Pete maalum kwa mabingwa Kombe La Dunia
Muktasari:
- Wazo hilo limechukuliwa kutoka kwenye utamaduni maarufu wa michezo ya ligi kuu za Amerika Kaskazini kama vile NBA na NFL, ikiwa ni sehemu ya kuongeza nakshi na kumbukumbu ya kipekee kwenye mashindano hayo makubwa zaidi duniani.
ATLANTA, MAREKANI: SHIRIKISHO la Soka la Kimataifa (FIFA), limethibitisha kuwa washindi wa Kombe la Dunia 2026 watatunukiwa pete maalumu za ubingwa (Championship Rings) kwa mara ya kwanza katika historia ya michuano hiyo.
Wazo hilo limechukuliwa kutoka kwenye utamaduni maarufu wa michezo ya ligi kuu za Amerika Kaskazini kama vile NBA na NFL, ikiwa ni sehemu ya kuongeza nakshi na kumbukumbu ya kipekee kwenye mashindano hayo makubwa zaidi duniani.
Kulingana na taarifa rasmi iliyotolewa na chombo cha habari cha The Daily Star pamoja na mtandao wa The Straits Times, jumla ya pete 2,026 pekee ndizo zilizotengenezwa ili kuendana na mwaka wa mashindano hayo.
Kati ya hizo, pete 30 za kipekee zimetengwa kwa ajili ya wachezaji na benchi la ufundi la timu itakayotwaa ubingwa, ambapo upande mmoja utakuwa na nembo ya Kombe la Dunia na upande mwingine utawekwa utambulisho wa nchi bingwa.
Kwa upande wa mashabiki na wakusanyaji wa kumbukumbu duniani kote, mtandao rasmi wa FIFA umefafanua kuwa pete 1,996 zitakazobaki zitauzwa kama bidhaa halisi zilizoidhinishwa na shirikisho hilo.
Kila pete itakayouzwa itakuwa na namba yake maalum ya utambulisho pamoja na cheti cha uhakiki ili kumfanya shabiki anayeimiliki kuwa na sehemu ya historia ya kipekee ya fainali hiyo itakayopigwa katika uwanja wa New York New Jersey Stadium.