Utamu mwingi wa namba Ligi Kuu England
Muktasari:
- Ingawa bado ni mapema sana, lakini msimamo wa awali wa Ligi Kuu England umeshachukua sura mpya kwenye mapumziko ya mechi za kimataifa.
LIVERPOOOL, ENGLAND: TAYARI zimeshachezwa mechi tano katika msimu wa 2026/27 wa Ligi Kuu England na kwa maaba hiyo kuna taarifa nyingi zaidi kuliko ilivyokuwa mwanzoni mwa msimu. Hivyo, utabiri wa ubingwa ukoje ikizingatiwa wababe wameshaanza kuangusha pointi na kasi ya timu ambazo haizkupewa nafasi inazidi kuongezeka.
Ingawa bado ni mapema sana, lakini msimamo wa awali wa Ligi Kuu England umeshachukua sura mpya kwenye mapumziko ya mechi za kimataifa.
Manchester City imekaa kileleni ikiwa na ushindi katika mechi zote tano, ikiwa ndiyo timu pekee yenye rekodi ya ushindi wa asilimia 100.
Arsenal, ambayo awali ilipewa nafasi kubwa zaidi kabla ya msimu kuanza iko nafasi ya pili ikiwa nyuma kwa pointi tatu, huku Brighton na Brentford ambazo zote zimeanza msimu kwa kiwango cha kuvutia zikikamilisha nne bora.
Lakini matokeo hayo ya mwanzo wa msimu yameathirije utabiri wa mwanzo kuhusu mbio za ubingwa? Hebu tuangalie.
Kwa kukumbushia tu ni kwamba Arsenal ndiyo iliyokuwa ikipewa nafasi kubwa zaidi na mifumo ya utabiri Ulaya kabla ya msimu kuanza na mathalani Opta iliipa nafasi ya asilimia 40.6 ya kutetea ubingwa wa 2025/26 kabla ya msimu kuanza.
Manchester City (asilimia 19.6) ilikuwa nafasi ya pili kwa tofauti kubwa ikifuatiwa na Liverpool (asilimia 9.2) na Manchester United (asilimia 6.6).
WANAOPEWA NAFASI KUBWA ZAIDI SASA
Licha ya kupata kichapo kikubwa kutoka kwa Brighton kabla ya mapumziko kupisha kalenda Fifa, Arsenal bado inaendelea kuwa timu inayopewa nafasi kubwa zaidi na Opta kutwaa ubingwa, ikiwa na asilimia 43.7, lakini ni kwa tofauti ndogo sana.
Manchester City (asilimia 39.8) iko nyuma yake kwa karibu. Mwanzo wake mzuri wa kushinda kila mchezo, pamoja na kipigo cha Arsenal kwa Brightoni, maana yake sasa mbio za ubingwa zimekuwa za timu mbili kwa mtazamo wa Opta badala ya kutarajiwa kuwa rahisi kwa Arsenal kama wengi walivyodhani.
Kwa pamoja, Arsenal na Manchester City zinachukua asilimia 83.4 ya nafasi zote za kutwaa ubingwa katika makadirio ya Opta
Liverpool (asilimia 5.7) ndiyo timu ya tatu inayopewa nafasi kubwa zaidi na mfumo huo. Kwa sasa haijafungwa chini ya kocha mpya Andoni Iraola, lakini imetoka sare katika mechi tatu kati ya tano ilizocheza. Kutokana na hilo, nafasi yake ya kutwaa ubingwa imeshuka kwa asilimia 3.5 kutoka asilimia 9.2 kabla ya msimu kuanza hadi asilimia 5.7 kwa sasa.
Brighton, ambayo ndiyo iliyosababisha kuanguka kwa Arsena imeanza msimu kwa kiwango cha kuvutia.
Timu hiyo ndiyo inayoongoza kwa kufunga mabao mengi kwenye ligi ikiwa na 16 ina tofauti bora zaidi ya mabao +11 na imeipa Arsenal kipigo chake cha kwanza tangu Aprili 19, 2026 yaani siku 155 zilizopita. Hii inaonekana kweli kuwa timu yenye uwezo mkubwa.
The Brighton sasa iko nafasi ya nne katika utabiri wa Opta kuhusu ubingwa, ikiwa na asilimia 4.2 ya nafasi ya kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu England ambao ungekuwa wa kushangaza.
Baada ya hapo, kuna kundi la timu kadhaa zikiwa karibu na asilimia moja. Brentford ina asilimia 1.2, Everton asilimia 1.1, Chelsea asilimia 1.0, huku Manchester United ikipewa asilimia 0.9 ya nafasi ya kutwaa ubingwa.
