Prime
Nyuma ya pazia usajili wa Chilambo, Kapombe atajwa
KWA miaka tisa, nafasi ya beki wa kulia Simba imekuwa kama ngome isiyotikiswa. Karibu kila msimu klabu hiyo imekuwa ikisajili mchezaji mpya kwa matumaini ya kumpa ushindani Shomary Kapombe lakini mwisho wa safari mkongwe huyo amekuwa akimaliza msimu akiwa chaguo la kwanza.
Sasa Nathaniel Chilambo amepewa jukumu la kubadili simulizi hiyo, kazi iliyowashinda Jimmyson Mwanuke, Israel Mwenda, David Kameta ‘Duchu’, Haruna Shamte na Zana Coulibaly.
Usajili wa Chilambo haukuwa kwa bahati mbaya, unajua kwanini? Simba imefikia wakati wa kuanza kujiandaa kwa maisha baada ya Kapombe huku ikihitaji kuongeza ushindani katika nafasi ambayo kwa muda mrefu imekuwa ikitawaliwa na mchezaji mmoja.
Swali kubwa ni kama Chilambo ndiye atakayevunja historia hiyo.
Tangu arejee Msimbazi 2017, Kapombe amekuwa nguzo ya safu ya ulinzi, akifanya kazi chini ya makocha 12, achana na wale wa muda lakini ameendelea kubaki chaguo la kwanza kwenye kikosi hicho.
Amefanya kazi chini ya Joseph Omog, Pierre Lechantre, Patrick Aussems, Sven Vandenbroeck, Didier Gomes, Pablo Franco, Zoran Manojlovic, Robertinho, Abdelhak Benchikha, Fadlu Davids, Dimitar Pantev na sasa Steve Barker.
Mkongwe huyo, amejenga heshima kutokana na ubora wake, uwezo wa kusaidia mashambulizi, nidhamu ya kiuchezaji na uzoefu mkubwa wa mechi za Ligi Kuu, dabi na michuano ya CAF.
Katika kipindi hicho, Simba haikukaa kimya. Kila ilipoona kuna haja ya kuongeza ushindani, iliingia sokoni kutafuta beki mwingine wa kulia.
Hata hivyo, kila usajili uliofanywa uliishia kuongeza upana cha kikosi huku Kapombe akiendelea kushikilia nafasi yake.
Miongoni mwa wachezaji ambao walipewa jukumu hilo kwa nyakati tofauti ni pamoja na Israel Mwenda kutoka KMC.
Mwenda aliwasili akiwa na sifa za beki wa kisasa anayependa kupanda kushambulia na kupiga krosi zenye ubora, lakini hata yeye hakudumu katika vita ya kuwania nafasi ya kwanza. Kapombe aliendelea kuaminiwa zaidi, hasa katika mechi zenye uzito mkubwa.
Pia walipita Haruna Shamte na hata Zana Coulibaly ambaye alikuwa beki wa kimataifa kutoka Ivory Coast.
Wote waliwasili wakitajwa ni mabeki wenye uwezo wa kuongeza ushindani katika nafasi ya beki wa kulia, lakini simulizi haikubadilika. Walibaki wakicheza kwa vipindi huku Kapombe akiendelea kuwa mhimili wa kikosi cha kwanza.
David Kameta ‘Duchu’ naye alipata nafasi msimu uliopita na kuonyesha uwezo wake. Alianza katika baadhi ya mechi na kuonyesha nidhamu nzuri ya uchezaji, lakini kila ilipofika mechi za maamuzi, benchi la ufundi lilimrudisha Kapombe kwenye nafasi yake.
Sasa jukumu hilo limehamia kwa Chilambo ambaye ameonyesha uwezo wa kucheza kwa kasi, kupandisha mashambulizi, kutoa krosi zenye ubora na kurudi haraka kujilinda, sifa zinazohitajika kwa beki wa kisasa akiwa na Azam FC. Hata hivyo, ubora huo pekee hautatosha.
Chini ya kocha Steve Barker, kila nafasi italazimika kupiganiwa. Barker anapenda mabeki wa pembeni wanaoweza kushambulia bila kupuuza majukumu ya ulinzi, hivyo Chilambo atalazimika kuonyesha ubora katika hilo, iwe mazoezini au kwenye mechi.
Faida kubwa anayoweza kuwa nayo ni umri.
Wakati Kapombe anaingia katika hatua za mwisho za maisha yake ya soka hivi sasa akiwa na miaka 34, Chilambo bado ana miaka 22 inayompa nafasi ya kujijenga na kuimarisha kiwango chake.
Hilo linaifanya Simba isifikirie ushindani wa msimu huu pekee, bali pia kumwandaa mrithi wa muda mrefu wa nafasi hiyo.
Lakini historia inaonyesha kuwa umri pekee hautoshi kumng’oa Kapombe. Mwenda, Shamte na hata Coulibaly walijaribu lakini wote walishindwa kuivunja utawala wa beki huyo mkongwe. Sasa ni zamu ya Chilambo.
Kwa upande mwingine, ujio wa Chilambo unaweza pia kuwa habari njema kwa Kapombe. Kwa muda mrefu amekuwa hana mpinzani anayemweka kwenye presha kubwa ya kupigania nafasi yake. Ushindani huo unaweza kumfanya aendelee kuongeza kiwango chake na kuifanya Simba inufaike kwa kuwa na mabeki wawili wenye uwezo wa kuanza kikosi cha kwanza.
MSIKIE COULIBALY
Miongoni mwa wachezaji waliowahi kuingia Simba kwa lengo la kuongeza ushindani kwenye nafasi ya beki wa kulia dhidi ya Shomary Kapombe ni Zana Coulibaly.
Beki huyo wa kimataifa kutoka Ivory Coast anaamini ushindani wa nafasi hiyo si jambo rahisi kutokana na kiwango na uzoefu ambao Kapombe ameonyesha kwa miaka mingi.
“Namkumbuka vizuri (Kapombe) ni mchezaji mwenye uzoefu mkubwa. Unapocheza nafasi moja na mchezaji wa aina yake unatakiwa kuwa tayari kufanya kazi kwa bidii kila siku, kwa sababu kiwango chake kinakulazimisha kuongeza juhudi zako. Simba ni klabu kubwa na kila mchezaji anayefika pale anatakiwa kuwa tayari kupigania nafasi yake,” amesema Coulibaly.