Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Rais FIFA awekwa kikaangoni upya

INFANTINO Pict

Muktasari:

  • Shinikizo hilo limetolewa kupitia barua ya mwenyekiti wa Chama cha Soka England (FA), Debbie Hewitt, ambaye pia ni makamu wa rais wa FIFA, akimtaka Infantino kuwasilisha nyaraka hizo kabla ya kikao kijacho cha Baraza la FIFA, Oktoba 15.

LONDON, ENGLAND: RAIS wa Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA), Gianni Infantino, amepewa shinikizo la kuweka wazi nyaraka zote zinazohusiana na mpango wake wenye utata wa kuuza sehemu ya umiliki wa haki za kibiashara za Kombe la Dunia.

Shinikizo hilo limetolewa kupitia barua ya mwenyekiti wa Chama cha Soka England (FA), Debbie Hewitt, ambaye pia ni makamu wa rais wa FIFA, akimtaka Infantino kuwasilisha nyaraka hizo kabla ya kikao kijacho cha Baraza la FIFA, Oktoba 15.

Hewitt pia ameitaka FIFA kutoa maelezo ya maandishi kwa wajumbe wa baraza hilo kuhusu uamuzi wa kusitisha adhabu ya mshambuliaji wa Marekani, Folarin Balogun, katika Kombe la Dunia.

Barua hiyo, ambayo pia imetumwa kwa Katibu Mkuu wa FIFA, Mattias Grafstrom, inaibua tuhuma za mapungufu katika uongozi na kudorora kwa utamaduni wa kiutendaji ndani ya chombo hicho kinachosimamia soka duniani.

INFA 01

Infantino amekuwa akikabiliwa na shinikizo linaloongezeka kufuatia mpango wake uliositishwa wa kampuni ya Fifa Forward Enterprise (FFE), iliyopendekezwa kusimamia haki za kibiashara na tiketi za mashindano yote ya FIFA, likiwemo Kombe la Dunia.

Mpango huo ulilenga kuanzisha kampuni mpya na kuuza asilimia 21 ya hisa zake kwa kampuni binafsi ya uwekezaji. Hata hivyo, ulisitishwa baada ya kupata upinzani mkubwa kutoka kwa vyama vya soka vya kitaifa.

Katika barua yake, Hewitt amependekeza pia kufanyika kwa uchunguzi huru utakaobaini namna mpango huo ulivyoanzishwa, waliohusika kuubuni na mchakato uliotumika kumpata mwekezaji binafsi.

Mwezi uliopita, UEFA ilianza kuandaa hatua za kisheria za jinai dhidi ya Infantino katika mahakama tatu za Marekani kuhusu mpango wa FFE, huku ikitaka nyaraka zote zinazohusiana na mpango huo ziwekwe wazi.

INFA 02

FIFA ilijibu kwa kuishutumu UEFA kwa kuendesha kampeni ya kuichafua taasisi hiyo na uongozi wake, kupitia pingamizi lake dhidi ya kesi hiyo.

Infantino, mwenye umri wa miaka 56, anatarajiwa kugombea urais wa FIFA kwa mara ya nne mwezi Machi, huku wapinzani wake wakiwa na hadi Novemba 18 kupata mgombea mbadala.


KISA BALOGUN CHAZIDISHA MASHAKA FA

Chama cha Soka England (FA) kilianza kuwa na wasiwasi kuhusu suala la Balogun tangu mwanzo na kilikuwa kimeomba kupewa nyaraka za uamuzi wa kuondoa adhabu yake ya kusimamishwa kucheza katika Kombe la Dunia.

Balogun, mwenye umri wa miaka 25, aliruhusiwa kucheza dhidi ya Ubelgiji katika hatua ya 16 bora, licha ya kutarajiwa kutumikia adhabu ya kutocheza mechi moja.

Mshambuliaji huyo alionyeshwa kadi nyekundu ya moja kwa moja baada ya kumchezea vibaya beki Tarik Muharemovic katika ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Bosnia na Herzegovina, hatua ya 32 bora.

Baadaye FIFA ilitangaza kuwa adhabu ya moja kwa moja ya kutocheza mechi moja ingesitishwa kwa kipindi cha mwaka mmoja. Hakukuwa na maelezo ya kina yaliyotolewa kuhusu uamuzi huo, isipokuwa kurejea kanuni inayoruhusu adhabu kusitishwa.

FA, ambayo ilikuwa imetuma barua ya kumuunga mkono Infantino katika uchaguzi wake wa kuwania muhula mwingine kabla ya tukio hilo, ilianza kuwa na wasiwasi mkubwa kuhusu uwezekano wa kuingiliwa kisiasa katika uamuzi huo.

INFA 03

Rais wa Marekani, Donald Trump, baadaye alithibitisha kuwa alimpigia simu Infantino na kumtaka suala la adhabu ya Balogun lipitiwe upya.

Baada ya hapo, mpango wa FFE uliofichuliwa na vyombo vya habari siku chache baada ya fainali ya Kombe la Dunia ulizidisha mgawanyiko katika soka la kimataifa.

Mwezi uliopita, UEFA, Concacaf na Shirikisho la Soka la Asia (AFC) zilimshutumu FIFA na Infantino kwa kuvunja imani kupitia kile walichokiita udanganyifu, katika barua ya wazi iliyotolewa kwa pamoja.

Vyama kadhaa vya soka vya kitaifa, vikiwemo vya England, Wales na Scotland, vimeondoa barua zao za kumuunga mkono Infantino katika uchaguzi wake wa urais.

Hata hivyo, Infantino bado anaungwa mkono na sehemu kubwa ya jumuiya ya soka duniani, huku mashirikisho ya Afrika, Amerika Kusini na Oceania yakisisitiza tena kumuunga mkono.

Baada ya mpango wa FFE kufutwa, Infantino aliitisha kikao cha bodi ya uongozi wa FIFA mjini Rabat, Morocco.

Hadi sasa, hakuna mawasiliano rasmi yaliyofanyika na Baraza la FIFA kwa ajili ya kutoa ufafanuzi kuhusu mpango huo wenye utata.

Hali hiyo inatarajiwa kubadilika mwezi ujao, wakati Infantino atakapokutana na Hewitt pamoja na wajumbe wengine 35 wa Baraza la FIFA katika kikao cha Oktoba 15.