
Mourinho anadaiwa kumkanya mshambuliaji huyo na kumtaka awe makini zaidi na namna anavyoendesha shughuli zake binafsi nje ya uwanja.
PRESHA IPO JUU
Licha ya changamoto hizo za ndani, Real Madrid imeanza msimu wa 2026/27 kwa matokeo yenye mchanganyiko chini ya Mourinho.
Timu hiyo imeshinda mechi tano kati ya saba za awali za LaLiga, lakini bado inadaiwa kuwa na pengo la pointi sita nyuma ya Barcelona.
Real Madrid sasa inaelekeza nguvu zake katika mchezo wa nyumbani dhidi ya Villarreal utakaochezwa kesho, kabla ya kusafiri kwenda Italia kukutana na Roma katika Ligi ya Mabingwa Ulaya Jumatano ijayo.
Huku michezo muhimu ikikaribia, macho yataendelea kuelekezwa kwa Mourinho kuona kama ataweza kurejesha umoja wa kikosi hicho na kudhibiti misuguano inayoripotiwa kuendelea ndani ya vyumba vya kubadilishia nguo vya Santiago Bernabeu.