Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

PSG yakubali kumlipa Mbappé Dola 68.5 Milioni

Muktasari:

  • Uchunguzi kuhusu madai ya unyanyasaji wa kisaikolojia yaliyowasilishwa na mchezaji huyo dhidi ya klabu hiyo umetupiliwa mbali, ambapo jopo la majaji wa uchunguzi jijini Paris walitoa uamuzi wa kutofungua mashtaka mwishoni mwa Mei 2026 kutokana na kukosekana kwa ushahidi wa kutosha ambao ulifahamika karibuni.

PARIS, UFARANSA: Mvutano wa kisheria kati ya mshambuliaji wa Real Madrid, Kylian Mbappe na klabu yake ya zamani, PSG, unakaribia kufika mwisho.

Uchunguzi kuhusu madai ya unyanyasaji wa kisaikolojia yaliyowasilishwa na mchezaji huyo dhidi ya klabu hiyo umetupiliwa mbali, ambapo jopo la majaji wa uchunguzi jijini Paris walitoa uamuzi wa kutofungua mashtaka mwishoni mwa Mei 2026 kutokana na kukosekana kwa ushahidi wa kutosha ambao ulifahamika karibuni.

Upande mwingine mkubwa wa mgogoro huo unaohusu masuala ya ajira nao umefungwa baada ya PSG kuamua kutokata rufaa dhidi ya hukumu iliyoitaka klabu hiyo kumlipa takriban Dola 68.5 milioni.

Kwa mujibu wa vyanzo vilivyo karibu na kesi hiyo vilivyonukuliwa na AFP na kuchapishwa na gazeti la L’Equipe, mahakimu walihitimisha kuwa hakukuwa na “ushahidi wa kutosha” kuendelea na shauri hilo. Pia walizingatia ukweli Mbappe aliondoa malalamiko yake baada ya uchunguzi wa mahakama kuanzishwa na kuweka wazi uamuzi huo.

Kutokana na hali hiyo, waliona kuwa “haiwezekani kuendelea na uchunguzi”. Kwa mtazamo wao, hakukuwa na sababu ya msingi ya kuwahoji mashahidi na wahusika wengine wakati mlalamikaji mwenyewe alikuwa tayari ameondoa tuhuma zake, jambo ambalo lingeweza kutumiwa na watu waliokuwa wakichunguzwa kujitetea.

Malalamiko hayo yaliwasilishwa Mei 16, 2025 na kuondolewa baada ya uchunguzi kuanzishwa. Mbappe aliishutumu PSG kwa unyanyasaji wa kisaikolojia na kujaribu kumshinikiza ili kumlazimisha kusaini makubaliano fulani. Katika malalamiko yake, alitaja utaratibu unaojulikana kama “loft”, ambao ulisababisha kutengwa kwake na kikosi cha kwanza cha timu hiyo katika majira ya kiangazi 2023.

Gazeti la L’Equipe linaeleza utaratibu huo, ambao hutumiwa na klabu mbalimbali katika soka tayari unachunguzwa katika kesi kadhaa jijini Paris.

Mbappe aliondoka PSG 2024 akiwa mchezaji huru na kusaini mkataba na Real Madrid. Baada ya hapo, mgogoro wa kifedha ulianza kati ya pande hizo mbili kuhusu mishahara, bonasi na malipo ya likizo ambayo mchezaji huyo alidai kuwa klabu ilikuwa haijamlipa.

Desemba 16, 2025, Mahakama ya Kazi jijini Paris iliiamuru PSG kumlipa Mbappe takriban Dola 68.5 milioni. Klabu hiyo iliamua kutokata rufaa dhidi ya hukumu hiyo ambayo sasa imekuwa ya mwisho na haiwezi tena kukatiwa rufaa katika utaratibu huo.