Chombo ajifananisha na Chama, Mzize
Muktasari:
- Amemchambua Chama ambaye msimu uliopita wa 2025/26, alikuwa na mabao manane, asisti saba, 2026/27 mabao manne, kwamba anatumia akili kubwa kuliko nguvu na akicheza anaufanya mpira kuonekana ni rahisi kwa upande wa Mzize ambaye msimu wa 2023/24, alikuwa na mabao sita, asisti saba, 2024/25 alikuwa na mabao 14 asisti tano, 2025/26 alikuwa anakabiliwa na majereha anamuona ni fundi wa kucheka na nyavu.
MSHAMBULIAJI wa timu ya Sauti Parasport ya mpira wa miguu ya walemavu, Salim Chombo amesema kama isingekuwa kupata ajali ya gari na kukatwa mguu mmoja, huenda angekuwa anatajwa katika ‘level’ za mastaa kama Clement Mzize wa Yanga na Clatous Chama wa Simba.
Amesema alikuwa anapenda kucheza soka tangu akiwa mdogo, namna alivyokuwa anaambiwa na watoto wenzake pamoja na walimu, anaamini angekuwa mchezaji mkubwa na wa kutegemewa katika timu.
“Kabla sijaanza darasa la kwanza mwaka 2006, ndipo nilipopata ajali, nilikuwa mimi na kaka yangu tulikuwa tumetoka shambani, kaka alikuwa anapiga ndege kwa manati, mimi nikawa narukaruka nikapitiwa na gari la mchanga,” amesema Chombo na kuongeza;
“Baada ya kutibiwa na kupona mwaka 2007, nilipelekwa shule ya Kikristo la Jeshi la Wokovu ambayo ina walemavu watupu, hilo lilinisaidia kuchukulia ni hali ya kawaida na natakiwa kuishi nayo”.
Chombo ambaye ni mchezaji wa timu ya taifa ya Tanzania ya mpira wa miguu kwa watu wenye ulemavu, (walemavu wa mguu mmoja), amesema:
”Uwanjani nacheza nafasi ya winga, namba 9 na beki wa pembeni, ndiyo maana nasema isingekuwa kukatwa mguu ningekuwa natajwa kama wanavyotajwa kina Chama na Mzize.
Amemchambua Chama ambaye msimu uliopita wa 2025/26, alikuwa na mabao manane, asisti saba, 2026/27 mabao manne, kwamba anatumia akili kubwa kuliko nguvu na akicheza anaufanya mpira kuonekana ni rahisi kwa upande wa Mzize ambaye msimu wa 2023/24, alikuwa na mabao sita, asisti saba, 2024/25 alikuwa na mabao 14 asisti tano, 2025/26 alikuwa anakabiliwa na majereha anamuona ni fundi wa kucheka na nyavu.
“Mashindano ya soka kwa watu wenye ulemavu ya Azam TV Amputee Football Tournament 2025, nilimaliza na mabao saba na kinara alikuwa na 11 wakati 2026 nilimaliza na mabao mawili na nilicheza mechi zote nikiwa na majeraha.” amesema.