Rasmi Baleba asaini miaka mitano Man United
Muktasari:
- Baleba amekamilisha dili hilo kwa ada ya Pauni 65 milioni inayoweza kufikia Pauni 70 milioni pamoja na nyongeza (takriban Sh230 bilioni za Tanzania), huku akisaini mkataba wa miaka mitano (5) wenye kipengele cha kuongeza mwaka mmoja zaidi.
Kiungo wa kimataifa wa Cameroon, Carlos Baleba amekamilisha usajili wa kujiunga na Manchester United akitokea Brighton & Hove Albion.
Baleba amekamilisha dili hilo kwa ada ya Pauni 65 milioni inayoweza kufikia Pauni 70 milioni pamoja na nyongeza (takriban Sh230 bilioni za Tanzania), huku akisaini mkataba wa miaka mitano (5) wenye kipengele cha kuongeza mwaka mmoja zaidi.
Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 22, anakuwa mchezaji wa tatu kutua katika safu ya kiungo ya miamba hiyo ya Old Trafford chini ya Kocha Mkuu, Michael Carrick msimu huu wa 2026/27, akifuata nyayo za Andrey Santos na Youri Tielemans.
Baleba ameeleza kujiunga na klabu hiyo ni moja ya ndoto zake na ana shauku kubwa ya kufanya kazi na Carrick ili kukuza zaidi kiwango chake cha soka.
“Ni hisia za kipekee sana kujiunga na klabu ya ndoto zangu,” alisema mchezaji huyo baada ya kukamilisha uhamisho wake wa kujiunga na Manchester United.
“Daima kucheza katika Uwanja wa Old Trafford ni jambo la kipekee, lakini kupata nafasi ya kufanya hivyo kama mchezaji wa Manchester United ni heshima kubwa kwangu.
“Siwezi kusubiri kuanza kufanya kazi na Michael Carrick. Uzoefu wake pamoja na uelewa wake mkubwa wa mchezo vinamfanya kuwa kocha sahihi wa kunisaidia kufikia kiwango cha juu zaidi.
“Dhamira ya kila mtu ndani ya klabu iko wazi kabisa. Mustakabali wa klabu unasisimua sana na nimeazimia kutoa mchango wangu katika kuifikisha timu kwenye mafanikio ambayo tuna uwezo wa kuyapata kwa pamoja.”
United ilirejesha tena nia ya kumsajili Baleba baada ya kujaribu kumpata mwaka uliopita karibu na siku ya mwisho ya usajili, lakini ilishindwa kutokana na Brighton kuweka thamani yake zaidi ya Pauni 100 milioni.
Baleba alijiunga na Brighton akitokea Lille mwaka 2023, lakini kwa sasa yupo nje ya uwanja kutokana na majeraha ya kifundo cha mguu aliyoyapata wakati wa kambi ya maandalizi ya msimu nchini Austria.
Mchezaji huyo ameitumikia Brighton mechi 112 na kufunga mabao manne, huku msimu uliopita akicheza mechi 31 za Ligi Kuu England, akisaidia timu hiyo kumaliza nafasi ya nane na kufuzu Conference League.
Usajili huo umeifanya Manchester United kutumia jumla ya Pauni 153 milioni katika dirisha hili la usajili, huku ikijiandaa kurejea kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya kwa mara ya kwanza tangu msimu wa 2023/24.