Nyota wa kuchunga kundi la Serengeti Boys
Muktasari:
- Serengeti Boys imepangwa Kundi I pamoja na Brazil, Ireland na Costa Rica, mataifa ambayo yanaingia kwenye mashindano hayo yakiwa na vijana waliokwishaonyesha uwezo wao kupitia mashindano ya kufuzu na rekodi za mashindano yaliyopita.
WAKATI Timu ya Taifa ya vijana chini ya miaka 17, Serengeti Boys, ikiendelea na maandalizi ya Fainali za Kombe la Dunia zitakazofanyika Qatar, kuna majina ya wachezaji kutoka kwa wapinzani wake ambayo yanapaswa kupewa uzito na benchi la ufundi.
Serengeti Boys imepangwa Kundi I pamoja na Brazil, Ireland na Costa Rica, mataifa ambayo yanaingia kwenye mashindano hayo yakiwa na vijana waliokwishaonyesha uwezo wao kupitia mashindano ya kufuzu na rekodi za mashindano yaliyopita.
Katika kundi hilo, Brazil ina silaha ya winga Eduardo Conceicao, Ireland inamtegemea kiungo mshambuliaji Ryan Sheridan, wakati Costa Rica ina washambuliaji Akenai Samuels na Paul Gonzalez ambao walikuwa na mchango mkubwa katika mabao ya timu hiyo wakati wa kufuzu.
EDUARDO CONCEICAO (BRAZIL)
Ni jina ambalo safu ya mabeki ya Serengeti Boys inapaswa kuliweka kwenye orodha ya wachezaji wa kumfuatilia kwa karibu kutokana na uwezo wake wa kucheza pembeni, kupenya kwa chenga na kufanya uamuzi ya haraka anapokaribia lango.
Winga huyo wa akademi ya Palmeiras ni miongoni mwa vipaji vinavyopewa nafasi kubwa katika kikosi cha Brazil, ambacho kina historia kubwa kwenye mashindano hayo baada ya kushiriki mara 19 kabla ya toleo hili na kutwaa ubingwa mara nne, mwaka 1997, 1999, 2003 na 2019.
Conceicao tayari ameonyesha uwezo wake kwenye mashindano ya kufuzu ya Amerika Kusini, akifunga bao katika ushindi wa Brazil wa 3-0 dhidi ya Argentina, Aprili 10, 2026.
Mbali na Conceicao, Brazil ina vijana wengine kutoka akademi zenye majina makubwa, akiwemo Kau Furquim wa Bahia, Joao Franca wa Palmeiras na Riquelme Henrique wa Atletico Mineiro.
RYAN SHERIDAN (IRELAND)
Kama kuna mchezaji ambaye Serengeti Boys inapaswa kumfuatilia katika eneo la kiungo, basi ni Ryan Sheridan wa St Patrick’s Athletic inayoshiriki Ligi Kuu ya Ireland, ambaye ana uwezo wa kucheza nyuma ya washambuliaji na kuanzisha mashambulizi.
Sheridan alionyesha umuhimu wake katika hatua ya kufuzu ya UEFA, ambako alifunga mabao mawili katika michezo mitatu ya hatua ya mwisho iliyoiwezesha Ireland kupata tiketi ya kucheza Kombe la Dunia.
Bao lake la kwanza alilifunga Machi 25, 2026, katika ushindi wa 3-0 dhidi ya Poland, kabla ya kuongeza jingine Machi 31, wakati Ireland ilipoichapa Slovakia mabao 7-0 na kuthibitisha nafasi yake ya kushiriki Qatar.
Mchezaji mwingine wa kuangaliwa ni Josh O’Dwyer wa Red Bull Salzburg, kiungo mwenye uwezo wa kusaidia timu kujenga mashambulizi kutoka eneo la kati.
Ireland pia ina faida ya kuwa na wachezaji wawili waliokuwapo kwenye kikosi kilichoshiriki Kombe la Dunia mwaka 2025, kipa George Moloney na beki Sean Spaight, ambao wana uzoefu wa mashindano hayo.
COSTA RICA
Kama kuna timu ambayo Tanzania inapaswa kuwa makini nayo kwenye eneo la ushambuliaji, basi ni Costa Rica, ambayo ilionyesha uwezo makubwa katika mashindano ya kufuzu ya Concacaf.
Miongoni mwa majina yanayopaswa kupewa uangalizi ni Akenai Samuels, mshambuliaji wa Alajuelense ambaye alikuwa na takwimu zinazovutia katika mashindano hayo.
Samuels alifunga mabao sita na kutoa asisti sita ndani ya dakika 225 alizocheza. Kwa maana nyingine, alihusika moja kwa moja katika mabao 12, wastani wa kuhusika kwenye bao kila baada ya dakika 18.
Takwimu hizo zinamfanya kuwa mmoja wa wachezaji hatari zaidi ambao Serengeti Boys inapaswa kuwafuatilia, hasa kutokana na uwezo wake wa kufunga na kutengeneza nafasi kwa wenzake.
Mbali na Samuels Paul Gonzalez naye alikuwa na mchango mkubwa kwenye mashindano hayo baada ya kufunga mabao sita na kutoa asisti moja.
Kwa ujumla, wawili hao walihusika katika mabao 19 kati ya 35 ambayo Costa Rica ilifunga kwenye mashindano ya kufuzu, ikiwa ni idadi kubwa kuliko timu nyingine zote zilizoshiriki mchujo huo.
Costa Rica pia ina Thiago Cordero, beki wa Saprissa, ambaye ana uzoefu wa kucheza Kombe la Dunia U-17 mwaka 2025 na kufunga bao dhidi ya Croatia. Anaungana na Adrián Espinoza na Bryan Calderón katika kundi la wachezaji wenye uzoefu wa mashindano ya kimataifa.
NYOTA WENGINE EBRIMA TUNKARA (HISPANIA)
Tunkara ni mmoja wa vijana wanaotajwa kuwa na uwezo mkubwa katika mashindano hayo kutokana na mafanikio aliyopata akiwa na umri wa miaka 16.
Kiungo mshambuliaji huyo wa Hispania alichaguliwa kuwa mchezaji bora wa mashindano ya vijana chini ya miaka 17 ya Ulaya yaliyofanyika mwaka huu.
IBRAHIM RABBAJ (MOROCCO)
Rabbaj ni kijana anayekipiga katika akademi ya Chelsea ambaye awali aliwahi kuiwakilisha England katika timu za vijana kabla ya kuamua kuitumikia Morocco.
Alijiunga na mfumo wa timu za taifa za Morocco mwaka 2026 na tangu wakati huo ameendelea kuonyesha kiwango kizuri katika kikosi cha vijana chini ya miaka 17.
Anacheza nafasi ya winga wa kulia na uwezo wake wa kupenya kwa chenga umekuwa ukilinganishwa na ule wa Lionel Messi.
BOYS INAHITAJI KUWA MAKINI
Takwimu za wachezaji hao zinaonyesha aina tofauti za changamoto ambazo Serengeti Boys inapaswa kujiandaa nazo katika Kundi I.
Brazil ina Conceicao mwenye uwezo wa kupenya kwa chenga na kufunga, Ireland ina Sheridan ambaye alifunga mabao mawili katika hatua ya mwisho ya kufuzu, huku Costa Rica ikiwa na Samuels na Gonzalez ambao kwa pamoja walihusika katika mabao 19.
Kwa hiyo, kazi ya Serengeti Boys haitakuwa kusubiri wapinzani wafike kwenye lango lake, bali kuhakikisha inaziba mapema mianya inayowapa nafasi nyota hao kutumia uwezo wao.