Rais FIFA kumwaga mabilioni
Muktasari:
- Kwa mujibu wa pendekezo hilo, kila chama cha soka kinapaswa kupata angalau Dola 10 milioni (Sh27 bilioni) katika kipindi cha miaka minne kuanzia 2027 hadi 2030.
ZURICH, USWIS: RAIS wa Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA), Gianni Infantino, ameagiza kufanyika kwa tathmini ya mapendekezo ya kuongeza fedha zitakazogawiwa vyama vya soka wanachama wa shirikisho hilo katika kipindi cha 2027 hadi 2030.
Hatua hiyo imekuja baada ya Shirikisho la Soka Ulaya (UEFA) na Shirikisho la Soka la Amerika Kaskazini, Kati na Caribbean (CONCACAF) kuomba FIFA itoe Dola 2.1 bilioni (Sh5.6 trilioni) kutoka kwenye akiba yake na kuzigawa kwa vyama vyake 211 wanachama.
Kwa mujibu wa pendekezo hilo, kila chama cha soka kinapaswa kupata angalau Dola 10 milioni (Sh27 bilioni) katika kipindi cha miaka minne kuanzia 2027 hadi 2030.
UEFA na CONCACAF pia zimependekeza kufanyika kwa ukaguzi huru wa akiba ya FIFA, ambayo inakadiriwa kufikia Dola 6 bilioni (Sh16 trilioni).
Mashirikisho hayo yameeleza kuwa hata baada ya FIFA kutoa Dola 2.1 bilioni, akiba yake ingeendelea kuwa zaidi ya Dola 1.5 bilioni (Sh4 trilioni), hivyo kutohatarisha uwezo wa kifedha wa taasisi hiyo.
Katika barua aliyowatumia marais wa mashirikisho sita ya mabara, Infantino amesema FIFA inahitaji kwanza kufanya tathmini ya kina kuhusu kiwango cha fedha kinachoweza kutolewa kabla ya uamuzi wa mwisho.
Infantino pia amesisitiza kuwa hakuna ahadi ya fedha hizo kutolewa hadi mapendekezo hayo yapitiwe na taratibu zote za kisheria na kiutawala zikamilike.
Tathmini hiyo itazingatia kiwango cha fedha ambacho FIFA inaweza kutoa kwa uwajibikaji, uhalali wa makadirio ya kifedha pamoja na namna ya kuhakikisha matumizi ya fedha hizo yanafanyika kwa uwazi.
Baraza la FIFA linatarajiwa kupokea mapendekezo ya awali kuhusu suala hilo ifikapo Oktoba 15, huku muda zaidi wa kufanya uchambuzi ukitarajiwa kuongezwa endapo utahitajika.
Pendekezo hilo limeibuka baada ya mpango wa awali wa FIFA wa kutafuta uwekezaji binafsi katika shughuli zake za kibiashara kukumbana na upinzani kutoka kwa baadhi ya mashirikisho ya mabara.
Infantino amekuwa akitetea mpango huo akisema ulikuwa na lengo la kuongeza mapato ya FIFA na fedha za maendeleo ya soka, badala ya kuchukua nafasi ya fedha zinazotolewa kupitia mipango iliyopo.
FIFA ilikuwa imepanga kupitia mpango wake wa FIFA Forward kuongeza fedha kwa kila chama kutoka Dola milioni nane katika kipindi cha 2023-2026 hadi Dola milioni 20 kwa kila chama katika kipindi cha 2027-2030, iwapo mpango wa kibiashara ungeidhinishwa.
Kwa sasa, mjadala mpya unalenga uwezekano wa kutumia sehemu ya akiba iliyopo ya FIFA kuongeza fedha zinazokwenda moja kwa moja kwa vyama wanachama.
FIFA ina vyama 211 wanachama vinavyotumia fedha za mipango yake kwa shughuli mbalimbali za maendeleo ya soka, ikiwamo miundombinu, timu za taifa, mashindano, makocha, soka la vijana na soka la wanawake.
Infantino amesema tathmini hiyo itasaidia kuweka msingi wa uamuzi unaozingatia uwezo wa kifedha wa FIFA pamoja na uwazi na uwajibikaji katika matumizi ya fedha.
Uamuzi wa mwisho kuhusu kiwango cha fedha kitakachotolewa na namna kitakavyogawiwa unatarajiwa kufuata baada ya mchakato huo wa tathmini na mashauriano kukamilika