Endrick aziingiza vitani Roma, Milan
Muktasari:
- Hata hivyo, klabu hizo zinakabiliwa na changamoto ya gharama ya kumsajili nyota huyo, kwani Real Madrid inadaiwa kuhitaji zaidi ya Euro milioni 60 (zaidi ya Sh180 bilioni) ili kumuuza.
MILAN, Italia: KLABU za AS Roma na AC Milan zimeanza kufuatilia kwa karibu hatma ya mshambuliaji wa Real Madrid, Endrick, baada ya kinda huyo wa Brazil kueleza kutokuwa na uhakika kuhusu mustakabali wake Januari kutokana na kukosa nafasi ya kucheza mara kwa mara.
Hata hivyo, klabu hizo zinakabiliwa na changamoto ya gharama ya kumsajili nyota huyo, kwani Real Madrid inadaiwa kuhitaji zaidi ya Euro milioni 60 (zaidi ya Sh180 bilioni) ili kumuuza.
Endrick, ambaye alikuwa uwekezaji mkubwa kwa Real Madrid ilipomnasa kutoka Palmeiras mwaka 2024 kwa ada iliyoweza kufikia Euro milioni 60 ikijumuisha malipo ya nyongeza, amekuwa akipata wakati mgumu kupata nafasi katika kikosi cha kwanza licha ya kuonyesha uwezo mkubwa anapopewa nafasi.
Akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari akiwa kwenye majukumu ya timu ya taifa ya Brazil, mshambuliaji huyo alisema kipaumbele chake ni kupata muda wa kutosha kucheza na kufurahia soka.
“Ninachotaka ni kucheza, kuwa na furaha na kuwasaidia wachezaji wenzangu. Kufunga mabao na kutoa pasi za mwisho, kama nilivyofanya Lyon. Hayo yalikuwa miongoni mwa mambo mazuri zaidi yaliyowahi kunitokea na kipindi nilichokuwa na furaha kubwa,” alisema.
Aliongeza: “Sijui nini kitatokea Januari. Hilo liko mikononi mwa Mungu. Ninachoomba ni kufanya kile kilicho bora kwa maisha yangu ya soka. Chochote kitakachotokea, kitokee. Nitaendelea kuwa mtulivu na kufanya kazi kwa bidii. Madrid ni jiji zuri, lakini nitafanya kila niwezalo kuendeleza taaluma yangu.”
Endrick aliwahi kucheza kwa mkopo katika klabu ya Olympique Lyonnais ya Ufaransa kwa kipindi cha miezi sita, kuanzia Januari hadi Juni 2026, hatua iliyomsaidia kurejesha makali na kupata nafasi katika kikosi cha Brazil kilichojiandaa kwa Kombe la Dunia.
Katika dirisha la usajili la majira ya kiangazi, Roma na Milan zilikuwa miongoni mwa klabu zilizovutiwa zaidi na huduma yake, pamoja na Aston Villa, zikihitaji kumsajili kwa mkopo. Hata hivyo, kocha wa Real Madrid, Jose Mourinho, alisisitiza kumbakiza mshambuliaji huyo Madrid.
Kwa mujibu wa The Athletic, Real Madrid kwa sasa haiko tayari kumruhusu Endrick kuondoka kwa mkopo, lakini inaweza kufikiria kumuuza kwa dau linalozidi Euro milioni 60 iliyotumia kumnasa kutoka Palmeiras miaka miwili iliyopita.
Cha kuvutia ni kwamba Endrick aliwahi kuingia akitokea benchi na kubadili mwelekeo wa mchezo dhidi ya Roma, wakati timu hiyo ya Italia ikiwa mbele kwa mabao 3-1, kabla ya kuchangia bao moja na kutoa pasi ya bao katika ushindi wa Real Madrid wa mabao 4-3.
Hata hivyo, tangu mchezo huo, mshambuliaji huyo amecheza jumla ya dakika 36 pekee katika mechi nne akiwa na jezi ya Real Madrid, hali inayozidi kuibua maswali kuhusu nafasi yake katika kikosi hicho.