Dili la Mike Maignan, Chelsea laanza upya
Muktasari:
- Mkataba wa Maignan unamalizika mwaka 2026, lakini Milan hawako tayari kumuuza, hivyo inapambana kumsainisha mkataba mpya.
CHELSEA imeanza tena kufanya mawasiliano na wawakilishi wa kipa wa AC Milan, Mike Maignan baada ya kujua kuwa kipa huyo wa kimataifa wa Ufaransa mwenye umri wa miaka 30 hataki kuongeza mkataba wa kuendelea kusalia katika klabu hiyo.
Mkataba wa Maignan unamalizika mwaka 2026, lakini Milan hawako tayari kumuuza, hivyo inapambana kumsainisha mkataba mpya.
Hata hivyo, msimamo wao huo huenda ukabadilika kwani ikiwa ataendelea kugoma kusaini itabidi auzwe tu Januari ili kuzuia asiondoke bure ifikapo mwisho wa msimu.
Mike Maignan ndio kipa namba moja wa Milan kwa sasa na tangu kuanza kwa msimu huu amecheza mechi 13 za michuano yote.
Ikiwa Milan itaamua kumuuza fundi huyu Januari inaweza kuhitaji zaidi ya Pauni 20 milioni ingawa inaweza ikazidi au ikapungua kutokana na ushindani wa timu zitakazohitaji saini yake.
Juventus pia wako kwenye mbio na wanafuatilia kwa karibu mwenendo na maendeleo ya Magnan. Klabu hiyo ya Turin inamthamini sana Maignan kama mrithi anayefaa wa Michele Di Gregorio.
Lakini kwa sasa, Chelsea inaonekana kuwa mbele kwani The Blues tayari imechukua hatua za kwanza za maana na ina mradi wa michezo unaoweza kumshawishi haraka kipa huyo wa Ufaransa.
Elliot Anderson
NOTTINGHAM Forest inataka kumbakisha na kumtumia kwa msimu mzima kiungo wake wa kimataifa wa England, Elliot Anderson, 23, na haitakuwa tayari kupokea ofa yoyote katika dirisha la usajili la Januari licha ya fundi huyo kuhitajika na timu nyingi. Anderson ambaye msimu huu amecheza mechi 13 za michuano yote, akifunga mabao mawili na kutoa asisti tatu, mkataba wake wa sasa unatarajiwa kumalizika mwaka 2029. Manchester United ni kati ya klabu zinazomhusisha Anderson.
Samu Aghehowa
TOTTENHAM inamnyemelea mshambuliaji wa FC Porto na timu ya taifa ya Hispania, Samu Aghehowa, ambaye huduma yake pia inahitajika na Arsenal na Chelsea.
Kwa mujibu wa tovuti ya Caught Offside mshambuliaji huyo mwenye umri wa miaka 21, amekuwa akizivutia timu nyingi za Hispania na England tangu msimu uliopita.
Mabosi wa Porto inahitaji zaidi ya Pauni 60 milioni kwa ajili ya kumuuza.
Joe Willock
CRYSTAL Palace inapima uwezekano wa kuwasilisha ofa kwenda Newcastle United kwa ajili ya kumsajili kiungo wa klabu hiyo, Joe Willock, 26, katika dirisha lijalo.
Newcastle inaweza kukubali kumuuza Willock kwa kuwa inataka kumsajili kiungo wa AZ Alkmaar Kees Smit, 19, Januari. Mkataba wa Willock unatarajiwa kumalizika mwaka 2027 na msimu huu amecheza mechi nane za michuano yote.
Promise David
WEST Ham inaongoza mbio za kumsajili mshambuliaji wa Union Saint-Gilloise, Promise David ambaye pia anawindwa Wolves na Leeds kwa ajili ya dirisha lijalo la majira ya kiangazi.
Tangu kuanza kwa msimu huu, Promise David amefunga mabao tisa na kutoa asisti mbili katika mechi 20 za michuano yote.
Kwa mujibu wa taarifa Union inaweza kuwa tayari kumuuza kwa kiasi cha Pauni 16 milioni.
Filip Jorgensen
CHELSEA inaweza kumuuza kipa wake wa kimataifa wa Denmark, Filip Jorgensen, 23, ili kupata nafasi ya kumsajili kipa mwingine katika dirisha lijalo.
Jorgensen ambaye alijiunga na Chelsea mwaka jana akitokea Villarreal kwa takribani Pauni 20 milioni, haonekani kuaminika na kocha Enzo Maresca ambaye anahitaji kipa mwingine atakayempa changamoto Roberto Sanchez ambaye amekuwa na makosa mengi.
Aston Villa na Brighton ni miongoni mwa timu ambazo zimeonyesha nia ya kutaka kumsajili.
Jorthy Mokio
MANCHESTER United inaonekana kuwa kinara katika mbio za kuiwania saini ya beki chipukizi wa Ajax, Jorthy Mokio, mwenye umri wa 17, ambaye pia anahitajika na Tottenham na Newcastle United. Mokio ni miongoni mwa mabeki vijana wanaofanya vizuri kwa sasa katika Ligi Kuu Uholanzi. Man United inamwona kama mrithi wa Lisandro Martinez.
Mkataba wake wa sasa unatarajiwa kumalizika mwaka 2027.
Julian Alvarez
MSHAMBULIAJI wa Atletico Madrid Julian Alvarez, 25, anahitajika na timu nyingi za England, lakini rais wa klabu hiyo Enrique Cerezo amesema kwamba mshambuliaji huyo wa kimataifa wa Argentina anataka kubaki Atletico. Álvarez alijiunga na Atletico mwaka jana akitokea Man City kwa uhamisho wa Euro 70M akihitaji muda mwingi zaidi wa kucheza kikosini.