TFF yaweka mezani mpango wa timu za taifa
Muktasari:
- Kwa upande wa Ngorongoro Heroes, Ndimbo amesema timu hiyo ipo kwenye mashindano ya kufuzu AFCON U20 kwa kanda ya CECAFA na tayari imeanza kwa ushindi dhidi ya Rwanda huku mchezo unaofuata ukiwa ni dhidi ya Ethiopia kwenye Uwanja wa Uhuru.
SHIRIKISHO la Soka Tanzania (TFF) limeweka ratiba na mipango ya timu mbalimbali za taifa zinazokabiliwa na mashindano ya kimataifa huku Taifa Stars ikiwa na michezo miwili ya kufuzu AFCON 2027 na Serengeti Boys ikiendelea na maandalizi ya Kombe la Dunia nchini Qatar.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, Ofisa habari na mawasiliano wa TFF, Clifford Ndimbo, amesema siku chache zijazo zitakuwa na shughuli nyingi kwa timu za taifa kuanzia vijana, wanawake hadi timu ya wakubwa.
Kwa upande wa Ngorongoro Heroes, Ndimbo amesema timu hiyo ipo kwenye mashindano ya kufuzu AFCON U20 kwa kanda ya CECAFA na tayari imeanza kwa ushindi dhidi ya Rwanda huku mchezo unaofuata ukiwa ni dhidi ya Ethiopia kwenye Uwanja wa Uhuru.
Ndimbo amesema Ngorongoro Heroes inaingia kwenye mashindano hayo ikiwa na hadhi ya kuwa mabingwa watetezi.
“Tunaendelea kuwaomba Watanzania kuiunga mkono timu yetu hii ili kuweza kuipata tiketi hiyo ya kufuzu AFCON ya chini ya miaka 20,” amesema Ndimbo.
Wakati Ngorongoro Heroes ikiendelea na kibarua chake, timu ya taifa ya Futsal nayo ipo kwenye maandalizi ya AFCON 2026 itakayofanyika Morocco huku Ndimbo akieleza kuwa kikosi hicho kinatarajiwa kwenda nchini humo Oktoba Mosi kwa ajili ya kuweka kambi na kucheza michezo kadhaa ya kirafiki.
Kwa upande wa Beach Soccer, TFF imeweka wazi kuwa timu hiyo itakutana na Msumbiji katika hatua ya kufuzu AFCON ambapo mchezo wa kwanza unatarajiwa kufanyika Dar es Salaam Oktoba 11, kabla ya mchezo wa marudiano kuchezwa Maputo kati ya Oktoba 16 na 18.
“Tayari tumekwisha cheza hiyo AFCON ya Beach Soccer takribani mara tatu hivi. Kwa hiyo nia yetu ni kuhakikisha kwamba tunaendelea kufanya vizuri na kuendelea kushiriki mashindano hayo makubwa barani Afrika,” amesema Ndimbo.
Kwa Serengeti Boys, maandalizi yanaendelea ya Kombe la Dunia la U-17 litakaloanza Novemba 19 nchini Qatar huku TFF ikiendelea na mpango wa kuipeleka timu hiyo England kwa kambi ya nje ya nchi.
Ndimbo amesema endapo mipango hiyo itakamilika, Serengeti Boys itakuwa England kuanzia Septemba 28 na inatarajiwa kucheza takribani michezo minne ya kirafiki kama sehemu ya maandalizi ya mashindano hayo.
“Taratibu zote sasa zinaendelea kuhakikisha kwamba kikosi hicho kinapata nafasi ya hiyo kambi ya nje. Pale ambako itakuwa imekaa sawasawa, tutawapa taarifa ya kwamba kikosi kitaondoka lini kuelekea kwenye hiyo kambi ya nje,” amesema.
Kwa upande wa wanawake, TFF imeeleza kuwa timu ya taifa itakutana na Botswana katika hatua ya kufuzu Michezo ya Olimpiki ambapo mchezo wa kwanza utafanyika Botswana Oktoba 9 na marudiano yatafanyika Oktoba 13.
Wakati huo huo, Timu ya Taifa ya U23 inaanza kambi kwa ajili ya michezo miwili dhidi ya Kenya katika harakati za kufuzu AFCON U23.
Ndimbo amesema mchezo wa kwanza utachezwa Uwanja wa Nyayo, Kenya, Septemba 28 saa 9:00 alasiri, kabla ya Tanzania kuwa mwenyeji wa mchezo wa marudiano Oktoba 10 kwenye Uwanja wa Uhuru kuanzia saa 10:00 jioni.
Kwenye kikosi cha wakubwa, Taifa Stars kinatarajiwa kuingia kambini kujiandaa na michezo ya kufuzu AFCON dhidi ya Guinea Bissau na Madagascar, pamoja na mchezo wa kirafiki wa kimataifa dhidi ya Ghana.
Ndimbo amesema Stars itaanza mazoezi kwenye Uwanja wa Gymkhana huku TFF ikiandaa matukio mawili maalumu ya kuongeza ushiriki wa waandishi na mashabiki katika maandalizi ya timu hiyo.
Septemba 21 imepangwa kuwa Media Open Day, itakayowapa waandishi nafasi ya kufanya mahojiano na wachezaji pamoja na benchi la ufundi, wakati Septemba 23 kutakuwa na Mashabiki Open Day, ambapo mashabiki wataruhusiwa kushuhudia mazoezi na kupata nafasi ya kupiga picha na wachezaji pamoja na benchi la ufundi.
Ndimbo amesema mchezo wa kwanza wa Taifa Stars utakuwa dhidi ya Guinea-Bissau Septemba 25 kwenye Uwanja wa Amani, Zanzibar, saa 10:00 jioni.
Baada ya mchezo huo, Stars inatarajiwa kuondoka Septemba 26 kuelekea Casablanca, Morocco, ambako itakutana na Madagascar Septemba 29 katika mchezo wa kufuzu AFCON, kabla ya kuvaana na Ghana katika mchezo wa kirafiki wa kimataifa Oktoba 4.