Infantino aanikwa, saini 100,000 zadai aondoke FIFA
Muktasari:
- Hadi juzi usiku zaidi ya watu 100,000 wanadaiwa kusajili majina na saini zao kwenye malalamiko dhidi yake wakidai kwamba kiongozi huyo wa juu wa soka duniani amekuwa akitumia vibaya madaraka yake, amekiuka wajibu kwa kutokuwa na upande wa kisiasa na pia kutokuwa mwaminifu kwa shirikisho hilo kupitia uhusiano wake na rais wa Marekani, Donald Trump.
ZURICH, USWISI: KAMPENI ya kutaka kumng'oa rais wa Shirikisho la Soka Duniani (Fifa), Gianni Infantino imeingia katika hatua nyingine Ulaya ambako harakati za kutaka kumshtaki kiongozi huyo zinaendelea, huku pia zikikusanywa saini kutoka kwa watu mbalimbali ili kuongeza shinikizo kutaka aachie madarakani.
Hadi juzi usiku zaidi ya watu 100,000 wanadaiwa kusajili majina na saini zao kwenye malalamiko dhidi yake wakidai kwamba kiongozi huyo wa juu wa soka duniani amekuwa akitumia vibaya madaraka yake, amekiuka wajibu kwa kutokuwa na upande wa kisiasa na pia kutokuwa mwaminifu kwa shirikisho hilo kupitia uhusiano wake na rais wa Marekani, Donald Trump.
Kampeni ya Reboot Fifa iliyoanzishwa kabla ya Kombe la Dunia 2026 ikiwa na lengo la kuwasilisha malalamiko ambayo Fifa imewahi kuyapokea ikilenga kile waandaaji wanachodai kuwa ni upungufu katika utawala kwenye taasisi hiyo, kwa sasa imeshika kasi na lolote linaweza kutokea.
Kampeni hiyo imeamua kupanua madai yake ikijumuisha pia kubatilishwa kwa adhabu ya uwanjani dhidi ya straika wa Marekani, Folarin Balogun wakati wa mashindano ya Kombe la Dunia 2026, kufuatia tukio lililomzawadia kadi nyekundu katika mchezo dhidi ya Bosnia and Herzegovina ambayo ingemfanya akose mchezo dhidi ya Ubelgiji. Adhabu hiyo ilifutwa baada ya Trump kuwasiliana na Infantino.
Pia, waandaaji wa Reboot Fifa wametaja makosa mengine ya Infantino kuwa ni sakata la Fifa Forward Enterprise (FFE), mpango uliolenga kuuza sehemu ya haki za mashindano yaliyopo chini ya shirikisho hilo kwa wawekezaji binafsi, sambamba na kitendo cha bosi huyo wa Fifa kumpa tuzo ya amani Rais Trump.
Ingawa mpango wa FFE ambao ulishasitishwa na Infantino kuomba radhi, lakini mashirikisho mengi ya Ulaya yamekomaa yakitaka aachie ngazi haraka na kwamba, asipofanya hivyo watatumia njia za kisheria ambazo tayari zimeshaanza kwa hatua za awali za uchunguzi.
Vilevile wanamtuhumu Infantino kushiriki katika Bodi ya Amani ya Trump kuhusu Mashariki ya Kati, suala ambalo ni sawa na kuliingiza soka katika mambo yasiyohusiana na mchezo huo, na katika hilo kuna kile kinachodaiwa ni ahadi ya Infantino kushirikiana na Trump kuifanya siyo Marekani pekee kuwa kubwa tena, bali dunia nzima.
Juzi, malalamiko manane dhidi ya Infantino yaliyoambatana na saini za watu 100,000 yaliwasilishwa katika Kamati ya Maadili ya Fifa, ambapo waandaaji wa Reboot Fifa na shirika moja la kutetea haki linalojiita Fair Square wameitaka kuchukua hatua wakikumbushia pia madai waliyowasilishwa Desemba, mwaka jana ambayo hayakupata majibu kutoka kwa kamati hiyo. Kwa pamoja malalamiko hayo na yale ya awali yanaungwa mkono na wabunge 50 wa Bunge la Ulaya.
Ikizungumzia malalamiko hayo Fair Square ilisema katika barua yake: “Ukweli kwamba watu 100,000 wameongeza majina yao kwenye wito huu wa uwajibikaji ni ushahidi wa wazi wa kuongezeka kwa wasiwasi wa umma.”
Shirika hilo limeongeza kwamba Kamati ya Maadili ya Fifa ambayo ni chombo huru cha kimahakama chenye jukumu muhimu la kulinda uadilifu na heshima ya soka haipaswi kuchukua hatua tu, bali kuonekana ikifanya hivyo kwa haraka, uwazi na umakini unaostahili.
Hata hivyo, Fifa ilipoombwa kutoa maoni na baadhi ya vyombo vya habari jana kuhusu madai hayo ilirejea kwenye taarifa iliyochapisha mwezi uliopita ambayo ilisema: “Inazidi kuwa wazi kwamba kuna juhudi zilizoratibiwa na zinazoendelea kutoka kwa baadhi ya watu za kuidhoofisha Fifa na rais wake. Wale ambao hawaungwi mkono na vyama wanachama vya Fifa hawapaswi kujaribu kufanikisha kupitia madai, kashfa au taarifa potofu kile ambacho hawawezi kukipata kupitia taratibu za kidemokrasia zilizowekwa na Fifa.”
MUHULA WA NNE
Jumapili iliyopita Fifa ilithibitisha kwamba Infantino atagombea tena urais wa shirikisho hilo katika uchagu mkuu utakaofanyika mwakani akilenga kulitumikia kwa muhula wa nne na wa mwisho.
Uamuzi huo unakuja wakati Infantino akikabiliwa na shinikizo kutoka Uefa, pamoja na ukosoaji ndani ya Shirikisho la Soka la Asia na Concacaf, linalosimamia soka la Amerika Kaskazini, Amerika ya Kati na Carribean.
Uefa tayari imemtaka Infantino aachie madaraka, huku hivi karibuni ikitangaza kwamba inakusudia kufungua madai ya jinai nchini Marekani kuhusiana na mipango ya FFE.