Vipers yajivunia maandalizi bora licha ya kutolewa CECAFA Kagame
Muktasari:
- Vipers ilimaliza nafasi ya pili Kundi A baada ya kuzifunga Garde Republicaine ya Djibouti na Gor Mahia ya Kenya, lakini ikashindwa kufuzu nusu fainali kufuatia kupoteza mchezo wake dhidi ya APR FC ya Rwanda.
KOCHA wa Vipers SC ya Uganda, Denis Lavagne, amesema licha ya timu yake kuishia hatua ya makundi ya Kombe la CECAFA Kagame 2026, mashindano hayo yamekuwa sehemu muhimu ya maandalizi kuelekea msimu mpya na ushiriki wao katika Ligi ya Mabingwa Afrika.
Vipers ilimaliza nafasi ya pili Kundi A baada ya kuzifunga Garde Republicaine ya Djibouti na Gor Mahia ya Kenya, lakini ikashindwa kufuzu nusu fainali kufuatia kupoteza mchezo wake dhidi ya APR FC ya Rwanda.
Lavagne alisema lengo kubwa la timu yake lilikuwa kupata mechi za ushindani na kuwapa nafasi wachezaji wengi kujionyesha kabla ya msimu mpya kuanza.
“Mashindano haya yametusaidia kujiandaa vizuri kwa sababu tupo kwenye kipindi cha maandalizi ya msimu mpya. Tumeweza kuwapa nafasi wachezaji wengi kucheza katika kiwango cha kimataifa huku tukijiandaa pia kwa Ligi ya Mabingwa Afrika,” alisema Lavagne.
Kocha huyo alisema mechi za CECAFA Kagame zimewapa picha halisi ya maeneo ambayo wanapaswa kuyaboresha kabla ya kuanza kwa mashindano rasmi.
Wakati Vipers ikirejea nyumbani kuendelea na maandalizi, Kombe la CECAFA Kagame liliendelea jana, Jumanne kwa hatua ya nusu fainali, ambapo Al Hilal ya Sudan ilicheza na Gor Mahia ya Kenya huku Rayon Sports ya Rwanda ikichuana na Jamus SC ya Sudan Kusini kusaka tiketi ya kucheza fainali.
Bingwa wa mashindano hayo ataondoka na kitita cha dola 30,000, mshindi wa pili atapata dola 20,000 huku timu itakayomaliza katika nafasi ya tatu ikizawadiwa dola 10,000.