Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Taifa Stars kuikabili Nigeria, Gamondi kwenye presha

Muktasari:

  • Katika fainali hizo zitakazofanyika kuanzia Juni 19, 2027 hadi Julai 17, 2027, Tanzania itakuwa mwenyeji kwa kushirikina na Kenya na Uganda.

TIMU ya Taifa ya Tanzania, Taifa Stars, itakuwa uwanjani leo Saa 1:00 usiku, kucheza dhidi ya Nigeria maarufu Super Eagles, katika mechi kali na ya kisasi kwa miamba hiyo ya kufuzu Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON 2027).

Katika fainali hizo zitakazofanyika kuanzia Juni 19, 2027 hadi Julai 17, 2027, Tanzania itakuwa mwenyeji kwa kushirikina na Kenya na Uganda.

Stars inaingia katika mechi hiyo ya kundi L itakayochezwa kwenye Uwanja wa Kimataifa wa Godswill Akpabio uliopo mjini Uyo, Nigeria, ikihitaji ushindi kabla ya kurudiana Novemba 17, 2026, kwenye Uwanja wa New Amaan, Complex, Zanzibar.

Katika kundi hilo la L, Stars inashika nafasi ya tatu na pointi moja baada ya kucheza mechi mbili, huku kikosi cha Nigeria kikiwa nafasi ya pili na pointi tatu, nyuma ya vinara Guinea Bissau inayoongoza ikiwa na pointi sita hadi sasa.

Pointi hiyo moja iliyonayo Stars, ni sawa na ya Madagascar inayoburuza mkia ambayo ilitokana na timu hizo zilipokutana kufungana bao 1-1 katika mechi iliyochezwa Morocco, Septemba 29, 2026.

Katika mechi mbili za Stars, ilichapwa nyumbani mabao 2-0 dhidi ya Guinea Bissau, Septemba 25, 2026, kisha ikatoka sare ya bao 1-1 na Madagascar, Septemba 29, 2026.

Licha ya Stars kufuzu moja kwa moja kutokana na uenyeji wake wa michuano hiyo, ila kiwango cha timu ya Tanzania kimeibua sintofahamu kutokana na mechi mbili ilizocheza hadi sasa, jambo linalotia shaka safari ya kikosi hicho kwenye AFCON.

Sababu za kutilia shaka Stars, ni kutokana na mwenendo mbaya wa timu hiyo inayofundishwa na Kocha Mkuu, Miguel Gamondi, ambaye tangu ajiunge na kikosi hicho ameshinda mechi moja tu, jambo linaloibua sintofahamu na wasiwasi huko mbeleni.

Gamondi aliyejiunga na Stars kwa mara ya kwanza Novemba 4, 2025, akikaimu kisha kukabidhiwa kikosi hicho rasmi Februari 16, 2026, ameiongoza katika jumla ya mechi tisa, ambapo kati ya hizo ameshinda moja, akitoka sare tatu na kupoteza tano.

Katika mechi hiyo moja aliyoshinda Gamondi ilikuwa ni ya kimataifa ya kirafiki ya ushindi wa mabao 6-0 dhidi ya Macau, ikiwa ni ya mashindano maalumu ya FIFA Series 2026, yaliyofanyika Rwanda, kwenye Uwanja wa Kigali Pele, Machi 29, 2026.

Katika mechi hizo tisa ambazo Gamondi amekiongoza kikosi hicho na kushinda moja, timu hiyo imekosa muunganiko mzuri wa eneo la kujilinda na la ushambuliaji, kwa sababu imefunga mabao 13, huku ikiruhusu nyavu zake kutikiswa mara 13.

Faida kubwa ya Stars katika mechi zote mbili kwa maana ya leo na ya Novemba 17, 2026, ni Nigeria kumkosa mshambuliaji wake, Victor Osimhen aliyepata majeraha ya goti la kushoto akiwa na Klabu ya Galatasaray ya Uturuki.

Nyota huyo alipata majeraha hayo Novemba 3, 2026, katika mechi ya Ligi ya Mabingwa Ulaya, wakati Galatasaray iliposhinda mabao 2-0 dhidi ya VfB Stuttgart ya Ujerumani na kugundulika anahitajika kufanyiwa upasuaji mdogo.

Hilo ni pigo kwa kocha wa Nigeria, Eric Chelle, ambaye anakabiliwa na changamoto ya kukosa huduma ya nyota huyo kwa mara nyingine, baada ya kuzikosa mechi za Septemba 2026 dhidi ya Madagascar na Guinea-Bissau kutokana na jeraha la misuli.

Nyota huyo ni muhimili mkubwa katika eneo la ushambuliaji la Super Eagles na Klabu ya Galatasaray ambayo kwa msimu huu ameonyesha kiwango bora, baada ya kufunga mabao tisa na kutoa asisti tatu katika mechi nane za Ligi Kuu ya Uturuki.

Mara ya mwisho kukutana, ilikuwa katika AFCON iliyofanyika Morocco mwaka 2025, ambapo Stars ilichapwa mabao 2-1, Desemba 23, 2025, yaliyofungwa na Semi Ajayi dakika ya 36 na Ademola Lookman dakika ya 52.

Bao la Stars lilifungwa na Charles M’Mombwa dakika ya 50 na kikosi hicho kumaliza nafasi ya tatu kundi C ikipata pointi mbili na kuaga michuano hiyo, ikiungana na Uganda iliyoburuza mkia na pointi moja.

Katika kundi hilo, Nigeria iliibuka kinara na pointi tisa baada ya kushinda mechi zote tatu ilizocheza, ikifuatiwa na Tunisia iliyomaliza nafasi ya pili na pointi nne, kufuatia kikosi hicho kushinda moja, sare moja na kupoteza moja.