Kipute Kombe la Dunia U-17 Kinaanza
Muktasari:
- Mechi saba zitapigwa leo ikiwemo ile ya Uganda dhidi ya Korea Kusini ambayo imepangwa kundi B itakayopigwa saa 10:30 jioni Uwanja wa Aspire Zone, Al Rayyan.
PAZIA la kumtafuta bingwa mpya wa mashindano ya Kombe la Dunia kwa vijana chini ya miaka 17, litafunguliwa leo Novemba 19 hadi Desemba 13, 2026 yatakapohitimishwa nchini Qatar.
Mechi saba zitapigwa leo ikiwemo ile ya Uganda dhidi ya Korea Kusini ambayo imepangwa kundi B itakayopigwa saa 10:30 jioni Uwanja wa Aspire Zone, Al Rayyan.
New Caledonia itapigwa dhidi ya Ecuador (Kundi B), Ufaransa dhidi ya Haiti (Kundi D), Korea Kusini dhidi ya Uganda (Kundi B), Saudi Arabia dhidi ya Uruguay (Kundi D), Msumbiji dhidi ya Denmark (Kundi C), Qatar dhidi ya Panama (Kundi A), Misri dhidi ya Ugiriki (Kundi A) na Argentina dhidi ya Australia (Kundi C).
Mchezo wa Qatar na Panama ndio utakaofungua rasmi mashindano hayo, huku wenyeji wakianza kampeni yao mbele ya mashabiki wao ambao wanatarajiwa kuhudhuria kwa wingi.
Miongoni mwa michezo inayovutia ni Saudi Arabia dhidi ya Uruguay, pambano linalokutanisha soka la Asia na taifa lenye historia kubwa ya kukuza vipaji Amerika Kusini. Pia, Argentina dhidi ya Australia itakuwa kipimo kwa vijana wa mataifa hayo, wakati Uganda itakuwa na kazi ya kuonyesha ubora wake dhidi ya Korea Kusini.
Tanzania iliyopangwa kundi I ikiwa inashiriki kwa mara ya kwanza mashindano hayo itacheza Jumamosi Novemba 21 kwa mchezo dhidi ya Costa Rica saa 10 jioni kabla ya kukutana na Brazil Novemba 24 saa 12 jioni kisha kumalizana na Ireland Novemba 27 saa 11 jioni.
Brazil ndiyo timu yenye rekodi kubwa zaidi katika kundi hilo ikiwa imetwaa mataji manne ya dunia ya vijana, lakini kwa Tanzania mchezo wa kwanza ni muhimu katika kujenga nafasi ya kusonga mbele. Kila pointi itakuwa na thamani katika kundi hilo lenye ushindani.
Hii ni fainali ya 21 tangu mashindano hayo yaanzishwe mwaka 1985, lakini pia ni sehemu ya historia mpya ya michuano hiyo, ambayo kwa mara ya pili mfululizo inashirikisha timu 48 badala ya mfumo wa zamani wa timu 24. Jumla ya mechi 104 zitachezwa katika makundi 12, kila kundi likiwa na timu nne
Qatar inaandaa mashindano haya kwa mwaka wa pili mfululizo, baada ya FIFA kuamua nchi hiyo kuwa mwenyeji wa matoleo ya kila mwaka kuanzia 2025 hadi 2029. Mechi zote zikipangwa zitafanyika katika viwanja vya Aspire Zone, huku fainali ikipangwa kuchezwa Desemba 13 katika Uwanja wa Ahmad Bin Ali.
Mashindano hayo yamekuwa daraja muhimu kuwakuza nyota mbalimbali kama Ronaldinho, Cesc Fabregas, Toni Kroos na Phil Foden ni miongoni mwa majina yaliyowahi kupitia michuano hiyo kabla ya kuwa mastaa wa kimataifa. Nigeria ndiyo taifa lenye mafanikio makubwa zaidi likiwa na mataji matano, ikifuatiwa na Brazil yenye manne, huku Ghana ikiwa imetwaa mawili.
Ureno ndiyo bingwa mtetezi baada ya kutwaa taji hilo mwaka 2025, hivyo itakuwa na jukumu la kulinda heshima yake dhidi ya mataifa mengine yanayotafuta nafasi ya kuandika historia. Katika miaka iliyopita, mataifa kama Ufaransa, Mexico, Uswisi, England na Ujerumani pia yamewahi kutwaa ubingwa huo, jambo linaloonyesha namna ushindani ulivyoenea katika mabara tofauti.
Afrika itakuwa na uwakilishi wa mataifa 10, yakiwamo Tanzania, Uganda, Msumbiji, Misri, Algeria, Cameroon, Ivory Coast, Mali, Morocco na Senegal. Mbali na Tanzania, mataifa mengine yatakayoshiriki kwa mara ya kwanza ni Ugiriki, Montenegro, Msumbiji, Romania, Serbia, Vietnam na Jamhuri ya Dominika. Hiyo inaifanya fainali hii kuwa nafasi ya mataifa mapya kujipima dhidi ya vigogo wa soka la vijana.