WALIOPANDA ZAIDI
Nafasi za Manchester City kutwaa ubingwa zimeongezeka kwa asilimia 20.2, ikiwa ni ongezeko kubwa zaidi la timu yoyote katika mechi tano za kwanza. Kama ilivyoelezwa, City ilianza msimu ikiwa timu ya pili kupewa nafasi kubwa zaidi na Opta, lakini imeanza maisha yake chini ya Enzo Maresca kwa kiwango bora kabisa.
Maresca ni kocha wa sita kushinda mechi zake tano za kwanza za Ligi Kuu England akiwa kwenye kikosi cha klabu, baada ya Carlo Ancelotti akiwa Chelsea (sita), Pep Guardiola (Man City sita), Craig Shakespeare (Leicester City tano), Maurizio Sarri (Chelsea tano) na Ole Gunnar Solskjær akiwa Manchester United (sita).
Nafasi ya Arsenal kutwaa ubingwa pia zimeongezeka kwa asilimia 3.0 kutoka makadirio yake ya kabla ya msimu. Hilo linaweza kuonekana la kushangaza kutokana na kipigo ilichopata kutoka kwa Brighton, lakini baadhi ya timu zilizokuwa miongoni mwa zinazopewa nafasi kubwa kabla ya msimu tayari zimeanza kuyumba.
Chelsea na Manchester United, kwa mfano zote zimeanza vibaya, huku Liverpool ikipoteza pointi katika mechi tatu kati ya tano za mwanzo.
Brighton ndiyo timu nyingine iliyopanda kwa kiwango kikubwa. Nafasi zake za kutwaa ubingwa zimeongezeka zaidi ya mara mbili, kutoka asilimia 2.0 hadi asilimia 4.2, kufuatia mwanzo wake bora.
WALIOSHUKA ZAIDI
Umekuwa mwanzo wa msimu wa kukatisha tamaa kwa Manchester United. Licha ya kupata pointi moja mwishoni mwa mechi dhidi ya Fulham, United imekusanya pointi tano pekee katika mechi zake tano za mwanzo za ligi, ikiwa ni idadi ndogo zaidi ya pointi ilizowahi kupata katika hatua hii ya msimu wa Ligi Kuu England ikilinganishwa na msimu wa 2014/15.
Hata hivyo, takwimu zake za msingi zinaonekana kutia moyo zaidi. United inaongoza Ligi Kuu England kwa jumla ya mashuti 113 na miguso 182 ndani ya eneo la hatari la wapinzani, lakini imeshindwa kubadilisha uwepo huo mkubwa wa mashambulizi kuwa mabao au pointi za kutosha.
Kutokana na hilo, United imeshuka kutoka nafasi ya nne kwa kupewa nafasi kubwa zaidi kabla ya msimu kuanza, wakati ilikuwa na asilimia 6.6 ya nafasi ya kutwaa ubingwa hadi asilimia 0.9 sasa. Hilo ndilo anguko kubwa zaidi kwa timu yoyote.
Aston Villa (-3.7%) pia imepata mwanzo mgumu. Ilipata ushindi wake wa kwanza wa msimu katika mechi ya tano dhidi ya Tottenham Hotspur iliyokuwa katika hali ngumu, lakini ilikuwa imepoteza mechi tatu kati ya nne za mwanzo.
Mwanzo huo wa kusuasua umetokea baada ya mabadiliko makubwa katika kikosi wakati wa kipindi cha usajili wa majira ya kiangazi.
Chelsea (-2.8%), kwa upande mwingine, ilianza msimu kwa kasi kubwa chini ya Xabi Alonso, ikifunga mabao manane katika mechi zake mbili za kwanza za ligi.
Hata hivyo, tangu hapo imecheza mechi tatu bila ushindi. Mwanzo huo usio na mwendelezo umefanya nafasi zake za kutwaa ubingwa kushuka, huku mfumo sasa ukiipa asilimia 1.0 pekee ya nafasi ya kutwaa ubingwa.
Kisha kuna Tottenham (-2.4%). Kwa mara ya kwanza tangu msimu wa 2008/09, Spurs iko mkiani mwa Ligi Kuu England baada ya mechi tano.
Katika msimu wa 2008/09, walipanda kutoka nafasi hiyo na kumaliza katika nafasi ya nane, na hiyo ni nafasi ambayo mashabiki wa Tottenham bila shaka wangeikubali katika hatua hii ya msimu wa sasa.
Bila shaka, bado safari ni ndefu. Mechi tano ni idadi ndogo ya michezo ya kutoa picha kamili, na utabiri wa Opta utaendelea kubadilika kadiri takwimu zaidi zitakavyoingizwa kwenye mfumo huo.