Raphinha aingia anga za Newcastle United
Muktasari:
- Raphinha ni miongoni mwa wachezaji tegemeo katika kikosi cha kwanza cha Barca na msimu uliopita alifunga mabao 10 na kutoa asisti 12.
MABOSI wa Newcastle United wapo tayari kuwasilisha ofa kubwa kwa ajili ya kumsajili winga wa kimataifa wa Brazil, Raphinha, 28, ikiwa Barcelona itakuwa tayari kumuuza mwisho wa msimu huu.
Raphinha ni miongoni mwa wachezaji tegemeo katika kikosi cha kwanza cha Barca na msimu uliopita alifunga mabao 10 na kutoa asisti 12.
Licha ya timu nyingi kuonyesha nia ya kumsajili tangu mwaka jana, Barca haikuwa tayari kumuuza staa huyu ambaye mkataba wake wa sasa unatarajiwa kumalizika mwaka 2028.
Hivi karibuni staa huyu pia amekuwa akisumbuliwa sana na majeraha ya misuli ya paja hali iliyosababisha akose mechi kadhaa na tangu kuanza kwa msimu amecheza mechi 10 za michuano yote, amefunga mabao matatu na kutoa asisti tatu.
Mabosi wa Newcastle wanaamini staa huyu atasaidia sana safu yao ya ushambuliaji kutokana na uzoefu wake wa EPL alioupata wakati anacheza Leeds United.
Mabosi wa arca huenda wakahitaji zaidi ya Pauni 90 milioni ili kumuuza staa huyu.
Iliman Ndiaye
MANCHESTER City, Tottenham na Liverpool, zimefanya mawasiliano ya awali ili kumsajili mshambuliaji wa Everton na timu ya taifa ya Senegal, Iliman Ndiaye, mwenye umri wa miaka 25. Ndiaye ambaye msimu huu amefunga mabao nne katika mechi 15 za michuano yote, mkataba wake wa sasa unatarajiwa kumalizika mwaka 2029. Kabla ya kutua Everton, alionyesha kiwango bora sana akiwa na Marseille ya Ufaransa.
Adam Wharton
MANCHESTER United inaamini itafanikiwa kumsajili kiungo wa Crystal Palace, Adam Wharton, 21, kwa takribani Pauni 70 milioni katika dirisha lijalo. Hata hivyo, Wharton anaripotiwa kuwaambia mashetani hao wekundu anasubiri kuona ikiwa itafuzu kucheza michuano ya Ulaya kabla ya kufikia uamuzi wa kujiunga nao au laa. Palace haitaki kuona fundi huyu anaondoka kwa bei rahisi kutokana na umuhimu wake katika kikosi chao.
Murillo
BEKI wa Nottingham Forest, Murillo, 23, anatajwa kuwa sehemu ya vipaumbele vya Barcelona kuelekea dirisha lijalo la usajili la majira ya baridi. Benchi la ufundi la Barcelona, linaamini staa huyu atasaidia sana kuboresha safu yao ya ulinzi kutokana na uwezo wake. Hata hivyo, Forest haitaki kumuuza ingawa Barca inadaiwa kuwa tayari kutoa zaidi ya Pauni 45 miliuoni ili kumpata.
Igor Thiago
ASTON Villa inataka kuwasilisha ofa ya Pauni 50 milioni kwenda Brentford kwa ajili ya kumsajili mshambuliaji wa klabu hiyo, Igor Thiago, 24. Thiago amekuwa katika kiwango bora msimu huu na tayari amefunga mabao 12 katika Ligi Kuu England jambo lililozivutia timu nyingi ndani ya ligi hiyo na nje ya ligi hiyo. Fundi huyu alisajiliwa na Brentford akitokea Club Brugge mwaka 2024.
Carlos Baleba
TOTTENHAM Hotspur inahisi ina nafasi ya kuingilia kati na kuipiku Manchester United katika mchakato wa wa kuiwania saini ya kiungo wa Brighton na timu ya taifa ya Cameroon, Carlos Baleba, 21. Baleba ameendelea kuwa miongoni mwa viungo bora EPL msimu huu na amekuwa akihusishwa na Man United tangu dirisha lililopita la majira ya kiangazi. Brighton inahitaji zaidi ya Pauni 90 milioni ili kumuuza Baleba.
Sergio Ramos
BEKI wa zamani wa Real Madrid, Sergio Ramos, 39, anatarajiwa kuachana na klabu ya Monterrey ya Mexico mwishoni mwa msimu huu na amepanga kutafuta timu nyingine ya kuitumikia licha ya umri wake kumtupa mkono. Ramos amecheza msimu mmoja tu nchini Mexico, akicheza zaidi ya mechi 30 kwenye mashindano mbalimbali na kuwa kiongozi wa safu ya ulinzi ya Monterrey.
Klabu kutoka Ligi Kuu Marekani na Saudi Arabia zinatajwa kuwa katika mazungumzo ya kumsajili.
Ivan Toney
MSHAMBULIAJI wa Al-Ahli ya Saudi Arabia, Ivan Toney, 29, ameendelea kuhusishwa na tetesi za kurejea Ligi Kuu England Januari natimu nyingi zinahitaji saini yake. Toney ambaye ameonyesha kiwango bora tangu atue Saudi Arabia msimu huu amefunga mabao tisa na asisti nne. Timu nyingi za England hususani Tottenham zinahusishwa sana na fundi huyu ambaye mkataba wake unamalizika 2028.