Nahodha wa Jamus avutiwa na Ligi Kuu
Muktasari:
- Muhire, ambaye ni raia wa Rwanda, alisema kufuatilia kwa karibu timu za Tanzania kwenye Kombe la CECAFA Kagame kumempa picha halisi ya maendeleo ya soka la nchi hiyo.
NAHODHA wa Jamus SC ya Sudan Kusini, Kevin Muhire, amesema amevutiwa na kiwango cha ushindani wa Ligi Kuu Bara (NBC Premier League), akieleza kuwa ni moja ya ligi zinazozidi kukua barani Afrika kutokana na uwekezaji mkubwa unaofanywa na klabu zake.
Muhire, ambaye ni raia wa Rwanda, alisema kufuatilia kwa karibu timu za Tanzania kwenye Kombe la CECAFA Kagame kumempa picha halisi ya maendeleo ya soka la nchi hiyo.
“Ligi ya Tanzania ni nzuri sana, ina ushindani mkubwa na timu zake zinawekeza kwa kiwango kikubwa ndiyo maana kila msimu unaona zinashindana vizuri kwenye mashindano ya CAF,” alisema Muhire.
Kiungo huyo alisema Simba na Singida Black Stars zilionyesha ubora mkubwa licha ya kushindwa kufuzu hatua ya nusu fainali ya Kagame, akisisitiza kuwa matokeo ya michuano ya maandalizi hayaondoi ubora wa ligi hiyo.
“Tulicheza dhidi ya Simba na ilikuwa mechi ngumu sana. Unaweza kuona ubora wa wachezaji na kiwango cha ushindani walichonacho,” alisema.
Kelvin jana, Jumanne alikuwa mzigoni kupigania timu yake kutinga fainali ya michuano hiyo ambayo inafanyika kwenye ardhi ya nyumbani kwao Rwanda.