Pointi za ubigwa EPL
Muktasari:
- Lakini, je ni pointi kiasi gani zinatosha kubeba ubingwa? Msimu uliopita, Liverpool ilinyakua taji hilo baada ya kukusanya pointi 84. Lakini, kiwango kilishuka mwishoni mwa Aprili baada ya kujihakikishia ubingwa tayari, ambapo ilivuna pointi mbili tu kati ya 12 ilizopaswa kuzibeba.
LONDON, ENGLAND: MSIMU wa Ligi Kuu England 2025/26 umeanza rasmi wikiendi hii, ambapo miamba 20 itachuana kuwania ubingwa huo.
Lakini, je ni pointi kiasi gani zinatosha kubeba ubingwa? Msimu uliopita, Liverpool ilinyakua taji hilo baada ya kukusanya pointi 84. Lakini, kiwango kilishuka mwishoni mwa Aprili baada ya kujihakikishia ubingwa tayari, ambapo ilivuna pointi mbili tu kati ya 12 ilizopaswa kuzibeba.
Kwa kifupi tu, pointi 84 zilikuwa ndogo kwa timu kubwa bingwa katika misimu ya hivi karibuni, ambapo huko nyuma ni Leicester City (pointi 81) msimu wa 2015/16 na Manchester United (80) msimu wa 2010/11 ndizo zilizobeba ubingwa wa Ligi Kuu England na pointi chache katika kipindi cha miongo miwili iliyopita.
Wastani wa pointi zilizotoa mabingwa kwa kipindi cha miaka 32 ya Ligi Kuu England ikiwamo misimu mitatu ya kwanza iliyokuwa na mechi 42 tofauti ya 38 za sasa ni pointi 87.7.
Hata hivyo, katika misimu tisa ambayo Pep Guardiola amekuwa Manchester City wastani wa pointi za ubingwa ni 92.6, hiyo ikionyesha upinzani umekuwa mkali kwelikweli na ubora umeongezeka.
Pointi nyingi zaidi katika historia ya Ligi Kuu England
1.Man City (2017/18, pointi 100)
2.Liverpool (2019/20, pointi 99)
3.Man City (2018/19, pointi 98)
4.Liverpool (2018/19, pointi 97)
5.Chelsea (2004/05, pointi 95). Man City imeshinda ubingwa mara sita katika misimu tisa iliyopita ikiwamo 2017/18 ilipoweka rekodi ya kuwa timu pekee Ligi Kuu England iliyofikisha pointi 100.
Man City na Liverpool ni miongoni mwa timu zilizokuwa na wastani mzuri wa pointi kwenye ligi katika kipindi cha Guardiola akiwa Ligi Kuu England.
Wastani wa pointi za klabu kuanzia 2016/17 hadi 2024/25:
-Man City, pointi 87.4
-Liverpool, pointi 82.3
-Arsenal, pointi 71.2
-Chelsea, pointi 68.7
-Man United, pointi 65.7
-Tottenham, pointi 65.6
Lakini, pointi za jumla kwa msimu zinabainisha nusu ya ukweli halisi. Liverpool ya kocha Arne Slot ilimaliza msimu wa 2024/25 ikiwa na pointi 84, lakini ingeweza kuwa kinara kwenye msimamo wa Ligi Kuu England hata kwa pointi 74 tu, ambazo ndizo ilizovuna Arsenal kwenye nafasi ya pili, kwa kuwa wao walikuwa na wastani mzuri wa tofauti ya mabao ya kufunga na kufungwa.
Kwenye Ligi Kuu England hakuna timu iliyowahi kushinda ubingwa ikiwa na pointi 74, kwa sababu misimu mitatu ambayo ilitoa bingwa kwa kuwa na pointi chache zilikuwa juu ya hizo, Man United 1996/97 (75), Arsenal 1997/98 (78) na Man United tena 1998/99 (79).
Kwenye historia ya Ligi Kuu England, ukitazama msimu wa kwanza kabisa, 1992/93, wastani wa pointi za ubingwa ulikuwa mkubwa kwa sababu timu iliyoshika namba mbili ilikuwa na wastani wa pointi 81.3. Na kwa misimu ya karibuni, hilo limekuwa na ongezeko kubwa kabisa, ambapo katika kipindi ambacho Guardiola amekuwa Man City, timu bingwa itahitaji kuwa na wastani wa pointi 84.2 kwenye juu ndiyo ianze kufikiria habari za kubeba ubingwa.
Katika msimu wa 2018/19, Liverpool ilivuna pointi 97, lakini bado ilimaliza kwenye nafasi ya pili baada ya taji kubebwa na Man City kwa pointi 98. Wakati msimu mpya ukianza usiku wa Ijumaa, ni pointi nyingi kiasi gani zitakwenda kutoa bingwa wa Ligi Kuu England msimu huu wa 2025/26?