Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Pochettino kuifufua Manchester United?

Muktasari:

  • Kocha huyo raia wa Argentina amekuwa akihusishwa na nafasi ya kuinoa United kwa takribani muongo mmoja, tangu jina lake lilipoanza kuhusishwa na klabu hiyo mwaka 2016, baada ya kuonekana akitoka kwenye mgahawa wa Scott’s, Mayfair jijini London, alipokutana na aliyekuwa kocha maarufu wa timu hiyo, Sir Alex Ferguson.

LONDON, England: MAURICIO Pochettino anaonekana kuwa kwenye nafasi nzuri ya kutua Manchester United na kuchukua nafasi ya Michael Carrick aliyetimuwa katika klabu hiyo baada ya mkutano wa viongozi wake kufanyika Monaco.

Kocha huyo raia wa Argentina amekuwa akihusishwa na nafasi ya kuinoa United kwa takribani muongo mmoja, tangu jina lake lilipoanza kuhusishwa na klabu hiyo mwaka 2016, baada ya kuonekana akitoka kwenye mgahawa wa Scott’s, Mayfair jijini London, alipokutana na aliyekuwa kocha maarufu wa timu hiyo, Sir Alex Ferguson.

Wakati huo, Ferguson alikuwa amestaafu kwa miaka mitatu, huku Pochettino akijijengea jina Tottenham Hotspur kwa kuunda kikosi kilichokuwa na soka la kushambulia kwa kasi na nguvu, aina ya uchezaji iliyomvutia kocha huyo mkongwe wa Scotland.

Pochettino aliwahi kuelezea mkutano huo kuwa ulikuwa ni mazungumzo kati ya watu wawili wa taaluma moja, akimwelezea Ferguson kama gwiji na yeye mwenyewe kama mwanafunzi.

Tangu wakati huo, jina la Pochettino limekuwa likitajwa mara kadhaa kama mgombea wa kuinoa Manchester United.

Alikuwa miongoni mwa makocha waliotajwa kuchukua nafasi ya Louis van Gaal baada ya kutimuliwa Mei 2016, kabla ya kuhusishwa tena na nafasi hiyo kufuatia kuondoka kwa Jose Mourinho Desemba 2018.

Aprili 2022, Pochettino alikuwa miongoni mwa makocha waliokuwa kwenye orodha fupi ya United kabla ya klabu hiyo kumteua Erik ten Hag. Jina lake lilitajwa tena Oktoba 2024, wakati kocha huyo raia wa Uholanzi alipoondoka Old Trafford.

Sasa, wakati Carrick akisubiri hatma yake, Pochettino anaonekana kuwa na nafasi kubwa ya kupewa jukumu la kuiongoza United na kujaribu kurejesha hadhi ya klabu hiyo.

Hata hivyo, changamoto inayomkabili ni kubwa, kwani United ambayo iliwahi kuwa moja ya klabu kubwa na zenye mafanikio zaidi duniani, imekuwa ikizama kutokana na uamuzi yasiyo sahihi ya kiutawala na uteuzi wa makocha usioleta matokeo yaliyotarajiwa.

Hali hiyo imechangia kuundwa kwa kikosi chenye mchanganyiko wa wachezaji walionunuliwa na makocha sita tofauti, jambo linaloifanya timu hiyo kukosa mwelekeo wa pamoja.

Miongoni mwa mambo yanayomtofautisha Pochettino ni tabia yake ya kuweka sanduku lenye ndimu ofisini kwake, akiamini kuwa matunda hayo hufyonza nguvu hasi. Hata hivyo, huenda akahitaji ndimu nyingi zaidi kukabiliana na hali mbaya ya kisaikolojia iliyotanda Old Trafford.

Kabla ya kufikiria kuhusu ujio wa kocha mpya, kinachosubiriwa ni uthibitisho rasmi wa kuondoka kwa Carrick, mchakato ambao umechukua muda mrefu na ambao umeibua maswali kuhusu namna suala hilo linavyoshughulikiwa na wamiliki wenza wa klabu hiyo, Sir Jim Ratcliffe, mtendaji mkuu Omar Berrada na mkurugenzi wa soka Jason Wilcox.

Carrick, mwenye umri wa miaka 45, ameonekana kushindwa kuhimili majukumu ya ukocha mkuu wa kudumu tangu alipothibitishwa katika nafasi hiyo baada ya kufanya vizuri alipokuwa kocha wa muda.

Hata hivyo, historia yake ya mafanikio akiwa mchezaji, tabia yake ya unyenyekevu na dhamira yake ya kuirejesha United kwenye mafanikio vinafanya namna anavyoshughulikiwa katika mchakato wa kuondoka kwake kuwa suala lisilopendeza.

Hisia hizo pia zinaonekana miongoni mwa mashabiki wa United ambao wameendelea kuonyesha kutoridhishwa na hali ya klabu yao, huku wakielekeza lawama kwa viongozi wanaowaona kuwajibika kwa mwenendo huo, wakati timu ikiwa katika eneo la kushuka daraja la Ligi Kuu England.