Pochettino atua Old Trafford kwa kishindo
Muktasari:
- United imekuwa na mwanzo mgumu wa msimu, ikiwa nafasi ya 18 kwenye msimamo wa Premier League baada ya kushinda mchezo mmoja pekee kati ya 10 iliyocheza.
MANCHESTER, ENGLAND: KOCHA mpya wa Manchester United, Mauricio Pochettino, amewataka mashabiki wa klabu hiyo kuungana na kuipa timu sapoti ya kutosha, akiahidi kuwa msimu huu utakuwa wa kipekee licha ya kikosi hicho kuanza vibaya kampeni ya Ligi Kuu England.
United imekuwa na mwanzo mgumu wa msimu, ikiwa nafasi ya 18 kwenye msimamo wa Premier League baada ya kushinda mchezo mmoja pekee kati ya 10 iliyocheza.
Pochettino aliwasili jijini Manchester Jumatano asubuhi kwa ndege binafsi, akitokea Marekani ambako alikuwa amemaliza majukumu yake ya mwisho kama kocha wa timu ya taifa ya nchi hiyo.
Kocha huyo raia wa Argentina alielekea moja kwa moja katika kituo cha mazoezi cha Carrington, ambako alifanya ziara, kukutana na wachezaji pamoja na baadhi ya wafanyakazi wa klabu hiyo.
Katika ujumbe wake wa kwanza kwa mashabiki wa United kupitia akaunti rasmi ya klabu hiyo kwenye mtandao wa X, Pochettino alisisitiza umuhimu wa umoja na ushirikiano ili kurejesha furaha Old Trafford.
"Habari mashabiki wa United, ni Mauricio Pochettino. Nina hamu kubwa ya kukutana nanyi. Nimesikia mambo mengi mazuri kuhusu nyinyi.
"Natumai tutaleta furaha kwa kufanya kazi pamoja na kuungana. Huu utakuwa msimu wa kipekee, tunahitaji sapoti yenu ili kuwapa wachezaji nguvu ya kupambana uwanjani na kupata matokeo tunayostahili," amesema Pochettino.
Katika ujumbe mwingine alioutoa kwa lugha ya Kihispania, kocha huyo alisisitiza kuwa jina la Manchester United linapaswa kuakisi mshikamano wa kila mmoja ndani ya klabu.
Amesema kila mmoja ana wajibu wa kushirikiana ili kuhakikisha wachezaji wanapata mazingira mazuri ya kuonyesha uwezo wao uwanjani.
Pochettino alieleza kuwa anaamini anaweza kurejesha nyakati za furaha kwa klabu hiyo na kujenga umoja unaohitajika ili United kurejea kwenye ushindani.
Akizungumza kupitia vyombo vya habari vya klabu hiyo muda mfupi baada ya kuwasili, amesema: "Asanteni sana. Nina furaha kubwa kuwa hapa. Ni heshima na upendeleo mkubwa kuwa sehemu ya klabu hii kubwa. Nina hamu ya kuanza kazi."
ATAMANI KUMALIZA UBABE WA MAN CITY
Katika mahojiano yake ya mwisho akiwa kocha wa timu ya taifa ya Marekani, Jumanne usiku, Pochettino alitoa kauli iliyoashiria nia yake ya kuibadilisha sura ya soka la Manchester, akiahidi kupambana na ubabe wa Manchester City.
Baada ya Marekani kuifunga Haiti mabao 2-0 katika mchezo wake wa mwisho jijini Cincinnati, Pochettino alikabiliwa na swali la mmoja wa waandishi wa habari aliyedai kuwa Manchester ni ya rangi ya bluu na itaendelea kuwa hivyo, akimaanisha Manchester City.
Kocha huyo alitikisa kichwa na kujibu: "Hapana kabisa. Mtaona. Nipeni muda, nipeni muda, halafu hilo litabadilika."
Kauli hiyo imeongeza hamasa miongoni mwa mashabiki wa United wanaosubiri kuona namna atakavyoanza kazi ya kuirejesha timu hiyo kwenye ushindani.
AAGANA NA MAREKANI KWA HISIA
Kabla ya kuanza safari yake mpya England, Pochettino aliandika ujumbe wa kuaga timu ya taifa ya Marekani, akieleza namna alivyothamini miaka miwili aliyokuwa akiiongoza timu hiyo.
Kocha huyo alikiri kuwa haikuwa rahisi kuachana na wachezaji, benchi la ufundi na mashabiki ambao alikuwa amejenga nao uhusiano wa karibu.
Amesema uzoefu wake nchini Marekani umempa mambo mengi mazuri katika maisha ya soka na binafsi, huku akitaja safari ya timu hiyo katika mashindano ya Gold Cup na kufuzu nusu fainali ya Nations League kuwa miongoni mwa kumbukumbu muhimu.
Pochettino pia aligusia wimbo wa Country Roads wa John Denver, ambao hupigwa kabla ya michezo kuanza katika Uwanja wa Old Trafford, akisema kila atakapousikia atawakumbuka watu wa Marekani kwa tabasamu.
Awali, kocha huyo alishindwa kuzuia hisia zake wakati wa mkutano na waandishi wa habari, akieleza kuwa uamuzi wa kuondoka Marekani na kujiunga na Manchester United ulikuwa miongoni mwa maamuzi magumu zaidi katika maisha yake ya ukocha.
"Hakuna nafasi nyingi zinazojitokeza katika maisha ya ukocha za kuifundisha klabu kubwa kama Manchester United. Ni vigumu kukataa fursa kama hiyo inapokuja," amesema.
MAANDALIZI YA LIVERPOOL YAANZA
Pochettino anatarajiwa kuanza mara moja maandalizi ya mchezo wake dhidi ya Liverpool utakaopigwa Jumapili kwenye Uwanja wa Anfield.
Kuwasili kwake mapema kunampa nafasi ya kukutana na wachezaji wanaorejea kutoka kwenye majukumu ya timu zao za taifa na kuanza kuweka mikakati ya mchezo huo.
Taarifa zinaeleza kuwa Manchester United imelipa takribani pauni milioni 10 ili kumwondoa Pochettino na benchi lake la ufundi katika majukumu yao ya timu ya taifa ya Marekani, licha ya kocha huyo kuwa amesaini mkataba mpya baada ya Kombe la Dunia la majira ya kiangazi.
Sasa macho ya mashabiki wa United yataelekezwa kwa kocha huyo mpya, wakisubiri kuona kama ataweza kutimiza ahadi yake ya kurejesha furaha, ushindani na mafanikio Old Trafford.