Wizara yapiga 'stop' jezi za Stars, TFF ikitia neno
Muktasari:
- Taarifa hiyo iliyotolewa leo, Septemba 18, 2026 imeeleza kuwa Wizara haikushirikishwa katika mchakato huo, hivyo haitambui jezi hizo ambazo siku chache zilizopita zilitangazwa na naibu wake, Hamis Mohamed Mwinjuma 'Mwana FA'.
WIZARA ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo imesema haitambui matangazo ya jezi mpya za timu za taifa za soka , ikieleza kuwa mchakato wa kuzibadilisha haukuishirikisha Wizara licha ya maelekezo yaliyotolewa Februari mwaka huu.
Taarifa hiyo iliyotolewa leo, Septemba 18, 2026 imeeleza kuwa Wizara haikushirikishwa katika mchakato huo, hivyo haitambui jezi hizo ambazo siku chache zilizopita zilitangazwa na naibu wake, Hamis Mohamed Mwinjuma 'Mwana FA'.
“Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo inapenda kutoa ufafanuzi kuwa, Paul Christian Makonda, Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, hatambui matangazo ya Jezi za Timu za Taifa kutokana na mchakato wa kuzibadilisha jezi hizo kutoishirikisha Wizara licha ya maelekezo aliyoyatoa mwezi Februari 2026,” imefafanua taarifa hiyo.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, Makonda alitoa maelekezo Februari 2026 kwamba, kutokana na Serikali kuwekeza fedha nyingi katika maandalizi ya timu za taifa zinazoshiriki mashindano ya kimataifa, kulikuwa na haja ya kuboresha jezi hizo ili ziakisi manufaa mapana kwa nchi.
Wizara imeongeza kuwa umuhimu wa kuboresha jezi hizo unaongezeka kutokana na Tanzania kuwa mwenyeji wa mashindano makubwa ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) mwaka 2027, hivyo suala la mwonekano na utambulisho wa timu za taifa linapaswa kupewa uzito.
Katika taarifa hiyo, Wizara imesema pamoja na kutotambua utambulisho wa jezi hizo, Waziri Makonda ataunda Kamati ya kuchunguza mkataba wa mzabuni wa jezi, hatua inayolenga kubaini manufaa ya mkataba huo kwa timu za taifa.
“Waziri Makonda ataunda Kamati ya kuchunguza mkataba wa mzabuni wa jezi hizo ili kubaini manufaa ya mkataba huo kwa timu za taifa ambazo zimekuwa zikigharamiwa na Serikali kwa fedha nyingi licha ya uwepo wa fursa ya mauzo ya jezi yanayopaswa kuchangia katika uendeshaji wa timu za taifa,” imefafanua taarifa ya wizara.
Hoja hiyo imekuja wakati kukiwa na mjadala kuhusu upatikanaji na matumizi ya jezi za timu za taifa huku Wizara ikitaka pia kuangaliwa namna mauzo ya jezi yanavyoweza kuwa sehemu ya kuchangia uendeshaji wa timu hizo.
Taarifa ya Wizara imeibuka baada ya picha za jezi hizo kusambaa kwenye mitandao ya kijamii na kuzua maswali kuhusu utambulisho wake, mchakato wa kuzibadilisha na namna zilivyoidhinishwa.
Awali, Ofisa Habari na Mawasiliano wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Clifford Mario Ndimbo, alipoulizwa kuhusu suala hilo katika mkutano na waandishi wa habari, alisema timu za taifa hazijawahi kukosa mavazi.
“Timu ya taifa haijawahi kukosa mavazi. Siku zote tumekuwa tunatumia jezi ambazo zinatumika mara zote,” amesema Ndimbo.
Ndimbo pia alisema suala lililokuwa likijadiliwa mitandaoni halikuwa jambo ambalo TFF ilitaka kulizungumzia kwa undani wakati huo, akieleza kuwa lilikuwa likishughulikiwa na mamlaka za juu.
“Kwa hiyo suala hilo ambalo lipo mtandaoni tusingependa sana kulizungumza. Linaendelea huko mtandaoni lakini linafanyiwa kazi na mamlaka za juu,” amesema.
Alipoulizwa iwapo Watanzania wataweza kuzipata jezi hizo kwa kuuzwa kwenye maduka, Ndimbo hakutoa muda wala utaratibu wa moja kwa moja wa upatikanaji wake, bali alisisitiza kuwa suala hilo linafanyiwa kazi na mamlaka za juu.