Ronaldo apewa nafasi nyingine
Muktasari:
- Ronaldo alikosa mchezo wa Ureno dhidi ya Norway Jumapili iliyopita, ambao Ureno ilishinda kwa mabao 2-1, baada ya kuondoka kwenye kambi ya timu hiyo kufuatia mvutano na Jesus.
LISBON, URENO: CRISTIANO Ronaldo amepewa nafasi nyingine ya kurejea kwenye kikosi cha timu ya Taifa ya Ureno, licha ya kuondoka kambini kwa kishindo baada ya kutofautiana na kocha Jorge Jesus hivi karibuni.
Ronaldo alikosa mchezo wa Ureno dhidi ya Norway Jumapili iliyopita, ambao Ureno ilishinda kwa mabao 2-1, baada ya kuondoka kwenye kambi ya timu hiyo kufuatia mvutano na Jesus.
Nyota huyo mwenye umri mkubwa kwenye kikosi hicho alikerwa na uamuzi wa kuachwa benchi katika mchezo wa kwanza dhidi ya Norway, hali iliyomfanya kukosa mazoezi mara tatu na pia kutoshiriki mchezo wa Alhamisi dhidi ya Denmark.
Baadaye aliondoka nchini humo kwa ndege yake binafsi, huku kukiwa na taarifa kwamba bado anaweza kukumbana na adhabu ya kufungiwa hadi miezi sita kwa kitendo chake.
Ronaldo pia amesema atakuja kueleza “ukweli” kuhusu sababu zilizomfanya kuondoka kambini, jambo lililofanya sakata hilo kuwa gumzo kubwa katika mapumziko ya mechi za kimataifa.
JESUS AFUNGUA MLANGO
Licha ya yote yaliyotokea, kocha Jesus ameweka wazi kuwa mlango wa Ronaldo kurejea bado uko wazi na anaweza kurudi kwenye kikosi cha Ureno katika michezo ya mwezi Novemba.
Jesus amesema uamuzi wa mwisho uko mikononi mwa Ronaldo mwenyewe, akisisitiza kuwa hakuna uhasama kati yao.
Kwa mujibu wa kocha huyo, endapo Ronaldo ataendelea kucheza vizuri akiwa na Al-Nassr na akatamani kuitumikia nchi yake, hakuna sababu ya yeye kuachwa nje ya kikosi.
Jesus pia alieleza kuwa suala la Ronaldo kuwa benchi halikupaswa kuwa kubwa kiasi hicho, lakini kwa sababu Ronaldo ni alama kubwa ya timu ya taifa, kila kinachomhusu huwa kinapata uzito zaidi.
WENZAKE WAMTAKA
Ujumbe wa Jesus umeungwa mkono na wachezaji wa Ureno ambao nao wameweka wazi kuwa wanataka Ronaldo arejee.
Beki Nuno Mendes amesema baada ya ushindi dhidi ya Norway kwamba Ronaldo, kama ilivyo kwa mchezaji mwingine yeyote ambaye hayupo kwenye kikosi, atakaribishwa kwa mikono miwili.
Nahodha msaidizi Joao Cancelo naye amesema Ronaldo bado ni nahodha wao, ishara ya timu ya taifa na mchezaji bora zaidi kuwahi kuichezea Ureno.
Bruno Fernandes pia amekuwa mstari wa mbele katika kutuliza hali hiyo baada ya kufichua kuwa amezungumza na Ronaldo ili kumaliza tofauti zilizopo.
Fernandes amesema Ronaldo ataendelea kuwa alama kubwa ya timu ya taifa na ya nchi hiyo kutokana na mambo yote aliyofanya kwa Ureno na duniani.
Alisisitiza pia kuwa timu ya taifa haipaswi kugawanyika kwa sababu ya suala hilo, akitaka tofauti zote zimalizwe ndani ya familia ya timu.
ANAWEZA KURUDI?
Ureno imeendelea kufanya vizuri hata bila Ronaldo, ikiwa imeshinda michezo yake mitatu ya hivi karibuni.
Katika ushindi wa 2-1 dhidi ya Norway, Ureno ilihitaji bao la dakika ya 79 kutoka kwa mshambuliaji wa AC Milan, Gonçalo Ramos, kukamilisha mapinduzi ya matokeo.
Mchezo huo pia ulimshuhudia Erling Haaland akitoka uwanjani akiwa anaonekana kupata maumivu.
Pamoja na mafanikio hayo bila Ronaldo, wachezaji wa Ureno bado wanataka nyota huyo arejee kwenye kikosi.
ZIDANE NAYE AMTETEA
Miongoni mwa majina makubwa yaliyomtumia ujumbe wa heshima kwa Ronaldo ni Zinedine Zidane, kocha wake wa zamani Real Madrid.
Zidane alimsifu Ronaldo kwa kazi kubwa aliyofanya katika soka na kusema ana heshima kubwa kwake kutokana na mafanikio waliyopata pamoja.
Wakati huo huo, mke wa Ronaldo, Georgina Rodriguez, naye alionekana kumtetea mumewe kwenye mitandao ya kijamii.
Rodriguez aliweka kwenye Instagram ujumbe uliokuwa ukimlenga Jesus pamoja na nukuu iliyodaiwa kutoka kwa aliyekuwa kocha wa Manchester United, Sir Alex Ferguson.
Hata hivyo, ujumbe huo ulifutwa muda mfupi baadaye. Ferguson hajawahi kutoa kauli kuhusu mgogoro huo na nukuu hiyo ilionekana kuwa ya kutengenezwa kwa kutumia teknolojia ya AI.
Kwa sasa, macho yote yanaelekezwa kwenye mapumziko yajayo ya mechi za kimataifa mwezi Novemba, ambapo Ronaldo anaweza kupata nafasi ya kurejea kwenye kikosi cha Ureno iwapo atakubaliana na Jesus na atakuwa tayari kuitumikia nchi yake.