Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

UEFA yamvuta Infantino mahakamani

INFANTINO Pict
INFANTINO Pict

Muktasari:

  • Kwa mujibu wa nyaraka za mahakama, UEFA imewasilisha ombi la kupata ushahidi na nyaraka ambazo inataka kuzitumia katika hatua za kisheria nchini Uswisi dhidi ya Infantino, ikimtuhumu kwa “usimamizi mbaya wa jinai”.

ZURICH, USWISI: SHIRIKISHO la Soka Ulaya (UEFA) limeanza mchakato wa kisheria unaoweza kufungua mashtaka ya jinai dhidi ya Rais wa FIFA, Gianni Infantino kutokana na mpango wake uliositishwa wa kuuza hisa katika mashindano ya Kombe la Dunia na michuano mingine ya FIFA kwa wawekezaji binafsi.

Kwa mujibu wa nyaraka za mahakama, UEFA imewasilisha ombi la kupata ushahidi na nyaraka ambazo inataka kuzitumia katika hatua za kisheria nchini Uswisi dhidi ya Infantino, ikimtuhumu kwa “usimamizi mbaya wa jinai”.

Mpango huo ulihusisha kuanzishwa kwa kampuni mpya iliyojulikana kama FIFA Forward Enterprise (FFE), ambayo ingekuwa na jukumu la kusimamia haki za kibiashara za mashindano ya FIFA, huku sehemu ya umiliki ikiuzwa kwa wawekezaji binafsi.

Hata hivyo, mpango huo ulisitishwa Agosti 1 baada ya kukabiliwa na upinzani mkubwa kutoka ndani na nje ya FIFA.

UEFA inadai kuwa Infantino aliendesha mpango huo kwa usiri, bila kuwashirikisha ipasavyo wadau muhimu wa soka, na kwamba muundo wake ungeweza kumnufaisha yeye binafsi pamoja na kundi dogo la wawekezaji.

Katika nyaraka zake, UEFA imehoji pia thamani iliyowekwa kwenye mpango huo, ikisema haikuthibitishwa na mthamini huru wala kuamuliwa kupitia ushindani wa wazi.

Kwa mujibu wa mpango huo, wawekezaji walitarajiwa kulipa Dola 4.2bilioni  kwa asilimia 20 ya kampuni hiyo mpya, jambo ambalo UEFA inaliona kama tathmini ya chini isiyokuwa na uhalali wa kibiashara.

UEFA YATAKA NYARAKA ZA FIFA

Katika hatua ya kwanza, UEFA imeomba mahakama ya Marekani iruhusu ipate nyaraka na ushahidi kutoka kwa kampuni mbili za FIFA zilizopo Florida, FIFA (AMERICAS), Inc. na FWC2026 US, Inc.

Nyaraka hizo zinatafutwa kwa lengo la kutumika baadaye katika mchakato wa kisheria nchini Uswisi. UEFA inaamini kampuni hizo zina taarifa muhimu kuhusu namna mpango wa FFE ulivyoanzishwa, ulivyopangwa, ulivyothaminiwa na kuidhinishwa.

UEFA pia imesema inaamini vyama vyake 55 vya soka barani Ulaya vingeweza kuathirika kutokana na mpango huo.

Shirikisho hilo limeonya kwamba hatua za kisheria huenda zisilenge Infantino pekee, bali pia maofisa wengine wa FIFA na washauri waliohusika katika mpango huo.

MPANGO ULIOZUA MGOGORO

Mpango wa FFE ulitangazwa mwishoni mwa Julai na ulilenga kuunda kampuni mpya ya kibiashara ambayo ingeweza kuuza sehemu ya umiliki kwa wawekezaji binafsi.

Thrive Eternal, kampuni inayohusishwa na Joshua Kushner, ilitajwa kuwa mwekezaji mkuu aliyekuwa akitarajiwa kuhusika katika mpango huo.

Mpango huo ulikumbana na upinzani mkali kutoka UEFA pamoja na wadau wengine wa soka, hali iliyosababisha FIFA kuamua kuusitisha.

Baada ya mpango huo kufutwa, uongozi wa FIFA ulikiri kuwa kulikuwa na makosa katika namna suala hilo lilivyoshughulikiwa na ukaahidi kuboresha taratibu za utawala na mawasiliano.

Sasa UEFA imeongeza presha kwa Infantino, huku ikiandaa uwezekano wa kufikisha malalamiko ya jinai katika mahakama za Uswisi kuhusu madai ya usimamizi mbaya wa mali na maslahi ya FIFA.

Hata hivyo, hatua hiyo bado iko katika maandalizi na haimaanishi kuwa Infantino amepatikana na hatia; UEFA kwa sasa inatafuta ushahidi na nyaraka kwa ajili ya mchakato unaotarajiwa.