Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Flick aweka rekodi ya kutisha La Liga

Muktasari:

  • Kwa mujibu wa takwimu zilizochapishwa na gazeti la AS, rekodi hiyo inamaanisha kuwa Flick ameitumia asilimia 77 ya muda wake wa kuinoa Barcelona akiwa kileleni mwa ligi, mafanikio yanayomweka miongoni mwa makocha waliofanya vizuri zaidi katika historia ya klabu hiyo.

MADRID, Hispania: KOCHA wa Barcelona, Hansi Flick, ameweka rekodi ya kipekee katika Ligi Kuu ya Hispania (La Liga), baada ya kuiongoza timu hiyo kukaa kileleni mwa msimamo kwa siku 68 kati ya 88 za mechi alizokuwa akiisimamia katika mashindano hayo.

Kwa mujibu wa takwimu zilizochapishwa na gazeti la AS, rekodi hiyo inamaanisha kuwa Flick ameitumia asilimia 77 ya muda wake wa kuinoa Barcelona akiwa kileleni mwa ligi, mafanikio yanayomweka miongoni mwa makocha waliofanya vizuri zaidi katika historia ya klabu hiyo.

Utawala huo umeenda sambamba na mafanikio ya kutwaa mataji mawili mfululizo ya La Liga katika misimu ya 2024/25 na 2025/26, huku Barcelona ikiwa kileleni tena katika msimu wa 2026/27 baada ya kucheza mechi 12, jambo linalompa Flick nafasi ya kusaka taji jingine.

Kwa mujibu wa takwimu hizo, katika mechi 88 za ligi alizosimamia, Barcelona imekuwa ikimaliza siku 68 ikiwa nafasi ya kwanza, huku siku 20 pekee zikiwa timu nyingine ndiyo iliyokuwa kileleni.

Kwa kulinganisha, ni Ernesto Valverde pekee aliyefikia rekodi bora zaidi ya Flick katika historia ya Barcelona. Valverde, aliyeinoa timu hiyo kati ya mwaka 2017 na 2020, aliiwezesha kukaa kileleni katika siku 80 kati ya 95, sawa na asilimia 84.

Hata hivyo, kwa idadi ya jumla ya nyakati ambazo makocha wameiongoza Barcelona kukaa kileleni, Flick tayari anashika nafasi ya nne. Pep Guardiola anaongoza orodha hiyo akiwa na siku 87, akifuatiwa na Frank Rijkaard mwenye siku 85 na Valverde mwenye siku 80.

Mafanikio ya Barcelona katika misimu mitatu ya Flick yanaeleza zaidi ukubwa wa rekodi hiyo.

Katika msimu wake wa kwanza, Barcelona iliongoza msimamo katika siku 31 kati ya 38 za mechi za ligi, sawa na asilimia 82. Msimu uliofuata wa 2025/26, idadi hiyo ilishuka hadi siku 26, sawa na asilimia 69, lakini haikuzuia timu hiyo kutetea ubingwa wake.

Katika msimu huu wa 2026/27, Barcelona imekuwa na utawala mkubwa zaidi baada ya kukaa kileleni katika siku 11 kati ya 12, sawa na asilimia 92.

Rekodi hiyo inatarajiwa kuongezeka baada ya mapumziko ya mechi za kimataifa, kwani Flick atafikisha mara 69 katika siku 89 akiwa kileleni, bila kujali matokeo ya mchezo dhidi ya Villarreal utakaofuata kurejea kwa mashindano ya klabu.

Kwa sasa, Barcelona ina pointi 33, ikiwa na tofauti ya pointi tatu dhidi ya Real Madrid na tano dhidi ya Atletico Madrid.

Hata ikipoteza mchezo wa nyumbani dhidi ya Villarreal, Barcelona haitapoteza moja kwa moja nafasi ya kwanza, kutokana na ubora wake wa tofauti ya mabao ambao unaipa faida dhidi ya Real Madrid.