Dakika 45 Za Ronaldinho akirejea uwanjani baada ya miaka 11
Muktasari:
- Ronaldinho aliyecheza nafasi ya kiungo mshambuliaji, alianza mchezo huo katika kikosi cha Ravenna, kabla ya kufanyiwa mabadiliko wakati kipindi cha pili kinataka kuanza, nafasi yake ikichukuliwa na Matteo Maggio.
NYOTA wa zamani wa Barcelona na AC Milan, Ronaldinho Gaucho, amerejea uwanjani baada ya miaka 11 tangu atangaze kustaafu soka, akicheza dakika 45 pekee katika mchezo ambao Ravenna imeibuka na ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Forli katika Ligi ya Daraja la Tatu Italia (Serie C), Kundi B, raundi ya 14.
Ronaldinho aliyecheza nafasi ya kiungo mshambuliaji, alianza mchezo huo katika kikosi cha Ravenna, kabla ya kufanyiwa mabadiliko wakati kipindi cha pili kinataka kuanza, nafasi yake ikichukuliwa na Matteo Maggio.
Katika muda aliokuwepo uwanjani leo Novemba 15, 2026, nyota huyo raia wa Brazil mwenye umri wa miaka 46, alionesha mchango wake katika ujenzi wa mashambulizi, akipata alama 7.0.
Takwimu zinaonesha kuwa, Ronaldinho aligusa mpira mara 28 na alifanikiwa kupiga pasi sahihi 17 kati ya 21, sawa na asilimia 81, huku akifanikiwa kupiga pasi moja muhimu iliyoweza kusaidia kutengeneza nafasi ya kufunga.
Aidha, alikamilisha pasi nane kati ya 12 katika eneo la mwisho la mashambulizi (67%), huku akipiga pasi tatu kati ya tano ndani ya eneo la hatari (60%).
Katika mipira ya krosi, alifanikiwa mmoja kati ya mitatu, sawa na asilimia 33. Pia alishinda pambano moja kati ya mawili ya ana kwa ana (50%).
Licha ya kutofunga bao, Ronaldinho alihusika katika maandalizi ya bao la kwanza la Ravenna lililofungwa na Giulio Donati dakika ya 36, baada ya kuanzisha shambulizi lililozaa bao hilo.
Uwepo wake uwanjani ulikuwa wa kihistoria kwani ilikuwa mechi yake ya kwanza ya ushindani baada ya takribani miaka 11 tangu kucheza kwa mara ya mwisho mwaka 2015.
Katika mchezo huo wa Ligi ya Serie C, Kundi B, Ravenna ilishinda mabao 2-0, Donati akifunga bao la kwanza dakika ya 36 kabla ya Simone Rabbi kuongeza la pili dakika ya 58, akihakikisha timu hiyo inapata pointi tatu muhimu dhidi ya Forli.
Ushindi huo umeifanya Ravenna kuimarisha nafasi yake ya pili katika msimamo wa Serie C, Kundi B ikifikisha pointi 32, ikishinda mechi kumi, sare mbili sawa na vipigo, huku ikiwa imefunga mabao 27 na kuruhusu manane. Ipo nyuma ya vinara Spezia yenye pointi 38, hivyo pengo ni pointi sita.
KUREJEA KWAKE
Kwa upande mwingine, kurejea kwa Ronaldinho nchini Italia ni kama awamu yake ya pili ya kucheza soka katika nchi hiyo, ingawa safari hii akiwa katika kiwango cha chini zaidi ukilinganisha na alipokuwa AC Milan. Alicheza kwa miamba hiyo ya Italia kwa misimu mitatu, kuanzia mwaka 2008 hadi 2011, ambapo alifanikiwa kutwaa taji moja la Ligi Kuu Italia (Serie A).
Katika maisha yake ya soka yaliyojaa mafanikio, Ronaldinho pia aliwahi kuzichezea Paris Saint-Germain na Barcelona. Miongoni mwa mafanikio yake makubwa ni kutwaa Kombe la Dunia mwaka 2002 akiwa na timu ya taifa ya Brazil pamoja na kushinda tuzo ya mchezaji bora duniani, Ballon d’Or, mwaka 2005.
Ronaldinho alijulikana kwa kipaji chake cha hali ya juu cha kumiliki na kuuchezea mpira, akitumia ufundi wa aina mbalimbali uliowashangaza mashabiki na wapinzani. Alikuwa na nguvu kubwa, uwezo wa kipekee wa kufunga mabao na jicho kali la kuona nafasi, huku akivutia pia kwa tabasamu lake maarufu lililoonesha meno yake na burudani aliyokuwa akiitoa uwanjani.
Akiwa Barcelona, alifunga mabao 94 katika michezo 207, kipindi ambacho alicheza pamoja na Lionel Messi aliyekuwa anaanza kung’ara katika soka la dunia. Kwa upande wa timu ya taifa ya Brazil, Ronaldinho alifunga mabao 33 katika michezo 97 aliyocheza.
Mbali na klabu hizo, Ronaldinho pia aliwahi kuzichezea timu za Brazil za Gremio, Flamengo na Atletico Mineiro, kabla ya kwenda Mexico kuichezea Queretaro. Mara ya mwisho aliitumikia Fluminense ya kwao Brazil mwaka 2015, akastaafu.
Baada ya hapo, akacheza mchezo wa Futsal nchini India na Beach Soccer kwao Brazil, kabla ya 2026 kurejea kucheza soka akisaini Ravenna ambapo pia ameingia klabuni hapo kama mwekezaji.
HAIKUWA RAHISI
Machi 6, 2020, Ronaldinho alikamatwa nchini Paraguay akiwa na kaka yake Roberto de Assis Moreira kwa tuhuma za kutumia pasipoti na vitambulisho bandia vya Paraguay. Wawili hao walikuwa wamewasili nchini humo kwa mwaliko wa kushiriki shughuli za kijamii na uzinduzi wa kitabu cha maisha ya Ronaldinho.
Baada ya kuhojiwa na polisi, Machi 7, 2020, mahakama iliamuru Ronaldinho na kaka yake kuwekwa mahabusu katika gereza la Agrupación Especializada jijini Asuncion, Paraguay, wakati uchunguzi wa tuhuma hizo ukiendelea.
Ronaldinho alikaa gerezani kwa siku 32 kabla ya Aprili 7, 2020, mahakama kuruhusu yeye na kaka yake kutoka mahabusu kwa dhamana ya dola za Marekani milioni 1.6.
Hata hivyo, kuachiwa kwake hakukuwa uhuru kamili kwani aliamriwa kutumikia kifungo cha nje katika Hoteli ya Palmaroga jijini Asuncion, ambako aliishi chini ya uangalizi wa mamlaka kwa takribani miezi minne akisubiri uamuzi wa mahakama.
Hatimaye, Agosti 24, 2020, Ronaldinho aliachiwa huru baada ya mahakama kuidhinisha makubaliano ya kusitisha mashitaka dhidi yake kwa masharti, huku yeye na kaka yake wakitakiwa kulipa faini ya jumla ya dola 200,000 za Marekani, hivyo kumaliza sakata lililomuweka kizuizini kwa takribani miezi mitano na nusu.