Radi, Joto, mvua zaleta shida Kombe la Dunia

Muktasari:
- Licha ya muda kwa baadhi ya michezo kutokuwa rafiki kwa mashabiki wa soka ikiwamo hapa nchini, lakini tatizo kubwa kwa timu shiriki kwa kipindi hiki ni hali ya hewa na hilo limesababisha kuvurugika kwa ratiba na kuchelewa au kuanza kwa mechi.
FLORIDA, MAREKANI: MICHUANO ya Kombe la Dunia kwa Klabu la Fifa inaendelea Marekani katika miji tofauti ikiwa ni hatua ya makundi. Hata hivyo, michauno hiyo ambayo imekuja katika mfumo mpya baada ya timu kuongezwa kutoka sita hadi 32, imeanza kwa misukosuko baada ya kukumbwa na dosari na kusababisha kupoteza msisimko na ladha iliyokuwa ikisubiriwa na wengi.
Licha ya muda kwa baadhi ya michezo kutokuwa rafiki kwa mashabiki wa soka ikiwamo hapa nchini, lakini tatizo kubwa kwa timu shiriki kwa kipindi hiki ni hali ya hewa na hilo limesababisha kuvurugika kwa ratiba na kuchelewa au kuanza kwa mechi.
Hali ya hewa ya jua kali katika baadhi ya michezo imeleta athari mbalimbali na hapa tunakuchambulia yaliyotokea kutokana na hali hiyo mbaya ya hewa na majibu ya Shirikisho la Soka Duniani (Fifa) juu ya athari hizo.

MECHI ZILIZOATHIRIWA
Hadi sasa katika fainali hizi, mechi nne zimecheleweshwa kutokana na hali mbaya ya hewa ambayo ni mvua, radi na joto kali.
Mamelodi Sundowns dhidi ya Ulsan HD ndiyo mechi ya kwanza kuathiriwa na ikasimama kwa zaidi ya saa moja kutokana na dhoruba kali lililoambatana na radi.
Mechi ya Salzburg dhidi ya Pachuca iliyopigwa huko Cincinnati ilisimama kwa takriban dakika 90 katika kipindi cha pili, kutokana na hali kama hiyo, wakati Palmeiras dhidi ya Al-Ahly pia ikichelewa kwa takriban dakika 40 huko New Jersey kutokana na radi na taadhari za kiusalama.
Pia katika mechi ya Benfica ilipoichapa Auckland City 6-0, kipindi cha pili kilichelewa kuanza kwa takriban saa mbili kutokana na radi.
Mechi iliyochelewa dakika 15 kabla ya kuanza kwa sababu ya joto kali ni Club Leon dhidi ya Al Ahly.

ATHARI KWA WACHEZAJI
Kutokana na hali mbaya ya hewa, imesababisha wachezaji wawe na uchovu kupita kiasi kutokana na upungufu wa maji mwilini pamoja na matatizo mengine ya kiafya na majeraha.
Nyota wa Atletico Madrid, Marcos Llorente alisema hali ilikuwa ya ‘joto sana’ katika mchezo waliopoteza 4-0 dhidi ya PSG huko Los Angeles na kukiri hali ya hewa ilikuwa nyuzi joto 32.
Hata hivyo, kuanzia wiki hii wachezaji huenda wakalazimika kucheza katika hali ya hewa ya nyuzi joto 41.
Fossil Free Football ambalo ni kundi la kampeni linaloangazia athari za mabadiliko ya tabianchi kwenye soka linasema: “Tuna wasiwasi mkubwa hasa kuhusu mechi zitakazochezwa kwenye uwanja wa Charlotte usio na kivuli cha kutosha na hali ya hewa inaweza kufikia nyuzi joto 38, wakati wa mechi ya Real Madrid na Pachuca na nyuzi joto 41 wakati wa mechi ya Benfica na Bayern.”
Kocha wa Chelsea, Enzo Maresca alikiri hawezi kuanzisha kikosi chake cha nguvu kila mechi kutokana na hali hiyo mbaya ya hewa.

MASHABIKI
Si wachezaji pekee walio hatarini. Mashabiki pia afya zao zipo hatarini na ripoti zinaeleza baadhi yao walilazimika kuondoka majukwaani wakati wa mechi kutokana na joto kali.
Vilevile wamekuwa wakikumbana na foleni ndefu na uhaba wa maji kwenye viwanja licha ya mahudhurio kubwa ni madogo.
WARUSHA MATANGAZO
Mechi ya Benfica dhidi ya Auckland ilitarajiwa kuisha saa moja kabla ya Chelsea dhidi ya Flamengo kuanza.
Hata hivyo, mechi hizo ziliingiliana baada ya mechi ya Benfica na Ackland kusimamishwa kutokana na joto na matokeo yake ilimalizika muda mfupi baada ya ile ya Chelsea kumalizika.
Kocha wa Benfica, Bruno Lage alisema: “Hii ndiyo mechi ndefu zaidi ya maisha yangu. Shukrani za kipekee kwa mashabiki wetu, waliokuwa hapa kwa saa tano wakituunga mkono. Tulicheza kadiri ya uwezo wetu. Joto lilifanya mechi iwe ngumu sana.”

MAJIBU YA FIFA
Wametangaza taarifa fupi wakidai afya ni kipaumbele chao kikuu na wataalamu wao wa tiba wamekuwa wakitoa mwongozo.
Shirikisho hilo la soka duniani limesema: “Kipaumbele cha FIFA ni afya ya kila mtu anayehusika na soka na wataalamu wa matibabu wa FIFA wamekuwa wakizungumza mara kwa mara na timu zinavyoshiriki ili kushughulikia usimamizi wa joto na hali ya mazingira.”
FIFA imethibitisha kutakuwa na mapumziko ya kunywa maji dakika ya 30 na 75 ikiwa itahitajika.
Wameongeza mashabiki wataruhusiwa kuingia na chupa za maji za hadi lita moja viwanjani.
MALALAMIKO
Kocha wa Real Madrid, Xabi Alonso alinukuliwa akisema: “Hatuwezi kucheza mechi ya kiwango cha dunia katika mazingira ya joto kama hili. Hii ni hatari kwa afya ya wachezaji wetu.” Baadhi ya viongozi wa timu pia wametoa wito kwa FIFA kuchukua hatua za haraka, ikiwezekana kufikiria upya ratiba au miji ya mechi zilizobakia.