Okwi alitamani Simba icheze fainali ya Kagame
Muktasari:
- Okwi ambaye aliwahi kuwa mmoja wa nyota waliowika Msimbazi, alisema Simba ilikuwa na kikosi chenye uwezo wa kufika mbali, lakini mabadiliko yaliyofanywa msimu huu yanahitaji muda kabla ya timu kufikia kiwango chake halisi.
MSHAMBULIAJI wa zamani wa Simba SC, Emmanuel Okwi, amesema alitamani kuiona timu hiyo ikifika fainali ya Kombe la CECAFA Kagame 2026, lakini anaamini michuano hiyo imekuwa hatua muhimu kwa benchi la ufundi kujenga kikosi kipya kuelekea msimu ujao.
Okwi ambaye aliwahi kuwa mmoja wa nyota waliowika Msimbazi, alisema Simba ilikuwa na kikosi chenye uwezo wa kufika mbali, lakini mabadiliko yaliyofanywa msimu huu yanahitaji muda kabla ya timu kufikia kiwango chake halisi.
“Kwa kweli nilitamani Simba icheze fainali kwa sababu ni timu yangu ya zamani na nina mashabiki wengi Tanzania. Lakini wakati mwingine kwenye soka mambo hayaendi kama unavyotamani,” alisema Okwi.
Nyota huyo wa Uganda alisema haoni sababu ya mashabiki kuwa na hofu kubwa kwa kuwa michuano ya Kagame imekuwa sehemu ya maandalizi ya msimu mpya.
“Nimeona Simba ndio ina wachezaji kadhaa wapya. Timu kama hii inahitaji muda wa kucheza pamoja ili kila mmoja aelewe mfumo na wenzake. Nafikiri watakuwa bora zaidi kadri muda unavyokwenda,” alisema.
Kauli ya Okwi inaendana na ile ya kocha wa Simba, Steve Barker ambaye alisema licha ya kutofuzu nusu fainali, amefurahishwa na maendeleo ambayo timu yake imeonyesha ndani ya kipindi kifupi cha maandalizi.
Barker alisema kikosi chake kilianza maandalizi rasmi siku chache kabla ya mashindano na CECAFA Kagame imekuwa sehemu muhimu ya kupima uwezo wa wachezaji wapya na kujenga mfumo anaoutaka.
Simba ilimaliza hatua ya makundi ya Kombe la CECAFA Kagame ikiwa na pointi tano baada ya kutoka sare mbili dhidi ya Mogadishu City na Jamus SC, kabla ya kuifunga Singida Black Stars mabao 2-1, matokeo ambayo hayakutosha kuifikisha hatua ya nusu fainali.