Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Rais al hilal afichua sababu ya kuidhamini Kagame

Muktasari:

  • Udhamini kati ya Al Hilal, CECAFA na Shirikisho la Soka Rwanda (FERWAFA), utashuhudia klabu hiyo ikitoa dola 100,000 kila mwaka kwa kipindi cha miaka mitatu kuanzia 2026 hadi 2028.

RAIS wa Al Hilal Omdurman ya Sudan, Yasir Hassan, amesema sababu kubwa iliyowafanya kuwekeza dola 300,000 (zaidi ya Sh800 milioni) kudhamini Kombe la CECAFA Kagame kwa miaka mitatu si kutangaza jina la klabu yao pekee, bali kusaidia kukuza soka la Afrika Mashariki na Kati.

Udhamini kati ya Al Hilal, CECAFA na Shirikisho la Soka Rwanda (FERWAFA), utashuhudia klabu hiyo ikitoa dola 100,000 kila mwaka kwa kipindi cha miaka mitatu kuanzia 2026 hadi 2028.

Hassan alisema Al Hilal imekuwa ikiamini kuwa mashindano ya kikanda ndiyo msingi wa kujenga klabu imara, kuibua vipaji na kuongeza ushindani wa soka barani Afrika.

“Al Hilal inaamini nguvu ya mashindano ya kikanda katika kukuza mchezo na kujenga klabu zenye ushindani. Kombe la CECAFA Kagame lina nafasi muhimu katika kuendeleza vipaji na kuongeza kiwango cha ushindani katika Afrika Mashariki na Kati, hivyo tunajivunia kuwa sehemu ya safari hiyo,” alisema Hassan.

Mbali na hilo, Hassan alisema uamuzi wa kuwekeza kwenye mashindano hayo umechochewa pia na namna Rwanda ilivyoonyesha uwezo mkubwa wa kuandaa matukio ya kimataifa.

“Rwanda imeonyesha weledi, maandalizi bora na miundombinu ya kisasa. Kusaidia mashindano yanayoandaliwa hapa kunakwenda sambamba na maono yetu ya kuona soka la Afrika linafikia viwango vya juu zaidi,” alisema.

Kwa mujibu wa makubaliano hayo, Al Hilal imekuwa mdhamini mkuu wa Kombe la CECAFA Kagame kwa miaka mitatu ijayo, hatua inayotarajiwa kuongeza utulivu wa kifedha kwa mashindano hayo ambayo katika miaka ya karibuni yamekuwa yakikabiliwa na changamoto za udhamini.

Rais wa FERWAFA, Fabrice Shema, alisema ushirikiano huo ni uthibitisho wa imani ambayo taasisi na klabu kubwa za Afrika zimekuwa nazo kwa Rwanda katika kuandaa mashindano ya kimataifa.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa muda wa CECAFA, Jean Sseninde, alisema udhamini huo utaisaidia taasisi hiyo kupanga mashindano kwa utulivu zaidi huku ukiongeza ushindani na ubora wa Kombe la Kagame.