Yamal kinara wa dakika kwa chipukizi Ulaya
Muktasari:
- Transfermarkt imechambua klabu za ligi tano kubwa za Ulaya ambazo zimewapa wachezaji wenye umri chini ya miaka 21 dakika nyingi zaidi za kucheza na kubaini wachezaji wa umri huo walipata muda mwingi zaidi katika timu zao.
PARIS, UFARANSA: ACHANA na ukweli kwamba ligi mbalimbali duniani kwa sasa zimesimama kupisha kalenda ya Shirikisho la Kandanda la Kimataifa (Fifa), kwa ajili ya mechi za timu za taifa, lakini ligi tano bora za Ulaya (EPL, LaLiga, Serie A, Bundesliga na Ligue 1), zimeendelea kutoa somo kwa zile za mabara mengine; na safari hii kwa kutoa nafasi kubwa kwa vijana kuonyesha vipaji viwanjani msimu huu.
Transfermarkt imechambua klabu za ligi tano kubwa za Ulaya ambazo zimewapa wachezaji wenye umri chini ya miaka 21 dakika nyingi zaidi za kucheza na kubaini wachezaji wa umri huo walipata muda mwingi zaidi katika timu zao.
Hakujawahi kuwa na kipindi kizuri zaidi katika historia ya soka kwa vipaji chipukizi kupata nafasi ya kucheza katika timu za wakubwa, huku klabu zikitambua kwa kina faida zinazotokana na kuendeleza vipaji hivyo. Kwa uhalisia, klabu nyingi duniani hulenga kuwauza wachezaji wao wenye vipaji vikubwa kwa timu za Ulaya kwa kuwa jambo hilo ni muhimu katika mfumo wa kibiashara.
Pia, kuna faida nyingine kwa mashabiki, kwani hakuna hisia nzuri zaidi kwao kama kushuhudia mchezaji aliyepitia akademi ya klabu yao akikuza kipaji chake na kuwa nyota wa kikosi cha kwanza. Katika uchambuzi huo Strasbourg ya Ufaransa ndiyo iliyowapa wachezaji chipukizi wenye umri chini ya miaka 21 dakika nyingi zaidi za kucheza.
Lakini, kwa upande wa wachezaji binafsi, ni nani anayeongoza? Lamine Yamal amekusanya dakika nyingi zaidi za kucheza miongoni mwa wachezaji wenye umri chini ya miaka 21 katika ngazi ya klabu msimu huu akiwa nazo 1,355 ndani ya Barcelona.
Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 19 amefikia mafanikio makubwa yasiyo ya kawaida katika kipindi kifupi tangu aanze soka, na amehusika moja kwa moja katika mabao 25, kwa kufunga na kutoa pasi za mwisho, katika michezo 16 msimu huu.
Lens ya Ufaransa inashika nafasi ya nane katika orodha ya klabu zilizowapa madogo wenye vipaji nafasi kubwa ya kucheza, huku kipa Robin Risser akiwa nafasi ya pili katika orodha ya wachezaji waliokusanya dakika nyingi zaidi akiwa nazo 1,350.
Jacobo Ramon anashika nafasi ya tatu akiwa na dakika 1,291, ambapo beki huyo wa kati wa Como amekuwa akizivutia klabu za Ligi Kuu England, huku Real Madrid ikiwa na kipengele cha kumnunua tena katika mkataba wake.
Nyota huyo amekuwa na msimu bora akiendelea kuibeba Como katika mashindano ya ndani ya Italia na Ulaya.
Nyota wa Brighton, Luka Vuskovic na Jeremy Jacquet wa Liverpool wanakamilisha orodha ya wachezaji watano waliopo nafasi za juu kwenye orodha wakiwa miongoni mwa mabeki bora wa kati katika Ligi Kuu England msimu huu.
Takwimu zinaonyesha kuwa Vuskovic amecheza dakika 1,270 huku Jacquet akiwa nazo 1,244 na wamekuwa wakizima mashambulizi hatari kutoka kwa kaka zao wanaozichezea timu zinazounda Top Six katika ligi hiyo.
Mnorway Antonio Nusa anayekipiga RB Leipzig na Mjerumani Ibrahim Maza wa Bayer Leverkusen ni miongoni mwa vipaji vikubwa zaidi katika Bundesliga, na wote wamecheza dakika 1,097, hivyo kufungana katika orodha hiyo.
Nusa amekuwa na msimu bora zaidi Ujerumani ambako anatambulika kuwa miongoni mwa nyota hatari wanaocheza kama winga sambamba na supastaa wa Bayern Munich, Michael Olise huku Maza kwa upande amelikamata vilivyo eneo la kiungo mshambuliaji katika kikosi cha Leverkusen akijihakikishia namba ya kudumu kikosini.
Ndani ya 20 bora kuna majina mengine yanayofahamika zaidi wapo beki wa kati wa Real Madrid, Dean Huijsen anayeshika nafasi ya 17 na Jobe Bellingham wa Borussia Dortmund katika nafasi ya 18.